Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tunapaswa kuthamini mchango wa wanawake katika jamii

815ba644e3e64ac77829c0536946f716 Tunapaswa kuthamini mchango wa wanawake katika jamii

Mon, 8 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MACHI 8, kila mwaka ni siku ya kimataifa ya kutambua nafasi na mchango wa wanawake katika kuchangia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa duniani.

Siku hii inatukumbusha matokeo chanya ya kisiasa, kijamii na kiuchumi waliyofikia wanawake na inatutaka kutafakari juu ya matokeo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi waliyofikia wanawake na msimamo wao imara katika ngazi ya kijamii kwa ujumla.

Lakini licha ya jitihada na msimamo wao bado changamoto ni kubwa katika mantiki za usawa. Katika maadhimisho ya siku hii muhimu, kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Wanawake katika uongozi: Chachu kufikia dunia yenye usawa.”

Umoja wa Mataifa (UN) uliridhia na kuanza kuadhimisha rasmi Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8, 1975 kwa lengo la kuikumbusha dunia juu ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia.

Uamuzi huu ulifikiwa ili kupingana na mfumo dume ambao ulitamalaki katika jamii mbalimbali duniani na kuminya haki za wanawake. Katika kuunga mkono siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anasema kutokuwepo na usawa wa kijinsia na ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana ni ukatili unaopaswa kushughulikiwa sasa na si wakati mwingine wowote.

Katibu Mkuu Guterres anahimiza kwamba ushirikishwaji wa wanawake ni muhimu sana kwa ajili ya kuhakikisha utulivu, kusaidia kuzuia migogoro na kuchagiza maendeleo endelevu na maendeleo jumuishi, kwani usawa wa kijinsia ni kigezo cha kuwa na dunia bora.

Anasema hili si suala jipya na anatolea mfano wa jinsi ambavyo wanawake wamekuwa wakipigania haki zao kwa miongo kadhaa na kwamba miaka 500 iliyopita Malkia Nzinga Mbandi wa Mbundu alipigana vita dhidi ya utawala wa kikoloni wa Kireno katika nchi ambyo leo inaojulikana kama Angola.

Pia mwanaharakati wa haki za wanawake, Mary Wollstonecraft, ambaye aliandika uthibitisho wa Haki za Wanawake mnamo 1792, mara nyingi huonekana kama mwanaharakati wa wanawake wa nchi za Magharibi.

Na miaka 60 baadaye Sojourner Truth aliwasilisha ombi kwa ajili ya haki za wanawake wakati akifanya kila awezalo kukomesha utumwa. Pia, baada ya kufahamu muhimu wa kutatua shida zinazoharibu na kuchafua kizazi chetu, na kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia na upatanishi hadi mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, wanawake na wasichana wa kizazi hiki, kwa muda mrefu, wamekuwa viongozi na wanaharakati wa mazingira.

Mfano mzuri ni Wangari Maathai na Jane Goodall. Katika uwakilishi wa kisiasa, ushiriki wa wanawake katika mabunge kote duniani umeongezeka maradufu katika miaka 25 iliyopita.

Lakini uwakilishi wa wanawake katika serikali si juu ya “masuala ya wanawake tu” kama ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia au kuchagiza utunzaji wa watoto.

Wanawake kwenye serikali huleta maendeleo ya kijamii na mabadiliko halisi katika maisha ya watu. Wanawake wana uwezekano mkubwa wa kutetea uwekezaji katika elimu na afya; na kuleta muafaka katika vyama na masuala ya kawaida.

Na ili kutimiza malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), usawa wa kijinsia ni lengo lenye ufunguo wa kufanikisha malengo mengine 16. Katika hotuba ya Katibu Mkuu Guterres kwenye Chuo Kikuu cha New School mjini New York Marekani mwaka jana, Guterres alisema kila mahali wanawake wako katika hali mbaya zaidi ya wanaume kwa sababu tu ni wanawake, na kwamba, kama ilivyokuwa utumwa na ukoloni katika karne iliyopita pengo la usawa kwa wanawake linapaswa kutuaibisha sote katika karne ya 21.

“Sababu si tu kwamba haukubaliki bali ni upumbavu. Ni kwa kupitia tu ushiriki ulio sawa wa wanawake ndiyo tutaweza kufaidika na tunaweza kufaidika na akili, uzoefu na ufahamu wa wanadamu wote,” anasema Guterres.

