Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tumuunge mkono JPM dhidi ya ‘ukoloni tiba’

19cc36364f854e732a3c47577b5844e7 Tumuunge mkono JPM dhidi ya ‘ukoloni tiba’

Thu, 25 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIKA kutembelea mitandao ya kijamii pamoja na kuzungumza na watu kadhaa, mintarafu suala zima la mlipuko wa pili wa ugonjwa wa corona na namna kapambana nao, nimekutana na makundi mawili ya Watanzania yenye mitazamo tofauti.

Kundi la kwanza ni la wale ambao wanaamini mapambano dhidi ya ugonjwa huu ni muhimu yafuate mtazamo, mbinu na maagizo ya mataifa ya Magharibi na kundi la pili ni lile linaloona kwamba mbinu ambazo tulitumia kuishinda corona mwaka jana ni mwafaka hata sasa.

Ingawa pia lipo kundi la wasio na msimamo, lakini kinachofurahisha ni kwamba wale wanaomini katika mbinu za 'kivyetu vyetu' zinazoongozwa na jemedari makini, msomi katika fani ya sayansi, Daktari John Magufuli, ndilo kundi kubwa la Watanzania.

Kundi hili bado halijatetereka sana licha ya propaganda kubwa zinazofanywa na mabeberu na vibaraka wao ili tuuvae mkenge kama baadhi ya majirani zetu.

Maagizo na matakwa ya mabeberu yamekuwa ni kututaka kuwasikiliza wao kwa kila kitu kama vile kujifungia ndani; kutumia dawa au chanjo kutoka kwao; kuvaa barakoa, tena siyo tujishonee sisi bali zinazotoka kwao; kunawa na kutumia vitakasa mikono kutoka kwao au kwa malighafi za kwao; kuwa na takwimu za wagonjwa kwa kuwapima kupitia vifaa wanavyotuuzia wao na pia kutomtegemea Mungu kwani inaonekana kama upuuzi hata kama wanaonekana kwenye nyumba za ibada!

Hata hivyo, wanaoamini katika nchi yetu kufuata maagizo hayo ya mabeberu, ni wachache migongoni mwao ambao bado wanaoamini katika

kujifungia ndani.

Tukumbuke kwamba linapokuja suala la nafasi ya Afrika katika uhusiano wa kimataifa, mabeberu bado yanalitazama bara hili kama soko lao, eneo la utafiti, na eneo la kupora rasilimali (mali ghafi). Waafrika tuna dhima sasa ya kubadili huu mtazamo.

Pamoja na ugonjwa huu kuwapiga sana wao na kuathiri vibaya uchumi wao, Wazungu wanapambana kuugeuza ugonjwa kuwa fursa kwa kupata soko la dawa zao kwetu kupitia hiki kinachoitwa mkopo au msaada wa kinga.

Kwa bahati mbaya na hasa kwa kuzingatia kwamba tumetawaliwa kiakili kwa muda mrefu (brainwashed), bado Waafrika wengi wakiwemo Watanzania wachache wanaamini kwamba cha kwetu si chema na hakifai isipokuwa kilichotoka Ulaya na kwamba hatuwezi kusimama kwa miguu yetu bila wao!

Kabla sijaangalia mambo mengine, nigusie hapa maandiko kuhusu nafasi ya Mwenyezi Mungu katika tiba. Nilivyomsikia Rais Magufuli ambaye ni Mkristu anavyoamini kuhusu nafasi ya Mungu katika tiba, ndivyo pia tunavyofundishwa sisi Waislamu. Kwamba kimsingi anayemtibu mtu yeyote anapoumwa ni Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba hizi dawa pamoja na madaktari ni sababu tu alizoziweka Mwenyezi Mungu katika mazingira yetu ya kibinadamu ili tupone.

