Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tumuunge mkono JPM, tumwamini Mkemia Mkuu

1dadbe10fa87064b664642408bd76b73 Tumuunge mkono JPM, tumwamini Mkemia Mkuu

Wed, 10 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MOJA ya madhumuni ya ya CCM yaliyochukuliwa kutoka chama kilichopigania uhuru cha TANU ni kuona Serikali inatumia mali yote ya nchi yetu kuondosha umaskini; ujinga na maradhi.

Hii pia inajidhihirisha katika hotuba ya kwanza ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya mwaka 1961 baada ya kuwa waziri mkuu wa Tanganyika. Na kimsingi katika kipindi chote alisistiza kwamba watanzania wanao maadui watatu kama walivokwisha kutajwa.

Katika Makala yangu ya leo nitapenda kujikita katika adui mmoja tu ‘maradhi’. Siyo kwamba adui umaskini ameondoka katika taifa letu la! Hasha ila tu angalau sasa nchi imeingia uchumi wa kati.

Kama ni mwanga umeanza kuonekana. Naye adui ujinga kwa kiasi kikubwa amepungua sana. Kwa sasa tunazungumzia elimu bure ambapo watoto wengi wanapata nafasi ya kwendaa shule kufuta adui ujinga.

Ni wazi kwamba idadi ya vyuo imezidi kuongezeka huku wasomi kutoka vyuoni humo wakizidi kuongezeka kila kukicha. Adui maradhi aambaye tunamjadili katika makala haya anazidi kusumbua katika taifa letu hasa katika kipindi hiki ambacho ulimwengu unahangaika kukabiliana na janga la COVID-19.

Kwa nyakati tofauti tumewasikia viongozi wa kiserikali wakitoa wito kwa watanzania kujihadhari na gonjwa hili kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa afya. Tangu kuingia kwa gonjwa hili, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi chache sana duniani ambayo haikuruhusu kufungia wananchi wake majumbani kwa kuwa kufanya hivyo ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kwenda kila wanapotaka.

Lakini pia ingeongeza ugumu wa maisha kwa watanzania walio wengi hasa wanaotegemea kazi ndogondogo katika kuwaingizia kipato cha kila siku. Kwa msisitizo kabisa Rais wa Magufuli amewasisitiza watanzania kutumia njia za asili katika kukabiliana na gonjwa hili, kitu ambacho kilizaa matunda kwa kiasi kikubwa. Njia za kufukiza na kunywa dawa za asili zilisaidia sana kukabiliana na janga hili.

Kitendo hiki cha Rais kuwatia nguvu na moyo watanzania kilisaidia sana kwani mwitikio ulikuwa mzuri kwa watanzania wote. Cha kushangaza katika siku za hivi karibuni kumeibuka uvumi mpya wa kwamba kuna kirusi cha COVID-19 sehemu ya pili ambayo ni mbaya zaidi kuliko ya kwanza. Uvumi huu unakuja kipindi ambacho mataifa ya Ulaya na Marekani yanajigamba kuwa yamepata chanjo ya kupambana na kirusi hiki cha Covid-19.

Ni chanjo hizi hizi ambazo hapo awali walitaka kuja kuzifanyia majaribio katika bara la Afrika, kana kwamba waafrika ni sehemu ya majaribio ya wazungu, hizi ni dharau sana kwetu waafrika.

Wakati chanjo hizo zinaendelea kutoka na kimsingi hazijaonyesha kuwasaidia wagonjwa naweza kusema, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linaoneonekana kuzikubali chanjo hizo sijui kwa vile zimetengenezwa na wazungu?

Maana tangu awali mataifa ya Afrika yalitangaza kuwa na dawa za asili za kutibu ugonjwa huu lakini WHO lilizitupilia mbali nafikiri kwa vile zimetengenezewa Afrika! Ingawa kiongozi mkuu kabisa wa WHO ni mwafrika lakini ninaanza kutilia shaka uafrika wake. Iweje adharau asili yetu kama waafrika?

Kwa nini ionekane dawa zinazotoka Afrika asizitilie maanani? Wakati wanajigamba kupata chanjo ya Covid-19, ugonjwa ambao umeibuka mwishoni mwaka 2019 na kushamiri 2020 wameshindwa kutengenea chanjo ya malaria hadi sasa, ugonjwa ambao unaua watu wengi.

Gonjwa la Ukimwi pia wameshindwa kulipatia chanjo pamoja na kugundulika ulimwenguni kwa takribani zaidi ya miaka 50 sasa! Kama wameshindwa kupata tiba ya haya wamewezaje kwa kipindi kifupi kupata dawa ya Covid-19? Je, inawezekana ni sehemu ya mpango mkubwa uliobuniwa miaka mingi ya nyuma kwa ajili ya kufanya biashara kwa mataifa masikini ya kiafrika na mengineyo duniani?

Je, inawezekana wanaodai kutengeneza chanjo hizi walishiriki kusambaza kirusi hiki? Kwa nini waaminishe ulimwengu wote kwamba wao ndo watengeneza dawa pekee na kwamba bila kuchanjwa watu wengi watakufa?

Mbona wao wamechanjwa lakini wanazidi kufa na kufungiana ndani kunaendelea? Nilifurahishwa na maneno ya Rais Magufuli aliyoyatoa hivi karibuni katika hotuba yake alipokuwa akizindua majengo ya magereza huko Dodoma aliposema: “Kamwe msifikirie kila dawa inayotoka nje ni kwa ajili yenu, ingekuwa hivyo malaria yangekuwa yameisha… kuna dawa nyingi ambazo ni nzuri za kujifukiza na za kunywa kama vile Covidal n.k. zile zinafanya kazi zimethibitishwa na Mkemia Mkuu, zinatibu virusi na bakteria kwa asilimia 99.9…

Watanzania tujitambue tusitumike kwenye biashara na wengine.” Kimsingi maneno haya yalinifariji sana hasa baada ya kuona kwamba Rais wangu aliona kile nilichokuwa nakiwaza toka mwanzo.

