Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tumekuwa na Aziz Ki watatu tofauti ndani ya miezi 10

Azizi Ki Stephen Leo Machi.jpeg Tumekuwa na Aziz Ki watatu tofauti ndani ya miezi 10

Tue, 14 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Nilimwona Stephane Aziz Ki katika pambano la Yanga dhidi ya Real Bamako wiki iliyopita. Alitolewa wakati wa mapumziko na hakuna shabiki wa Yanga ambaye alishangaa au kuchukia. Huenda Aziz Ki alikuwa mchezaji mbovu kuliko wote wa Yanga jioni ile.

Nasikia alichukia kutolewa. Sijui alichukia nini? Kama kuna mtu anaweza kumpa mkanda wa pambano lile sidhani kama anaweza kumlaumu kocha wake, Nassiredine Nabi kumtoa nje ya uwanja wakati wa mapumziko.

Alipotolewa akaingia Khalid Aucho ambaye alirudi kucheza kama kiungo wa chini. Mudathir Yahya akaenda kucheza nafasi ya Aziz Ki. Yanga ikatulia. Jaribu kufikiria wakati ule Yanga ikikimbizana na Aziz Ki kuinasa saini yake. Kuna siku ingetokea Mudathir angekuwa mchezaji bora uwanjani kuliko Aziz? Hatukuwahi kufikiria.

Hii ni matokeo ya kuwa na Aziz Ki watatu ndani ya muda mfupi tu. Aziz Ki wa kwanza ni yule ambaye Simba na Yanga walimuona uwanjani akiwa na jezi ya ASEC Mimosas kiasi cha mwisho wa msimu uliopita kuanza kukimbizana kuinasa saini yake. Alionekana kuwa mchezaji aliyetimia hasa.

Alikuwa na umiliki mzuri wa mpira. Alikuwa ana mashuti mengi yaliyolenga lango. Alikuwa ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho. Katika hali ya kawaida, Yanga walikuwa wamemuona Aziz kama namba 10 kamili ambaye alikuwa jibu lao kwa kiungo wa Simba, Clatous Chama ambaye kwa muda mrefu alikuwa anawasumbua akili.

Zaidi ya kila kitu, Aziz Ki alionekana kama vile angekuwa ‘Chama mwenye nguvu’ zaidi kutokana na umri wake, lakini misuli yake iliyojengeka vyema. Huyu alikuwa Aziz Ki wa kwanza ambaye tulimwona uwanjani katika mechi mbili ambazo Simba walicheza na ASEC Mimosas nyumbani na ugenini katika michuano ya CAF.

Baada ya hapo akasajiliwa Yanga na kuwa mchezaji anayelipwa zaidi klabuni. Wengine wanadai ni mchezaji anayelipwa zaidi katika Ligi Kuu. Sina uthibitisho. Ujio wake Yanga ilionekana kama vile Yanga walikuwa wanaunda timu ya kutisha barani Afrika.

Hata hivyo, tangu atue klabuni Aziz akawa mtu mwingine kidogo. Huyu alikuwa Aziz Ki wa pili tofauti na yule wa kwanza. Aziz Ki huyu alikuwa bora katika matukio, lakini kwa mpira wa jumla alikuwa tofauti na Aziz Ki wa kwanza.

Kuna matukio kadhaa ambayo ukiyakusanya na kuyaweka katika video unaweza kudhani Aziz amefanya mambo ya maana sana lakini ukweli ni kwamba mpaka sasa hajafikia katika kiwango chake cha ASEC na badala yake haya matukio ndio ambayo walau yameweza kumtofautisha na wachezaji wengine.

Bao lake dhidi ya Aishi Manula lilikuja kwa wakati mwafaka. Litakumbukwa kwa muda mrefu ujao kwa sababu alifunga katika mechi muhimu dhidi ya watani wa jadi. Lilikuwa bao la kusawazisha. Pia alikuwa amefunga kwa umaridadi mzuri wa mpira wa kutengwa.

Mabao ya aina yale huwa yanakumbukwa kutokana na umuhimu wake. Hata mchezaji akiondoka zake nchini huwa anakumbukwa kwa mabao ya aina yale.

Hata kama lingekuwa pambano la watani wa jadi wa Manchester, London, Milan au Paris bado aina ya bao lile lingekumbukwa kwa umuhimu wake.

Lakini anakumbukwa kwa bao lake ambalo liliwapeleka Yanga katika hatua ya makundi ya michuano ya Shirikisho. Bao pekee dhidi ya Club Africain ugenini katika ardhi ya Waarabu.

Huwa inatokea nadra kwa mchezaji kuibuka shujaa katika ardhi hiyo. Aziz alifanikiwa kufanya.

Lakini Aziz huwa anakumbukwa kwa madaha yake ya kupenda kupiga tobo wachezaji wa timu pinzani mara kwa mara. Anaweza akaondoka uwanjani bila ya bao wala pasi ya bao, lakini usiku wakati ukipitia video mbalimbali za mechi ukaona mara kadhaa alifanikiwa kuwapiga tobo wachezaji wa timu pinzani. Watanzania huwa wanapenda pia hivyo.

Pamoja na yote hayo, Jumapili wiki iliyopita tulimuona Aziz Ki wa tatu. Aziz Ki anayechukiza ambaye mashabiki wa Yanga hawakutarajia kumuona uwanjani wakati ule wakiwania saini yake. Huyu alikuwa Aziz Ki ambaye kocha aliona bora nafasi yake ichezwe na Mudathir kuliko yeye.

Kwanza kabisa alichezeshwa katika nafasi yake pendwa. Namba 10. Kazi yake ilikuwa ni kumchezesha Fiston Mayele, pia alipaswa kurudi nyuma kuwasaidia kazi viungo wake wa chini Yannick Bangala na Mudathir.

Hakufanya hivyo. Wakati Yanga ikiwa haina mpira alikuwa mzito kurudi kiasi cha kuwafanya Real Bamako watawale mpira zaidi katika eneo la kiungo. Kama hilo lilikuwa jambo baya basi jambo baya zaidi lilikuwa pale alipokuwa anapasiwa mipira.

Aziz alikuwa hatulii. Alikuwa anapoteza karibu kila mpira aliokuwa anapewa. Alitaka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Alitaka atulize, apige kanzu au chenga. Hakutaka kucheza mpira rahisi. Kila wakati alicheza mpira mgumu. Matokeo yake hakuweza kufanya kazi yoyote katika zile mbili ambazo Nabi alimpa.

Hakuwezi kuwaona wenzake kina Mayele na kuwapasia kwa haraka, pia alishindwa kuwasaidia kina Bangala katika ulinzi.

Huyu ndiye aliyekuwa Aziz Ki wa tatu. Aziz Ki tofauti kabisa na yule ambaye tulimuona na ASEC Mimosas.

Columnist: Mwanaspoti