Pengine nitaeleweka vizuri nikitolea mfano wa riziki. Mafundisho yanaonesha kwamba kabla mtu hujafariki dunia, riziki yako duniani aliyokupangia Mungu, huwa inakutafuta wewe. Lakini huwezi kukutana nayo (kuipata) kwa kulala tu nyumbani bali utaratibu aliotuwekea Mungu ni kufanya sababu ya kuipata hiyo riziki ambayo ni kufanya kazi.

Tukuridi kwenye dawa, maandiko yanasema kwamba Nabii Musa ambaye alikuwa mara kadhaa akizungumza na Mungu moja kwa moja, siku moja aliumwa, Mwenyezi Mungu akamwambia akachume mti fulani ndio dawa yake.

Musa akachuma majani ya mti huo na alipoyatumia akapona. Siku nyingine alipokumbwa na ugonjwa uleule akaenda tena kuuchuma ule mti lakini hakupona.

Akamgeukia tena Mungu kwamba mbona nimekunywa dawa ileile sijapona? Mwenyezi Mungu akamwambia kwamba kosa lake ni kutomtanguliza Mungu kwa kudhani dawa kama dawa ndiyo inayoponyesha na siyo kwa kuwezeshwa na mwenyewe aliyeumba dunia na vilivyomo.

Mafundisho pia yanasema kwamba Mungu ndiye amejaalia kuwepo kwa magonjwa kama mitihani anayotupima nayo lakini kwa kila ugonjwa ameumba pia dawa yake na hivyo anawawezesha wanadamu kugundua dawa hizo.

Na hii maana yake ni kwamba uwezo huo wa kutafiti na kugundua dawa hajawapa wazungu pekee bali Waafrika pia.

Pamoja na mbinu zote za kujikinga na corona tulizofanya Watanzania mwaka jana, kilichoonekana kama muujiza hadi taifa letu kutokuwa na corona, ilikuwa maombi na kumtegemea Mungu. Huwezi kuilezea hiyo hali kisayansi abadani, kubali usikubali.

Lakini kinachoonekana sasa ni Watanzania kujibweteka na kuacha kutomtegemea yeye licha ya kutukumbusha tena uwepo wake kwa kuwaondoa duniani wenzetu.

Katika kujadili suala hilo, napenda kumpongeza Mohamed Wage kwa andiko lake ambalo nimeliona kwenye mitandao ya kijamii alilolipa kichwa cha habari: Corona imewavua nguo Marekani, Uingereza na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Anasema mwezi Oktoba 2019, wiki moja kabla janga la corona kuanza kuitikisa dunia, taasisi mbili za John Hopkins Centre for Health Security na Nuclear Threat Initiative zilitoa kinachoitwa Global Health Security Index (GHSI) .

Watafiti hao wa GHSI walitathmini utayari wa nchi mbali mbali katika kupambana na magonjwa ya mlipuko kwa nchi 195 duniani na Marekani ikapewa namba moja katika utayari wa kupambana na magonjwa ya mlipuko kama corona na huku swahiba wake Uingereza ikipewa nafasi ya pili

Watafiti hao wakaipa nchi ya New Zealand nafasi ya 35 huku Vietnam ikipewa nafasi ya 50 katika orodha hiyo ya nchi 195. Tanzania ilikuwa ya 101.

Wakati corona imekita kila kona duniani na watu wanahangaika angalau kupata nafuu, zikaja tafiti mpya zinazoonyeaha kuwa New Zeeland na Vietnam ni katika nchi zikizoweza kupambana vizuri na mlipuko wa corona huku Marekani na Uingereza zikiwekwa chini kwa kushindwa kudhibiti maradhi haya na kusababisha vifo vya raia wake wengi.

Pengine tafiti hizo za sasa zingefanywa kwa uwazi zaidi na nafasi ya Mungu kuzingatiwa, bila shaka Tanzania ingekuwa juu zaidi.

Wage anasema watu wengi wanashindwa kujua kuwa ingawa corona ni tatizo la kiafya lakini pia lina sura ya siasa na utamaduni katika kulitafutia ufumbuzi wake.

