Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuhuma za rushwa kwa waamuzi Bongo - 5

Waamuzi Zz.jpeg Tuhuma za rushwa kwa waamuzi Bongo

Tue, 10 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jana katika mfululizo wa Ripoti Maalumu kuhusu waamuzi wa soka nchini, tuliona tuhuma za kuwepo kwa upendeleo kwa baadhi ya waamuzi na kupewa mechi mfululizo.

Leo tunaendelea nayo kusikia kauli za Kamati ya Waamuzi na tuhuma za kuwepo kwa viendo vya rushwa kwa waamuzi na vipi juu ya usalama wao kazini. Je, kuna ukweli katika madai hayo? Endelea nayo upate majibu.

KAULI YA HAMDUNI

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi nchini, Nassor Hamduni anasema wanachozingatia kumteua mwamuzi ni kiwango anachokionyesha na sio upendeleo kama ambavyo wengi wao wamekuwa wakizungumzia suala hilo.

"Duniani kote mwamuzi anateuliwa kutokana na kiwango chake na wala sio vinginevyo, ni kweli kwenye michezo ya Yanga na Simba wamekuwa wakijirudia sana lakini tunapaswa kukubaliana ndio wapo bora," alisema na kuongeza;

"Tunachoamini tuna waamuzi wazuri ambao kadri ambavyo wanazidi kuchezesha tutawaona tu kwenye hii michezo mikubwa na isitoshe tumeanza kufanya hivyo hivi karibuni ingawa kikubwa kwao ni kuzingatia sheria 17 za soka.

NJE YA UREFA HATARI

Waamuzi licha ya kufanya kazi zao kwa ajili ya soka, lakini wana maisha nje ya uwanja kwani kila mmoja ana maisha yake yanayompa riziki.

Wapo ambao ni askari, wengine ni walimu, wapishi, wafanyabiashara na wengine ni wajasiriamali wadogo wadogo, lakini wote wanakutana kwenye mwamvuli mmoja wa uamuzi wa soka nchini.

Hata hivyo, inaelezwa wengi wao hawana ajira nyingine ya kuwaingizia kipato, zaidi ya ile ya uamuzi, baadhi ya waamuzi wanasema asilimia kubwa ya kundi hili ndiyo lipo kwenye uamuzi.

"Ili kuthibitisha ninachokimaanisha, chukua kalamu halafu anza kuorodhesha waamuzi wote wa Ligi Kuu utagundua kubwa ya waamuzi hawana kazi nyingine nje ya uamuzi," anasema mmoja wa waamuzi maarufu nchini.

Anataja majina ya waamuzi wenzake akisisitiza kwamba asilimia kubwa hawana ajira ila hiyo asilimia ndogo iliyobaki ndio wenye ajira za kudumu.

"Hapo tujiulize! kwa mazingira haya kama hakuna weledi tunatarajia ligi isiwe mbovu? pia angalia waamuzi wenye beji ya Fifa wale wanaochezesha kati halafu jiulize wanakazi gani, nenda kwa wale wa pembeni nao angalia wangapi wenye ajira ukimtoa baadhi yao kama, Frank (Komba) ambaye anajulikana anakazi yake na mwenye elimu yake ya maana ndio maana hana wasiwasi, Mkono yeye ni mwalimu na wengine wachache.

"Lakini wengi wao hawana ajira za kudumu, wapo pia wale wasiokuwa na beji ya Fifa japo wanastahili kupewa lakini wana ajira ambazo zinawabeba hivyo hawana njaa, mfano ni Charles Simon (Dodoma) mtu mwenye elimu yake (Mhadhiri) lakini bado anaisotea beji ya Fifa, Bugado Anold (Tanga) mtu mwenye elimu na kazi yake (Compassion), Meshack Suda (Singida).

"Wakaja kumpa beji ya Fifa, Kassim Mpanga (Tanga) Abdulaziz Ali (Arusha) lakini ndani ya msimu mmoja tu kafanya madudu na kupokonywa halafu rudi nyuma anza kuangalia elimu zao, hapo utagundua, kazi ya uamuzi ni kama imekuwa kimbilio la watu wasio na kazi maalumu," anasema.

CHANGAMOTO NA USALAMA

Hata hivyo, lile kundi dogo la waamuzi wenye ajira pia linadai kuwa na changamoto ambazo zinasababishwa na majukumu yao ndani ya uwanja, miongoni mwao wanasema, kazi ya uamuzi imewahi kuwaletea shida kwa waajiri wao, lakini yote kwa yote walisimamia misingi yao ya kazi.

