Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tumeepushwa na Adel Amrouche, tujipange

Amreouche Adxdh.jpeg Adel Amrouche

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Adel Amrouche ni mmoja wa makocha ambao wamewahi kupewa timu na kwa muda mfupi wakawa na mafanikio, kama hayo ya kuiwezesha timu ya taifa ya soka, Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, Afcon 2023.

Ni kocha ambaye hata falsafa yake ya uchezaji inaonekana kirahisi, hasa anapokabiliana na timu ambayo kwa kiasi kikubwa inatofautiana kiuwezo na Tanzania. Alidhihirisha hilo wakati Tanzania ikisaka pointi moja ili ifuzu kwenda fainali zinazoendelea Ivory Coast na akaipata, tena ugenini kwa Waalgeria ambako kwa kawaida huwa ni vigumu.

Hata tulipocheza na Waganda ambao ni wenzetu hapa Afrika Mashariki, tuliwamudu na hivyo kurahisisha njia ya kwenda Ivory Coast.

Pengine mafanikio yake ndani ya muda mfupi yalimuinua juu na kumfanya aanze kuogopewa, jambo ambalo inaonekana alilijua, hivyo kujenga kiburi ambacho kilijenga hofu, hata kwa waajiri wake, yaani Shirikisho la Soka (TFF).

Alijibu kwa dhihaka swali la mwandishi ambaye alitaka kujua sababu za kuachwa kwa kinda, Kelvin John kwenye kikosi kilichokwenda Ivory Coast. Ingawa alisema anamlinda, kauli kama za kutumia jina la Kylian Mbappe kumwelezea kijana huyo, zililenga kuhoji na upande mwingine kudhihaki sababu za Kelvin kufananishwa na Mbappe. Alisema Mbappe halisi anacheza Ligi Kuu ya Ufaransa, wakati huyu yuko kikosi cha pili cha timu ya Ubelgiji.

Lakini kibaya zaidi ni kueleza umma kuwa alikuwa mtovu wa nidhamu. Ningeelewa kama angekuwa anamzungumzia Bakar Mwamnyeto au Simon Msuva kwa sababu wawili hao wameshakomaa na wanajua jinsi ya kukabiliana na hali kama hiyo, lakini si Kelvin ambaye ndio kwanza anafikia umri wa miaka 20. Tatizo lake lilitakiwa liishie huko kambini, akalishwe chini, aonywe na kupewa muda wa kujirekebisha. Lakini alimuua kisaikolojia na hivyo zinahitajika juhudi nyingine za kisaikolojia kumrejesha kwenye hali ya kawaida.

Niliandika humu kuwa vyombo vya habari vinapaswa kulichunguza suala hilo na kuupa umma taarifa, ili suala hilo lijulikane kwa kina na kila upande ujifunze. Lakini kocha alitakiwa aonyeshe kuwa ni mzazi na si mtoaji shutuma.

Tangu aje nchini, Amrouche amekuwa akiongea na waandishi pale tu anapolazimika, kama wakati wa mechi. Lakini hajawahi kuitisha vyombo vya habari kwa hiari yake na kuzungumzia mipango yake na nini Watanzania watarajie kutoka kwake.

Kufanya hivyo ni kuonyesha kuwajibika kwa taifa ambalo limekuajiri, hivyo kujenga imani kwa mashabiki. Lakini kutarajia matokeo ndiyo yazungumze, hujenga kiburi kama matokeo yanakuwa mazuri.

Hata TFF ilitakiwa imwajibishe kwa kumuandalia mikutano na waandishi wa habari kuzungumzia masuala kadhaa ya timu ya taifa badala ya kuwaacha Watanzania wasubiri litakalotokea.

Wakati akiwa kocha wa Burundi alijenga mawasiliano na Rais Pierre Nkurunzinza, hivyo akawa hashikiki. Hakuna kiongozi wa soka wa Burundi aliyekuwa na sauti kwake isipokuwa kauli ya Nkurunzinza pekee.