Kwa mujibu wa Wage, mataifa haya yaliyofanikiwa katika mapambano haya kwa kiasi kikubwa yalizungatia pia dhana ya "Siasa na Utamaduni'" katika kutatua changamoto hii.

Kupitia nukta hii ya siasa na utamaduni, Rais John Magufuli ni kinara wa hili katika Afrika na ulimwenguni kwa ujumla, kamwe watanzania hatutakiwi kurudi nyuma katika kutumia tiba zetu za asili katika vita hii yenye maadui wengi.

Wage anasema vita ya kinachoitwa tiba ya maradhi imezungukwa na ujasiriamali na biashara ya makampuni makubwa ya dawa ya kimagharibi.

Wage anatutaka tutafute kitabu kinachoitwa 'Kill Shot: A shadow Industry, A Deadly Disease,' cha Jason Dearen ili kumwelewa vyema JPM na vita ya biashara ya makampuni makubwa ya dawa ya nchi za Mgharibi na athari zake.

Anasema ukikisoma kitabu hicho utajua kwa nini Tanzania inachafuliwa sasa baada ya kupinga chanjo hadharani na mengine wanayotutaka tufanya kupitia Amir Jeshi wetu Mkuu ambaye ameusoma mchezo huu mapema na kuelewa.

Kwa ufupi, Jason Dearen anaeleza kuhusu chanjo (Steroids Injection) ambayo mwaka 2012 ilijaribiwa kwa watu 800 nchini Marekani na baada ya muda zaidi ya watu 100 katika hao walipoteza maisha huku wengine wakipata dalili za magonjwa mengine hatari kama Fungal Menengetics n.k

Taasisi ya CDC ilipopewa kazi ya kuchunguza ndipo ilipogundulika hii ilikuwa ‘dili’ la kampuni moja kubwa ya dawa ya kifamilia na kisha jambo hilo likaenda mahakamani na baadae kupotea.

Kwa mujibu wa Wage, hii ni aina mpya ya ukoloni duniani ambayo hujulikana kama ‘ukoloni tiba’ ambao umedumu kwa miaka mingi dhidi ya nchi zinazoendelea na sasa umefikia hatua ya juu kabisa duniani. Tanzania umeishtukia mapema ukoloni huu na hakika tunatakiwa sana kuipongeza serikali ya JPM na nchi nyingine za Afrika zinapaswa kutuunga mkono.

“Ni kweli corona inaondoa wapendwa wetu na hakika inasikitisha, yatupasa kuchukua tahadhari kubwa huku tukijua tuko kwenye mapambano ya kulinda afya zetu na uchumi wetu,” anasisitiza Wage.

Kimsingi, kama anavyoamini Wage, mataifa ya Magharibi hayafurahi namna tunavyopambana na corona kama ambavyo yamechukizwa na namna New Zeeland na Vietnam walivyopambana na corona na kuibuka vinara.

Ni kwa mantiki hiyo, ni muhimu sana kwa Watanzania kutodharau hizi silaha mbili; tiba toka kwa wataalamu wetu wa ndani wakiemo wanaotupa tiba za asili na mbadala na kumtanguliza Mwenyezi Mungu. Cha kuzingatia, ili kuepuka utapeli na usalama wa mili yetu ni kuhakikisha kwamba dawa hizo zimethibitishwa na Mkemia Mkuu.

Hapa haimaanishi tufunge milango kupokea tiba za wenzetu au kushirikiana na dunia katika janga hili na mengine ya aina yake bali kwa sababu ya kuwa katika vita ya kiuchumi, ni vyema tusipokee kikasuku kila kinachotoka Ulaya, Marekani, China na kwinginko bali tuchunguze kama vina faida nasi na hasa kama kweli tunavihitaji kwa sababau sisi hatuna.

Columnist: habarileo.co.tz