Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuliwapelekea Hazard wameturudishia majanga

IMG 4242 Hazard Avunja Mkataba.jpeg Eden Hazard

Mon, 19 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ilikuwa hadithi nzuri na ya kusisimua ambayo mwandishi wake alikuwa mahiri, akaiandika vizuri mwanzo lakini akaimaliza ovyo. Hadithi ya Eden Hazard na mpira. Hadithi ya sisi na Eden Hazard. Ilikuwa hadithi nzuri lakini imekuwa na mwisho wa ovyo.

Kwa Eden mwenyewe, nadhani kwa sasa angetamani aendelee kuiota ile ndoto yake. Asingeamshwa katika utamu wa usingizi aliokuwa anaupata Chelsea. Ikafika nyakati akaamka zake na kwenda kucheza Real Madrid. Hapo ndipo kila kitu kilivurugika.

Wiki iliyopita Real Madrid wametangaza kuchana mkataba wake. Na yeye mwenyewe ameridhia. Sidhani kama ana hamu ya kucheza soka. Hapana. Sidhani. Nasikia anataka kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 32 tu.

Kumbuka kwamba Cristiano Ronaldo ana miaka 38 lakini bado anacheza soka. Kumbuka kwamba Zlatan Ibrahimovic amestaafu soka wiki iliyopita akiwa na miaka 41. Leo Eden anataka kuondoka katika soka akiwa na umri wa miaka 32 tu.

Nini kimetokea kwa Hazard? Sijui. Wakati mwingine maisha ya mpira yana nuksi zake. Wakati mwingine nuksi zenyewe zinajitokeza pale unapoamua kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Kila kitu kinaharibika.

Hazard alikuwa na kila sababu ya kuondoka Chelsea kwenda Real Madrid katika dirisha kubwa la majira ya joto 2019. Umri sahihi. Alikuwa na miaka 28. Pale Chelsea na England kwa ujumla alikuwa ameonyesha kila maajabu.

Unamkumbuka Hazard? Mpira ulikuwa hauchomoki katika miguu yake. Alikuwa kama vile ana gundi katika viatu vyake. Chenga zake na uwezo wa kukaa na mpira kwa muda mrefu vilistaajabisha wengi. Lakini zaidi ya yote alikuwa na uamuzi sahihi kila wakati. Kifupi Hazard alikuwa hatari.

Alipokwenda Madrid? Ghafla Hazard akawa mzigo. Kwanza akakutana na majeraha ambayo hakuwahi kuwa nayo England. Hii ni nuksi ya kwanza. Inaaminika kwamba karibu mwili mzima wa Hazard ulikuwa na matatizo. Leo goti, keshokutwa mfupa mdogo karibu na kisigino, mara mgongo. Hata Corona pia ilimpitia Hazard.

Baadaye Hazard akaandamwa na uzito. Mwisho wa siku alibakia kuwa mchezaji aliyekaa katika vitanda vya hospitali kwa muda mrefu kuliko kugusa nyasi za Santiago Bernabeu. Msimu wake alicheza mechi 22 tu na kufunga bao moja.

Kumbuka kwamba hapo Real Madrid huwa inashiriki mechi 38 za La Liga, mechi nyingi za Ligi ya Mabingwa na mechi nyingi za Kombe la Mfalme. Hata hivyo, kwa msimu mzima alifunga bao moja tu na kucheza mechi 22.

Inachekesha nitakapokwambia kwamba msimu wake bora ulikuwa 2020/2021. Kisa? Alicheza mechi 25 akafunga mabao manne na kupiga pasi nne za mabao. Umewahi kufikiria kwamba katika ubora wake Hazard angeweza kuambiwa kwamba alikuwa ana msimu bora kwa kufunga mabao manne tu na kutoa pasi za mabao manne tu?

Hata hivyo, namba zinatuambia hivi. Namba hazidanganyi. Msimu uliofuata 2021/2022 Hazard alifunga mabao mawili akatoa pasi za mabao mawili huku akicheza mechi 23. Kufikia hapo Madrid wakaanza kumchoka.