Hiki ni kiburi ambacho angeweza kukiendeleza kama angepata nafasi ya kuongea na viongozi wakuu wa nchi na wakamwelewa. Ni dhahiri kuwa angepata nafasi hiyo, Wallace Karia na wenzake wasingekuwa na ubavu wa hata kumsimamisha kazi baada ya kufungiwa mechi nane na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Hata kauli ya viongozi wa soka Tanzania baada ya Amrouche kuropoka katika mahojiano na televisheni ya kwao, inaonyesha ni kwa jinsi gani raia huyo wa Algeria alishaanza kujijengea nguvu kubwa kiasi cha kuogopewa na mamlaka.

Katika hali ya kawaida, TFF ndio walitakiwa waanze kuchukua hatua kwanza dhidi ya Amrouche baada ya kuingiza siasa za chuki kati ya Algeria na Morocco kwenye timu ya taifa.

Amrouche alidai kuwa Morocco imekuwa na nguvu kubwa kiasi kwamba huwa inajipangia, hata waamuzi ili waipendelee. Alitaka kucheza mechi ya kisaikolojia (mind game) kabla ya Taifa Stars kuivaa Morocco, lakini akashindwa kuzuia chuki za nchi yake dhidi ya Morocco.

Kwa kawaida, kuituhumu timu kuwa huwa inapendelewa na inajipangia waamuzi, kunahitaji ushahidi usio shaka kwa kuwa huwa na athari kubwa katika mechi zote ambazo timu imecheza.

Lakini aliweka weledi kando, akaweka mbele mambo binafsi. Rungu la kwanza lilitakiwa litoke TFF kwa kumuondoa kambini na baadaye lifuate la CAF. Lakini TFF ikabaki kujitetea na kujitenga na tuhuma hizo, ikisubiri CAF ndio waadhibu. Kulikuwa na woga kidogo kushughulikia suala hilo.

Nimejaribu kuzungumzia mambo kadhaa kuonyesha kasoro za Amrouche na lengo langu ni kutaka kujenga hoja kuwa huu ni wakati wa kumpa mkono wa kwa heri kabla mengine makubwa hayajakuja.

Kwa kawaida, timu ya taifa hucheza mechi sita hadi nane kwa mwaka ukichanganya na zile za kirafiki. Maana yake, baada ya kukosa mechi mbili za mwisho za hatua ya makundi, kama hatutasonga mbele kutakuwa na kiporo cha mechi sita mwaka huu. Maana yake hataweza tena kuihudumia timu hadi mwakani.

Sasa tunamhitaji wa nini tena? Ameshakata tiketi ya kurudi Algeria na hivyo hatuna budi kuungana naye kwa kumuacha aendelee na mambo yake kuliko kumsubiri amalize kifungo, huku akiendelea kujijenga na baadaye kuwa tatizo kubwa kwa soka letu.

Ni muhimu sana TFF ikawa na falsafa inayoiongoza timu ya taifa na ambayo makocha wote wakija ni lazima waifuate. Kuwajibika kwa jamii ni jambo kubwa linalomfanya kocha ajue anachokisema kitaulizwa baadaye na hivyo kuwa na weledi kazini.

Kujali nyota wetu wanaoibukia, ni jambo muhimu sana. Leo hii, Clement Mzize, Kelvin John, Kennedy Juma wala Abdul Suleiman ‘Sopu, kwa kutaja wachache, licha ya CAF kuongeza wachezaji watano wanaotakiwa wamemo kwenye vikosi vilivyokwenda Ivory Coast.

Tungekuwa na falsafa ya timu, tungemwambia kocha kati ya hao watano walioongezwa hadi kufikia jumla ya wachezaji 27, watatu ni lazima wawe vijana wanaosakata soka ndani ya nchi. Kwa jinsi hiyo tungeepukana na kina Tarryn.

Kwa hiyo, tumeepushwa na Amrouche tuachane naye vizuri, lakini tujipange upya jinsi ya kushughulikia makocha ili timu ya taifa iwe kitu cha kipekee na si kitu ambacho yoyote anaweza kujifanyia chochote.

Columnist: www.tanzaniaweb.live