Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tumefuzu Afcon, lakini hatuna raha!

Rais Samia Atoa Mil. 500 Taifa Stars Kufuzu AFCON.jpeg Tumefuzu Afcon, lakini hatuna raha!

Fri, 15 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kumbukumbu zitaendelea kuonyesha Taifa Stars imefuzu Kushiriki michuano ya AFCON mara tatu.

Historia itaendelea kutulinda na kutuheshimu kama Taifa lilofuzu Kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika mara tatu. Sio jambo dogo. Haikuwa rahisi hata kidogo.

Asilimia 70 ya Watanzania umri wao ni chini ya miaka 34, tafsiri yake ni kuwa tayari wameshuhudia timu yetu ikifuzu mara mbili kwa macho yao na mara moja kwa kuhadithiwa.

Stars ilifuzu mbele yao mwaka 2019 kwa kumchapa Uganda mechi ya mwisho 3-0 pale Benjamini Mkapa Stadium na sasa inafuzu mbele yao kwa kutoka suluhu dhidi ya Algeria ugenini mbele ya macho yao.

Lakini je, Watanzania wana raha? Wanafurahia timu yao inavyocheza? Sina majibu ya moja kwa moja. Najua uzuri au ubaya ni mtazamo wa mtu na mtu lakini kizuri huwa hakijifichi.

Tulifuzu mbele ya Uganda mechi ya mwisho mwaka 2019 wakiwa wameshafuzu. Kiukweli, haikuwa mechi ambayo Waganda waliitaka sana. Walicheza bila presha yoyote na ikiwa rahisi kwetu Kufuzu.

Tumefuzu kwa mara nyingine juzi Algeria huku wao wakiwa tayari wameshafuzu. Hakukuwa na presha kubwa kwao.

Hawakuwa wanataka chochote kwenye mechi ile ndiyo maana ikaleta pia wepesi kwetu. Ni kweli tumefuzu kwa mara nyingi lakini kama unafuatilia vizuri uchezaji wa timu yetu ya Taifa, utakuwa tu na wasiwasi.

Hakuna mpira mwingi tunaocheza. Hakuna soka lolote la kuvutia! Tumefuzu tena lakini hatuna raha!

Ukitazama klabu zetu zinavyocheza hasa Simba na Yanga, wanacheza vizuri sana kuliko Taifa Stars. Unaona burudani. TP Mazembe anafungwa vizuri tu. Al Ahly anapasuka kirahisi tu. Lakini ukitazama Taifa Stars, wasiwasi ni mkubwa.

Hakuna burudani ya uhakika. Niheshimu kazi kubwa inayofanyika kwenye harakati za kufuzu kwenye michuano hii mikubwa lakini sijaona burudani yoyote.

Kama tungekuwa na timu bora, tungefuzu kabla ya kukutana na Algeria mechi ya mwisho. Tufuzu kwenye mechi yetu ya pili dhidi ya Uganda. Tungefuzu Kwa Mkapa. Ni kama tunafuzu kwa kubahatisha.

Ni kama tumejaa wasiwasi. Kwa miaka hii mitano ya hivi karibuni, mpira wa Tanzania umekuwa sana pengine kuliko nchini yotote kwenye ukanda wa CECAFA.

Kwa miaka ya hivi karibuni, mpira wa Tanzania ndiyo unatengeneza pesa nyingi kuliko nchini yoyote ya CECAFA lakini bado tunafuzu kwa kusuasua. Bado Taifa Stars inabutua butua sana! Kuna kazi kubwa ya kufanya.

Badala ya kwenda kutangaza Taifa letu kwenye Afcon kule Ivory Coast, tusijeenda kujitia aibu.

Kwa aina ya wachezaji tulionao tunastahili kuona walau mpira unaovutia. Tunastahili kuona boli likitembea. Sio kukaba tu kila wakati. Sio nguvu tu dakika zote 90. Ni kweli siku hizi tunafuzu kucheza Afcon lakini tunacheza mpira mbovu sana.

Bado ukuaji wa ligi yetu hauakisi moja kwa moja uchezaji wa Taifa Stars. Uganda wamekuwa taifa bora kisoka kwenye ukanda wetu kwa miaka mingi sana lakini kwa sasa hawatuwezi.

Nadhani kuna kazi kubwa ya kufanya pale kwenye benchi la ufundi. Mechi ya ugenini Algeria haina lawama yoyote lakini mechi dhidi ya Niger na Uganda, tulipaswa kucheza vizuri zaidi. Hawa hawa kina Mzamiru Yassini wakiwa Simba wanavutia zaidi kuwatazama kuliko wanapokuwa Taifa Stars.

Kwenye kundi la kina Feisal Salum, Simon Msuva, Kibu Denis, Novatus Dismas unashindwaje kucheza vizuri? Watu wa benchi la ufundi watusaidie kwenye hili. Stars ikiwa dimbani ni presha tupu hata kama inacheza na Kenya au Uganda tunaowazidi kwa sasa.

Timu yetu ni kama kila siku inatafuta muunganiko. Ni kama kila siku tunaanza upya. Hatuna kima Riyard Mahrez kama wenzetu lakini tunao wachezaji wa walau kucheza vizuri. Huku kufuzu kwa mbinde baada ya mpinzani kuwa ameshafuzu mechi ya mwisho kuishe sasa.

Tuko kwenye zama ambazo ukanda wetu kufuzu Afcon inapaswa kuwa lazima. Kenya, Uganda, Burudani, Rwanda wote tumewaacha Kisoka kwa sasa. Ni wakati wa kufuzu kwa kishindo sio presha tunazokutana nazo Stars ikiwa uwanjani.

Ni kweli tumefuzu Afcon lakini ni wasiwasi mtupu kuelekea michuano yenyewe hapo baadaye Ivory Coast. Hakuna mwenye uhakika wa kwenda kufanya vizuri. Timu yetu bado haionyeshi soka safi uwanjani. Bado Taifa Stars haikupi matumaini. Tunakwenda kwa nguvu ya dua na maombi.

Benchi la ufundi lina kazi kubwa sana ya kufanya kuelekea Ivory Coast. Tukienda kama tulivyo, tutaenda kutia aibu. Ni lazima tufanye maandalizi ya Kikubwa.

Afcon kuna wanaume kule kutoka Senegal. Kuna miamba kutoka Misri. Ni mchaka mchaka hasa. Kuna watu wanaitwa Morocco, kuna vijeba kutoka Nigeria. Sio mchezo.

Tunahitaji kujipanga kweli kweli kuelekea Afcon. Ni kweli tunafuzu Afcon siku hizi lakini bado uwezo wetu unaonekana kuwa chini sana uwanjani.

Ukitazama Simba na Yanga uwanjani, wanavutia zaidi kuwatazama kuliko Taifa Stars. Sio tu kwa sababu za wachezaji wa Kigeni, hata wazawa pia wanaupiga mwingi.

Sioni bado mpira mwingi pale Stars. Sioni burudani yoyote kwenye timu yetu. Ni Mwendo wa maombi tu kuanzia dakika ya kwanza hadi 90.

Nadhani tunapaswa kutoka huku na kuiona timu yetu ikicheza Vizuri.

Umeonaje kiwango cha Taifa Stars? Naomba maoni yako kwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Wasiwasi ni mkubwa sana Stars ikiwa uwanjani. Ni kweli Tumefuzu lakini wengi tuna mashaka na uchezaji wetu.

Columnist: Mwanaspoti