"Nakumbuka nilipewa uamisho wa kikazi kutoka Dar es Salaam, kisa ilikuwa ni mechi ya hizi timu zetu kubwa za Simba na Yanga," anasema Israel Nkongo, mmoja wa waamuzi maarufu nchini.

Nkongo ambaye kitaaluma ni mwalimu anasema, bosi wake kazini alikuwa ni mmoja wa mashabiki kindaki ndaki wa mojawapo wa timu hizo za Kariakoo.

"Hakuridhishwa na matokeo ya timu yake kwenye mechi ambayo mimi nilikuwa mwamuzi wa kati, kwa kuwa ni bosi wangu alinitishia, lakini sikujali," anasema.

Anasema baada ya ile mechi, alipewa uamisho kutoka jijini Dar es Salaam na kupelekwa kwenye shule nyingine ya kijijini, lengo likiwa kumkomesha kutokana na uamuzi ambao haukumfurahisha bosi.

"Niliitumia ile changamoto kuwa fursa, wala sikujali, nilikubaliana na mpango wa bosi, lakini mwisho wa siku mwenyewe alijiona amekosea, kwani matokeo ya mpira hayahusiani na maisha yangu binafsi," alisema.

Tukio jingine ambalo Nkongo analikumbuka ni la kutishiwa maisha na mashabiki ikiwamo kwenye moja ya mechi ya Yanga na Azam ambayo alimpa kadi nyekundu Niyonzima Haruna na Nadir Haroub 'Canavaro'.

"Ukiwa mwamuzi unapaswa kusimama kwenye misingi ya taaluma yako na kusimamia sheria tu, kuna mashabiki hawapendi na hili ni tatizo.

"Nakumbuka kwenye ile mechi nilitishiwa sana, waliniambia watanifuata nyumbani, ingawa ni kweli kuna maisha mengine nje ya mpira, lakini hamaki ya mashabiki uwa inakuwepo uwanjani tu, baada ya pale mkikutana mtaani wapo watakaoishia kukwambia umewanyima ushindi na watakaokupongeza watakupongeza," anasema.

Hata hivyo waamuzi wanapata ulinzi kuingia uwanjani kuchezesha na wanapotoka, nje ya hapo wanajilinda wenyewe kuanzia kufika kwenye kituo cha mechi hadi wanapoingia uwanjani.

Mwamuzi mwingine, ambayeni mpishi, anasema, aliifanya kazi hiyo kwa mapenzi kutokana na utashi wake wa kupenda soka, hivyo kusomea uamuzi.

"Mimi ni mtaalamu wa kupika, uwa napika kwenye shuhuli mbalimbali, lakini ukinikuta uwanjani niko makini, japo baadhi ya watu uwa wanawachukulia waamuzi kama watu fulani hivi wameshindwa shuleni.

"Lakini wapo waaamuzi wasomi wengi tu, wengine mpaka madaktari, ila wanafanya kazi hii kwa mapenzi, kwa kuwa ni ya muda," anasema mwamuzi huyo.

MAADILI YAO YAKOJE?

Nkongo anasema maadili ya waamuzi hayatofautiani sana na watendaji wengine, akifafanua kwamba hiyo ni kazi kama zilivyo kazi nyingine na zina miiko yake. Kauli ya Nkongo inakolezwa na katibu mkuu wa Chama cha waamuzi (FRAT), Charles Ndagala ambaye anasema maadili kwa waamuzi ni jambo la kwanza wanaloambiwa kabla hata ya kuanza mafunzo. "Wapo ambao tuliwatimua kwa kukosa maandili, siwezi kuwataja kwa majina lakini walikuwa ni walevi kupindukia, hivyo waliondolewa kwenye orodha ya waamuzi nchini," anasema.

Anasema katika suala la maadili, cha kwanza anapofundishwa ni kutakiwa kuwa kioo cha jamii na mfano wa kuigwa kuanzia nyumbani, mtaani na anapoingia uwanjani. "Hii inajumlisha pia mavazi yake, anavyotembea, lugha na masuala mingine, aonekane mtu mwema mwenye maadili, lakini pia anakanywa kuhusu rushwa, ushabiki wa timu na kuwa kwenye magenge yanayobishania mpira.

Columnist: www.tanzaniaweb.live