Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tukio la Lee Masson limetufundisha mengi

Lee Mason Tukio la Lee Masson limetufundisha mengi

Tue, 28 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kila siku kuna cha kujifunza kutoka kwa mwingine. Ndivyo binadamu anavyojisahihisha na kujiendeleza kila wakati. Kuna mambo ambayo pengine huwa hatuyakubali yanapoingizwa, lakini mwishoni tunakuja kuona umuhimu wake na kuyakumbatia.

Wakati wanateknolojia wakifikiria kuingiza teknolojia ya kubaini mpira kama umevuka mstari (goalline technology), Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) wa wakati huo, Sepp Blatter hakuikubali sana teknolojia hiyo, akitetea waamuzi kuwa nao ni binadamu na lazima wafanye makosa, akisema mpira wa miguu unachezwa na binadamu.

Lakini teknolojia ni kama mafuriko! Huwezi kuizuia kwa mikono. Kadri makosa ya waamuzi yalivyokuwa yanazidi, ndivyo wataalamu walivyonyesha kuwa yanaweza kupunguzwa kwa teknolojia.

Taratibu Fifa ikafanyia majaribio teknolojia hiyo na baadaye kuanza kuitumia. Teknolojia imezidi kufurika kwenye soka hadi hii ya sasa ya mpira janja ambao unaweza kung’amua mchezaji aliyeotea.

Mechi za Ligi Kuu ya England za wiki moja iliyopita zilikuwa na matukio ya uamuzi wa makosa ulioonekana kuwa ungeweza kuzuilika kama waamuzi wangekuwa makini kidogo zaidi.

Tukio la kwanza lilikuwa katika mechi kati ya Brighton& Hove dhidi ya Crystal Palace, ambayo ilipoteza mchezo huo kutokana na makosa ya refa msaidizi anayetumia video, maarufu kama V.A.R. Kosa la pili lilikuwa katika mechi baina ya Arsenal na Brentford wakati wenyeji walipopoteza pointi mbili kutokana na makosa ya V.A.R.

Waamuzi hao wasaidizi, ambao hukaa kwenye chumba maalum chenye runinga zilizounganishwa na kamera kadhaa zinazofuatilia matukio uwanjani wakati wa kuelekea golini, hutakiwa kumtaarifu refa kuhusu tukio ambalo amelifanyia uamuzi na kumtaka aliangalie kwa makini zaidi kabla ya kuendelea au kubadilisha uamuzi wake.

Hufanyua hivyo kwa kumuonyesha picha za marudio na za mwendo wa taratibu kwa kutumia runinga inayofungwa uwanjani. Baada ya kuangalia video hizo za marudio, mwamuzi huwa amepata taarifa nzuri kuhusu matukio hayo na kuamua kubadili uamuzi au kuendelea na msimamo wake.

Lakini waamuzi wa mechi hizo mbili walishindwa kutoa taarifa za kutosha, huku wa mechi ya Arsenal anayeitwa Lee Masson, akishindwa kuchora mstari unaoweza kuonyesha vizuri kama kulikuwa na kuotea kabla ya bao la kusawazisha kufungwa na Brighton.

Matukio hayo mawili yalikuja kipindi ambacho waamuzi wasaidizi wa V.A.R walifanya makosa mengi kiasi kwamba chombo maalum cha waamuzi, PGMOL (Professional Game Match Officials Limited) kililazimishwa kutoa taarifa kuelezea kwa undani matukio hayo.

Yalianzia Septemba wakati Ligi Kuu ya England ilipoitaka PGMOL itoe maelezo ya sababu za refa kukataa bao la West Ham United dhidi ya Newcastle na bao la Chelsea dhidi ya Crystal Palace. Ilikuwa ni hatuia ambayo haikuwahi kuchukulia huko nyuma.

Hata bao la Marcus Rashford katika mechi kati ya Manchester United na Manchester City lilisababisha mijadala, lakini jopo huru lililoundwa kuchukua tukio hilo, liliamua kuwa hakukuwa na kuotea kabla ya bao hilo.

Kwa tukio la Arsenal, PGMOL ililazimika tena kukubali kuwa kosa la Masson lilikuwa kubwa na halikustahili. Kabla ya hatua zaidi, Masson, ambaye ameshachezesha kwa takriban miaka 15, alitangaza kujiondoa PGMOL kwa ridhaa yake, uamuzi ambao ulitangazwa na chombo hicho wiki iliyopita.

PGMOL inafanya mabadiliko makubwa katika kusimamia majukumu yake na imeahidi kuongeza uwazi katika kushughulikia masuala ya mechi za soka ili wapenzi wa soka wawe na taarifa za kutosha kuhusu uamuzi na makosa yanayotendeka.

Katika mabadiliko hayo, PGMOL imemchukua mwamuzi wa zamani wa England ambaye amestaafu, Howard Webb kuongoza chombo hicho.