Viongozi wenye maono ya namna hii ni wachache sana duniani na sisi kama watanzania tumebahatika tu kumpata yatupasa kuungana naye katika kupambana na janga hili.

Ni wazi kwamba chanjo zinazohubiriwa sasa ni biashara tu ya matajiri wa ughaibuni. Kwa kuwa walifungiwa muda mrefu na mzunguko wa biashara umekuwa mdogo wametafuta njia ya kupumulia kwa kuumiza mataifa masikini.

Hivi ni nani aliyepitisha kuwa Shirika la Afya Duniani ndilo linaamua hatima ya taifa letu? Kama hatuwezi kumwamini Mkemia Mkuu wetu kama watanzania tutawezaje kumuamini mkemia wa Marekani ambaye hata hajali kama tunakufa au tunaishi?

Ni lini kama Watanzania na Waafrika kwa ujumla tutaacha kutumika katika michezo ya kijinga ya hawa mabeberu? Hadi sasa wametuachia gonjwa la ulibelari linatutesa kuzidi ugonjwa wowote ule! Kama kweli WHO lingekuwa linafanya kazi yake lingeshirikiana na shirika la chakula duniani kutatua bala la njaa ambalo huua wototo na wazee wengi kila siku.

Ama lingehakikisha kunapatikana dawa ya Ukimwi ambayo huua watu wengi kila siku badala yake wameleta dawa za kufubaza ili mtu augue tena aendelee kutumia dawa hizo huku wao wakinufaika kama biashara. Naamini umefika wakati wa waafrika kuacha kuchezewa afya zao kwa njia ya biashara.

Ni wazi kwamba Covid- 19 ni mafua kama yalivyo mafua mengine ingawa haya ni mapya. Kwa jamii za kiafrika ni mara nyingi sana tunaugua ugonjwa huu na huwa tunatumia dawa zetu za asili na tunapona kabisa. Sasa iweje leo tuje kutishiwa na wafanyabiashara hawa?

Kwa nini tuache kutumia dawa zetu za asili badala yake tunajawa na hofu kwa kitu ambacho kimeanza kutibiwa na mababu na mababu zetu? Kinachonisikitisha hivi sasa hata watabibu wameingiwa na hofu kiasi cha kufanya wasifanye kazi zao kwa weledi.

Unakuta mgonjwa anakuja kifua kimebana labda ni pumu, badala ya kumpatia huduma wote wanamkimbia hadi anafia pale hospitalini bila kupewa huduma! Huku ni kukosekana kwa uzalendo kabisa. Kwani lazima kumtibu mtu utumie madawa ya kibeberu?

Au ndo ile mmekwenda kusomea kugawa dawa zao tu? Nafikiri kuna umuhimu wa kukumbuka misingi ya kitabibu na kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli katika kukabiliana na janga hili.

Kuna baadhi ya watabibu wamefika hatua ya kutoa siri za wagonjwa pindi wakifariki na kuongeza taharuki kwa wananchi. Yaani mmewafanya wananchi wahisi kila mtu anayefariki dunia ni kwa sababu ya Covid-19, jambo ambalo siyo kweli kabisa. Kazi ya kwanza ya tabibu ni kuokoa maisha ya mgonjwa, ni vyema hili likazingatiwa katika utendaji.

Katika kipindi kama hiki ni vyema tukatumia maneno ya Hayati Baba wa taifa aliyoyatoa katika hotuba yake ya mwaka 1963, aliposema: ‘Ninapoulizwa kwa mfano, ni nini mwezi wa Machi kwa muda wa siku mbili tu, jibu langu ni moja, umoja. Wenzangu na mimi tulikuwa kitu kimoja. Na tulikuwa kitu kimoja kwa sababu Tanganyika (kwa sasa Tanzania) yenyewe ni kitu kimoja.

Na vile vile katika mambo yetu yote ya maisha ya taifa letu. Nani asiyejua kwamba msingi wa kufanikiwa kwa TANU, ni umoja wa TANU. Kadhalika katika vyama vya ushirika au vyama vya wafanyakazi wanachama wake wanaposhikana bega kwa bega, mambo yao yatawaendea vyema. Wanachama wake wakigombana na kutengana, mambo yao na mambo ya taifa zina yatakwenda tenge.

Ndugu zangu, huu si wakati wa kuchezea umoja wetu, tunauhitaji sasa kama tulivyohitaji zamani kwa ajili ya kuinua hali zetu na ndugu zetu’. Huu ndiyo wito wangu kwa kila mtanzania kuhakikisha anaunga jitihada za Rais Magufuli katika kukabiliana na janga hili la Covid-19 kwa kutumia dawa zilizokwisha thibitishwa na mkemia mkuu wa serikali.

Ikumbukwe kwamba hadi sasa serikali ya Tanzania imethibitisha takribani dawa tatu kupitia kwa mkemia mkuu wa serikali. Siyo lazima zitambuliwe na shirika WHO kwa kuwa siku zote watabaki kuwa vibaraka wa mabeberu.

Tuamke na kujitambua watanzania kwa kuwa hii vita ni yetu sote. Mungu mbariki Rais Magufuli, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika. Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni: +255-71224-6001 [email protected]

Columnist: habarileo.co.tz