Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tumuunge mkono Rais Samia kwa kuchapa kazi 

12649eb5f2f25b227bb48ca504655e43 Tumuunge mkono Rais Samia kwa kuchapa kazi 

Tue, 29 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS Samia Suluhu Hassan ametimiza siku 100 tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 19, mwaka huu.

Rais Samia ameapishwa kuwa Rais kutokana na kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu kutokana na matatizo ya moyo.

Kipindi cha siku 100 katika utawala kinatumika kupima mwelekeo, utashi, maono na mwelekeo wa kiongozi katika siku zake za mwanzo za uongozi wake.

Katika kipindi cha siku 100 ambazo Rais Samia amekuwa madarakani, ameonesha uwezo mkubwa wa kiuongozi, ameonesha dira ya wapi Tanzania inaelekea na amefungua milango kwa kila Mtanzania kushiriki katika ujenzi wa taifa.

Wakati tukimpongeza Rais Samia kwa mwanzo mzuri aliouonesha, rai yetu kwa Watanzania wote sasa ni kuungana na Rais wetu kuchapa kazi kwa bidii na maarifa ili tuweze kulijenga kwa kasi taifa letu lenye changamoto nyingi.

Watanzania wote kila mmoja wetu kwa nafasi yake, aliweke taifa letu mbele na maslahi ya taifa kwa kuchapa kazi kwa moyo wa ufanisi yaani, juhudi na maarifa.

Bila kujali tofauti zetu za itikadi za siasa, dini wala makabila, tushirikiane na Rais Samia kupitia kwake mwenyewe na wasaidizi wake katika vita ya kupambana na ufisadi, rushwa, uzembe, ubadhirifu, umasikini, ujinga na maradhi.

Aidha, tunatoa rai kwa viongozi wa umma wakiwemo mawaziri na wa vyama vya siasa kushirikiana vyema na Rais Samia ili kuwahudumia wananchi sawia na bila mikwaruzano.

Tunawasihi wanasiasa wetu wakati wote waongozwe na busara na utulivu ili Tanzania iendelee kudumisha mshikamano, amani na utulivu wakati wote na pale inapobidi kukosoana, basi iwe kwa hoja, staha na kwa kuheshimiana na kwa kuzingatia sheria za nchi na maadili ya Kiafrika na na hasa, maadili ya Kitanzania.

Tunawasihi wananchi wote bila ya kujali tofauti zao za itikadi za kisiasa kudumisha umoja, amani na upendo miongoni mwao na kushirikiana vyema na serikali ili kuijenga Tanzania yenye uchumi imara kwa manufaa yao na vizazi vijavyo chini ya jemadari Rais Samia.

Umoja, utulivu na amani uendelee kuwa msingi na ngao imara katika kuipaisha Tanzania kiuchumi na kuwa mahali bora na salama pa kuishi kwa kila mmoja.

Ndiyo maana tunazidi kusema: “Tumuunge mkono Rais

Samia kwa kuchapa kazi kwa moyo wa ufanisi, uaminifu na uadilifu katika maisha yetu.”

Columnist: www.habarileo.co.tz