Huku ambako hakuna teknolojia hiyo, kuna makosa mengi ya uamuzi ambayo bahati mbaya sana hayashughulikiwi kiweledi na mengi yanaamuliwa kimazoea. Bado hatujawa tayari kukubali mbinu mpya zinazotumiwa na wenzetu, achilia mbali teknolojia ya V.A.R ambayo inaweza kuchukua muda kuikumbatia.

Kwanza, kwa kuwa na chombo huru kinachohusika na masuala tofauti, uwajibikaji unakuwa mkubwa. Ligi Kuu ya England ni huru. Ilishajitoa kutoka FA ya England na hivyo akili yake yote ni katika kuboresha ligi hiyo kwa kila hali—uamuzi, udhamini, uendeshaji na kuhakikisha maslahi ya klabu yanazingatiwa.

Hakuna siasa katika uendeshaji wa Ligi Kuu ya England kwa kuwa ni biashara kubwa iliyoajiri watu wengi na inayoingiza mapato makubwa na kuitangaza nchi. FA inabakia katika maendeleo ya mpira na uendeshajiwa mashindano mengine. Uamuzi wa kuahirisha mechi ya Ligi hauwezi kufanywa na FA, bali na Ligi Kuu tu.

Ni kwa jinsi hiyo, Ligi Kuu ya England inaweza kuiwajibisha PGMOL iwapo uamuzi unaonekana kuzidi kuwa mbovu na kuondoa ladha ya ushindani.

PGMOL pia ni chombo huru ambacho kinashughulikia maendeleo ya waamuzi. Hukutana kila baada ya muda kutathmini uchezeshaji wa mechi na waamuzi wanaonekana wana matatizo huingizwa kwenye program ya kuboresha stadi zao.

Na kwa kujua umuhimu wake na taswira mbaya inayoweza kusababishwa na uamuzi mbovu, PGMOL ililazimika kutoa maelezo ya makosa yaliyosababisha baadhi ya mechi kuisha kwa manung’uniko. Imeeleza wazi kuwa kuna makosa ya kibinadamu, lakini hayastahili kuendelea kuwepo kwa sababu ya kurahisishiwa kazi na teknolojia.

Hivi ni vitu ambavyo tulivianza kwa kuanzisha Bodi ya Ligi ambayo ingeweza kufikia hatua hii kama isingemezwa na Shirikisho la Soka (TFF). Kadri soka linavyokuwa duniani, ndivyo kunavyohitajika mgawanyiko wa majukumu ili kila upande uweke akili yote katika vigtu vichache vilivyo chini yake. Wazungu wanasema specialist is a person who knows a lot about a little, yaani mtaalamu ni mtu anayejua mengi kuhusu kidogo.

Kwanini tusigawanye majukumu ili waamuzi wajue mengi kuhusu uamuzi wao na kufanya kila kitu kuboresha fani yao ili umuhimu wao uonekane zaidi.

Hivi mashabiki watapokeaje taarifa ya chombo cha waamuzi kwamba uamuzi dhidi ya tukio fulani ulikuwa ni kosa ambalo lingeepukika na hatua kadhaa zinachukuliwa ili kuboresha uwezo wake kama kumuweka chini ya uangalizi na ikishindikana kuondolewa kwa muda kwenye ratiba?

Mwamuzi kama huyo anaposhughulikiwa na chombo chake, hawezi kuingiza siasa kwamba kuna mtu pale TFF hampendi, au ameshuhghulikiwa kwa sababu anadai malipo yake ya muda mrefu.

Lakini jingine la kuiga ni kitendo cha PGMOL kukubali hadharani kuwa kulikuwa na kosa katika mechi hizo, huku Masson mwenyewe akikubali kuwajibika kwa kujiondoa PGMOL.

Kama huku kwetu, pamoja na ukubwa wa kosa, mwamuzi angeweza kujitetea kwamba ndio kwanza ameanza kazi ya V.A.R na hivyo atajirekebisha kadri siku zinavyokwenda. Lakini Masson ameona hapana. Pamoja na kwamba ni kosa moja, ukubwa wake unatosha kumfanya ajiondoe pamoja na waamuzi wengine kumuonea huruma.

Huu uwajibikaji ndio tunautaka kwenye soka letu. Watu hawataki kuwajibika hata pale wanapofanya makosa makubwa. Kibaya zaidi, wakati mwingine mtu mkubwa kabisa katika soka anajitokeza na kumtetea, huku akilinganisha kosa lake nay a watu wengine. Hakuna kosda linalohalalisha kosa jingine.

Tutaweza kupiga hatua pale tutakapochukua hatua kulingana na kasi ya mpira inavyokwenda duniani badala ya kuridhika na mambo yanavyowenda hata kama hatusongi mbele.

Columnist: Mwanaspoti