Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tulia, Bunge si chawa wa Serikali

Bunge Pic Data Bunge

Sat, 15 Apr 2023 Chanzo: Luqman Maloto

TULIA, BUNGE SI CHAWA WA SERIKALI

BUNGE, kazi yake namba moja; Kuisimamia Serikali.

Bunge, msingi wa utumishi wake; Uwakilishi wa wananchi.

CAG amesema fedha za wananchi hazipo salama serikalini.

Rais Samia alikiri alipopokea ripoti ya CAG kuwa wizi, uhuni na ufisadi vimeshamiri. Aliahidi kuchukua hatua.

Bosi mkuu wa nchi ni wananchi. Wamesikia kwenye ripoti ya CAG kuna ubadhirifu wa fedha zao.

Wananchi huajiri (kwa kupiga kura). Humchagua mtu ambaye humpa kila kitu ili akaendeshe nchi yao kwa mujibu wa Katiba, sheria na maadili. Huyo mwajiriwa ndiye Rais - Mkuu wa Serikali.

Wananchi hutaka nchi yao iendeshwe kwa uadilifu. Huajiri chombo cha kusimamia uendeshaji wa nchi yao, vilevile kutunga sheria zinazoongoza nchi. Chombo hicho ni Bunge.

Kuhakikisha matakwa ya wananchi yanatimizwa; Bunge kama chombo kinachomwakilisha bosi (wananchi), kimepewa mamlaka ya kuvunja serikali (kirahisi) kupitia kumng'oa Waziri Mkuu.

Bunge pia limepewa nguvu ya kumng'oa Rais, ingawa kuna "kamchakato". Ila mamlaka linayo.

Bunge ni kutovu cha mihimili, a mothership connection au the supreme organ. Katiba, ibara ya 38 (2) (a), inasema, Bunge likivunjwa, Rais na Serikali yake hawana kazi. Bunge ni mhimili mama.

CAG anafanya kazi kwa niaba ya Bunge, kuikagua Serikali na kukabidhi ripoti. Bunge huiwajibisha Serikali. Lengo ni wananchi watumikiwe kwa uadilifu na wahudumiwe vema.

Bunge lipo kwenye vikao vya Bajeti mpya (2023-2024). Kuitenda vema kazi yao, wamekabidhiwa ripoti ya ukaguzi wa Bajeti iliyokamilika Juni 30, 2022.

Unaomba fedha mpya, za nyuma ulitumiaje? Huo ndio msingi wa ripoti ya CAG kabla ya Bunge kupitisha Bajeti mpya.

Tumeshaona. Kuna Ubadhirifu. Ufisadi.

Bunge linapaswa kugoma kujadili Bajeti mpya mpaka kuridhishwa na uwajibikaji wa Bajeti ya nyuma.

Spika Tulia ameahirisha mjadala wa ripoti ya CAG hadi Novemba. Anataka Bunge lipitishe Bajeti kwanza. Anakwepa wajibu wa Bunge kuiwajibisha Serikali.

Si mpaka wananchi wavamie Bunge wandoke na Siwa (fimbo ya mamlaka). Bunge kwenda kinyume na matarajio ya wananchi hupoteza uhalali.

Bunge si chawa wa Serikali. Ni mboni ya wananchi. Tulia akitaka uchawa wa Serikali aache Uspika wa Bunge.

Ndimi Luqman MALOTO

Columnist: Luqman Maloto