Katika karne ya 21 vuguvugu la haki za wanawake limeshika kasi huku wanawake walioshikilia nyadhifa za ukuu wa nchi wakifuta shaka na shuku zote kuhusu uwezo wa wanawake wa kuongoza, hata hivyo, bado kuna mtihani mkubwa katika haki za wanawake.

Kutokuwepo na usawa na ubaguzi imekuwa mazoea kila mahali, hatua zimedorora kila mahali na katika baadhi ya sehemu zimebadilika na kuna msukumo mkubwa wa kuzirudisha nyuma haki za wanawake.

Ukatili dhidi ya wanawake ikiwemo mauaji umefikia kiwango cha kutisha, takwimu za dunia zinabainisha kuwa zaidi ya mwanamke mmoja kati ya watatu anakabiliana na ukatili wa aina fulani katika maisha yake.

Ulinzi wa kisheria dhidi ya ubakaji na ukatili majumbani imekuwa kama kitu cha kawaida kwenye jamii zetu. Hata ubakaji ndani ya ndoa bado unaendelea kuhalalishwa katika nchi 34, na haki za wanawake za afya ya uzazi ziko katika tishio kubwa kutoka kila upande.

Katibu Mkuu Guterres anabainisha kuwa wanawake ni viongozi mashuhuri katika jamii lakini wanakabiliwa na udhalilishwaji, vitisho na ukatili, mtandaoni na nje ya mtandao.

Anaongeza kwamba si jambo la kushangaza kwa mamilioni ya wanawake na wasichana kufuatiliwa kuhusu uhuru wao binafsi, kuanzia kwenye serikali hadi kwenye kampuni.

Sera za kuwakandamiza na kuwaadhibu wanawake zinarejea kwa kishindo huku mijadala ya amani ikiendelea kuwatenga miaka 20 baada ya nchi zote kutoa ahadi ya kuwajumuisha.

Na zama hizi za kidijitali zinaweza kufanya pengo hilo la usawa kupanuka zaidi kwa kuwa tunaishi katika dunia iliyotawaliwa na mfumo dume na yenye utamaduni unaodhibitiwa na wanaume.

Katika suala la urithi mfumo dume umekuwa ukutoa upendeleo kwa wanaume na hadi sasa mfumo huu unaendelea kuathiri kila nyanja ya maisha yetu na wote tunabeba gharama zake.

Guterres anasisitiza kuwa pengo la usawa lililojificha limejengeka ndani ya taasisi na mifumo ambayo inaendesha maisha yetu lakini inatokana na mahitaji ya nusu tu ya watu wote na hili limesababisha pengo kubwa la takwimu duniani, mara nyingi wanawake hawahesabiwi na uzoefu wao haujumuishwi.

Guterres anasema athari zake ziko katika kila upande kuanzia huduma za vyoo hadi kwenye safari za mabasi na wako katika hatari kubwa ya kupata ajali kwani mikanda ya usalama hata kwenye magari imewekwa kwa kuwatosha wanaume.

Wanawake wako kwenye hatari ya kufa na shinikizo la damu kwani hata vifaa vya kupimia vilitengenezwa kwa minajili ya mahitaji ya wanaume. Athari hizi zilizosababishwa na mfumo dume na pengo la usawa unaenda mbali zaidi ya wanawake na wasichana.

Mwandishi wa vitabu Chimamanda Ngozi Adichie inabainisha anaposema: “Uanaume ni ngome ngumu ndogo na tunawaweka wavulana humo. Tunauelezea uwezo wa wanaume katika njia ambazo zinakuja na gharama kubwa kwa wanaume wenyewe.” Jambo moja ambalo wanaume wengi hawalijui pengine ni kwamba usawa wa kijinsia una faida kubwa kwa uhusiano wa jinsi hizi mbili.

Wanaume wanaoshiriki utunzaji na kutumia wakati mwingi na familia zao wana furaha zaidi, na wana watoto wenye furaha zaidi.

Kwa kiwango kikubwa, kubadilisha usawa wa mamlaka ni muhimu, si tu kama suala la haki za binadamu bali pia kwa maendeleo ya kibinafsi, afya na ustawi wa jamii.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari. 0685 666964 au bhiluka@ gmail.c

Columnist: www.habarileo.co.tz