Msimu huu ulioisha hivi karibuni Hazard amecheza mechi saba tu huku akifunga bao moja na kutoa pasi ya bao moja. Kufikia hapo Madrid wakaona bora wauchane mkataba wake ambao walikuwa wanamlipa kiasi cha pauni 400,000 kwa wiki.

Mkataba wake ulipaswa kumalizika mwakani 2024. Nadhani hata Hazard mwenyewe hakutaka kuwa mbishi na mnyonyaji. Aliamua bora yaishe aondoke zake. Ni wazi kwamba dhamira yake ilimsuta. Kwanini apokee pesa ya bure wakati anashinda zaidi hospitalini?

Kifupi Hazard alipata majeraha mara 18 pale Santiago Bernabeu kiasi cha kukosa mechi 78 kutokana na matatizo hayo. Kwa misimu mitatu aliyokaa klabuni amefunga mabao manane tu. Haya mabao alikuwa anayapita kwa miezi mitatu tu pale England ndani ya msimu mmoja.

Kabla ya kula Krismasi, tayari alikuwa anapita idadi hii ya mabao lakini pale Santiago Bernabeu amelazimika kutumia misimu mitatu kufunga mabao haya. Ni kweli huyu ni Hazard ambaye tunamfahamu? Hapana. Sio kweli.

England hakuwa hivi. Alikuwa fiti kimwili na kiakili. Amewasumbua watu wengi England kiasi kwamba alifikia hatua ya kuwa mchezaji hatari zaidi katika Ligi. Hata hivyo, Hispania amekuwa mchezaji wa ovyo na aliyeandamwa na majeraha.

Nini kimetokea? Huwa inatokea mara nyingi kwa baadhi ya wachezaji. Huwa wanang’ara katika ligi moja au klabu moja. Wanapojaribu kuvuka tu kutoka upande mmoja kwenda mwingine basi kila kitu kinakwenda kombo. Ni kama vile wanajitilia nuksi katika maisha yao. Hazard na mejaraha wapi na wapi? Lakini amekwenda Hispania tu kila kitu kimekwenda kombo.

Mkumbuke Philippe Coutinho. Naye ilikuwa hivi hivi. Kila kitu kilikuwa kinakwenda sawa pale Anfield. Mashabiki walevi wa Liverpool wakamuona kama ‘Mungu mtu’. Alipoamua kunyanyua mguu kwenda Barcelona kila kitu kikabadilika.

Akatolewa kwa mkopo kwenda Bayern Munich lakini haikusaidia. Akarudi tena Barcelona haikusaidia. Ameuzwa kwenda Aston Villa bado haijasaidia. Jaribu kufikiria eti Coutinho yule hata Aston Villa hana nafasi ya kucheza. Hizi ndio nuksi za kuhama timu.

Kuna ambao kila kitu kinakwenda sawa lakini kuna wale ambao wakihama tu katika klabu ambazo walikuwa wanapendwa basi kila kitu kinakwenda ovyo. Hazard ni mfano halisi wa wachezaji wa namna hii. Na nadhani tumeshuhudia mwisho wake.

Hata kama akiamua kutostaafu na kuendelea kucheza soka siamini kama anaweza kwenda kwingine na tukashuhudia ubora wake. Nadhani kipindi chake bora katika maisha ya soka kitabakia kile kile ambacho alikuwa Chelsea.

Kitu ambacho naweza kumtofautisha na Coutinho ni ukweli kwamba yeye alikuwa na sababu lukuki za kuondoka zake Chelsea na kwenda Real Madrid. Coutinho hakuwa na sababu za msingi za kwenda Barcelona. Alikuwa katika timu sahihi na yenye mwelekeo sahihi. Hazard alikuwa ameshashinda kila kitu Chelsea na wakati huo Real Madrid walikuwa wametoka kumuuza Ronaldo kwenda Juventus.

Labda ulikuwa muda sahihi kwake kwenda kujaribu kuvaa viatu vya Cristiano. Hata hivyo, haikuweza kutokea. Kifupi ni kwamba sisi tunaopenda Ligi Kuu ya England tuliwapelekea rafiki zetu wa Hispania mchezaji anayeitwa Hazard lakini wameturudishia mchezaji anayeitwa majanga. Ni kama tafsiri ya jina lake kwa Kiswahili.

Columnist: Mwanaspoti