Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tunalaani mauaji, vurugu kampeni za uchaguzi

77249c7f0445b11356045fa167698d5d Tunalaani mauaji, vurugu kampeni za uchaguzi

Tue, 29 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKATI kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge, wawakilishi na madiwani zikishika kasi nchini, kumejitokeza matukio mabaya na ya aibu ya vurugu na mauaji yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa.

Tukio la kwanza ni lile lililotokea Pemba, Zanzibar, ambako watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa chama kimoja walivamia msikiti alfajiri na kuwajeruhi kwa mapanga wafuasi wa CCM waliokuwa wakiswali ndani ya msikiti huo.

Tukio jingine la kusikitisha liliripotiwa kutokea Agosti, mwaka huu mkoani Songwe likihusisha kifo cha Briton Mollel anayedaiwa kuwa kada wa CCM ikihusisha ugomvi kati ya wafuasi wa CCM na wa Chadema.

Kama hiyo haitoshi, tukio jingine liliripotiwa kutokea Njombe ambako kumefanyika mauaji ya kiongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Emmanuel Mlelwa.

Tunafarijika kusikia kuwa, baadhi ya watu wameshakamatwa kuhusiana na matukio hayo.

Ukiangalia kwa undani dalili zinaonesha, kwa kiasi kikubwa matukio haya yanapangwa au kuchochewa na baadhi ya wagombea na vyama vyao ili kuudhofisha upande mwingine au kujitengenezea urahisi wa kushinda kwa gharama ya maisha ya watu wengine.

Tukiwa sehemu ya jamii, tunalaani vikali matukio haya, kwani yanakwenda kinyume cha utamaduni, hulka na silka za Watanzania walio wastaarabu, wenye upendo, wenye kujali utu, kusaidiana na kuheshimiana bila kujali tofauti zao za aina yoyote.

Uchaguzi usitumike kuwagawa Watanzania, bali uwe njia wa kuwawezesha kuwachagua viongozi wao wanaowataka kwa kuzingatia utashi wao na bila vitisho.

Tunawataka wagombea na vyama vyao kuepuka kutoa kauli zinaweza kuhamasisha wananchi kuchukua sheria mkononi kama ilivyotokea katika matukio hayo tuliyoyaeleza hapo juu.

Tunasema hivyo kwasababu zimekuwa zikisikika kauli zisizo za kiungwana za baadhi ya wagombea wakihamasisha wafuasi wao kujitayarisha kwa silaha ikiwamo mapanga na marungu kwa kile wanachodai hawatendewi haki.

Aidha, baadhi ya wagombea wamekuwa wakisikika wakisema uchaguzi huu ni wa kufa au kupona kwao, kwamba hawatakuwa tayari kutangazwa wameshindwa wakiwaaminisha wafuasi wao kuwa wataibiwa kura.

Tunalaani vikali kauli hizo za wanasiasa kwasababu mara nyingi ndio zimekuwa zikichochea matukio ya vurugu na hata mauaji ya watu wasio na hatia kwa kisingizio cha siasa.

Wagombea ni lazima watambue kuwa uchaguzi unaendeshwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ambazo vyama vyao vimezikubali na kutia saini, hivyo wanapaswa kuzizingatia ipasavyo ili uchaguzi ufanyike na kumalizika kwa amani.

Tunatoa rai kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutofumbia macho wagombea wanaotoa lugha za uchochezi na kuchonganisha wananchi kwa kutumia tofauti za kiitikadi za kisiasa.

Aidha, tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuwatafuta popote walipo na kuwatia mbaroni wote waliohusika na matukio haya bila kuangalia sura, wawe wagombea, viongozi wa vyama ama wafuasi wao, na kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake iwe fundisho kwa wengine

Columnist: habarileo.co.tz