Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Tumshukuru Mungu maisha ya JPM’

559a24354f224ef842a9dadcfa5d1ab5 ‘Tumshukuru Mungu maisha ya JPM’

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VIONGOZI wa dini wamewataka Watanzania kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha ya Rais John Magufuli kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kupokea uponyaji wa nafsi zao zilizoumia kutokana na kifo chake.

Walisema hayo jana kwa nyakati tofauti walipozungumza na HabariLeo kwa njia ya simu kuhusiana na kifo cha kiongozi huyo ambacho kimegusa hisia za wananchi wengi.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Jimbo la Ruaha Iringa, Joseph Mgomi alisema Watanzania wanapaswa kumtanguliza Mungu mbele kwa sababu faraja kubwa kuliko zote ni Mungu mwenyewe na isitoshe jambo hilo Rais Magufuli mwenyewe enzi za uhai wake alilisitiza.

“Mwenyezi Mungu ndiye aliyemwandaa Rais Magufuli na akaitumikia nchi yetu, akatuhudumia kwa kipindi chake na sasa Mungu ameona muda wake umetosha na amemuita kwake, ingawa ni ngumu sana kupokea hali hii tusinung’unike kufikia hatua ya kumkosea, lakini lazima tuamini kabisa alianzisha jambo na Mungu amemwandaa mwingine ambaye ataendeleza pale alipoishia.

” Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo alisema njia pekee kwa Watanzania kupona maumivu waliyoyapata kutokana na kifo cha Rais Magufuli ni kumwomba Mwenyezi Mungu awapatie faraja.

“Tukubali mapenzi ya Mungu kwamba alimpangia Rais wetu muda wake wa uhai na tumshukuru kwa yale mema ambayo tulipokea kupitia Rais wetu Magufuli, pia tujue kwamba kila mtu ana mwisho wake hapa duniani,” alisema Askofu Shoo.

Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum alisema Watanzania wanatakiwa kuongeza dua ya kumwombea Rais Magufuli na wasinung’unike na kusema mambo yasiyomridhisha Mwenyezi Mungu.

Naye Shehe Nurdin Kishki wa Masjid Ihsaan Veterinari Dar es Salaam alisema japo taifa limepata msiba mkubwa, Watanzania wanapaswa kuwa na subira na kumwomba Mwenyezi Mungu ili awavushe salama katika kipindi hiki cha huzuni na maombolezo.

“Tumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuwa kazi yake haina makosa na kila anachofanya kina hekima kubwa kwa wanadamu, pia tumwombe Mwenyezi Mungu ili taifa hili liendelee kuwa na amani na utulivu, kuondokewa na Rais wetu mpendwa isiwe sababu ya utulivu kukosekana katika nchi na Watanzania wajue kuwa tuna maadui wengi,” alisema.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini alisema msaada mkubwa wa uponyaji kwa maumivu waliyonayo Watanzania kutokana na kifo cha Rais Magufuli ni uamuzi wa serikali wa kuuzungusha mwili wake maeneo mbalimbali ya nchi ili watu waone na kutoa heshima zao za mwisho.

Alisema kisaikolojia jambo hilo limeleta uponyaji kwa wananchi kwa sababu waliweza kuuona na kumuaga mpendwa wao ama moja kwa moja au kupitia vyombo vya habari na kitendo cha wao kulia kumewasaidia kupunguza maumivu waliyonayo ya kufiwa na kiongozi waliyempenda.

Columnist: www.habarileo.co.tz