Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tufikie mwenyekiti akiwa mwanaume, katibu mwanamke

C59c3b2442e115a04f9de9ca559f80c6 Tufikie mwenyekiti akiwa mwanaume, katibu mwanamke

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

DIBAJI iliyoandikwa mwaka 2010 na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mariam Mwafisi katika Itifaki ya Nyongeza ya Mkataba wa Kuondoa Ubaguzi Dhidi ya Wanawake iliyotafsiriwa Juni 2010 na kutolewa na wizara hiyo, inataka kila mmoja kuchukua hatua kuhakikisha vitendo vyote vya ubaguzi dhidi ya wanawake vinatokomezwa.

Aidha, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia nchini kwa muda mrefu wamekuwa katika harakati za kuonesha uwezo wa mwanamke katika siasa na uongozi huku pia, wakipambana dhidi ya ubaguzi, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.

Wanaharakati hao ni pamoja na taasisi kama Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Afrika (WilDAF), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), African Women Leaders Network (AWLN) na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa).

Taasisi hizo na nyingine mbalimbali kwa namna mbalimbali zimepambana ili kuona ushiriki kamilifu wa wanawake kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa nyakati tofauti.

Hii ni kwa kuwa katika jamii nyingi za Kiafrika Tanzania ikiwamo, watu bado wanawaona wanawake kama watu wasiopaswa na wasioweza kuongoza kwa ufanisi.

Hii inanikumbusha Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani aliyesema kwamba kama ilivyo kuwa wapo wanaume wasioweza uongozi, ndivyo ilivyo pia kuwa wapo wanawake wengi wenye uwezo wa uongozi.

Mbali na Katiba yetu, pia Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza Aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW, 1979) na mapendekezo ya Baraza la Usalama (UNSC 1325 (2000) yanatambua na kutoa haki kwa wanawake kushiriki uchaguzi kama wapiga kura au wagombea wa nafasi za uongozi.

Kifo cha Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli na kisha kuapishwa kwa aliyekuwa Makamu wake, Samia Suluhu Hassan kama inavyoagiza katiba, kinaonesha kuwa wanawake wana uwezo mkubwa kiuongozi pale mifumo kandamizi na baguzi dhidi yao inapoondolewa.

Ndiyo maana, wanaharakati mbalimbali wanapendekeza katiba za vyama vyote vya siasa, zitamke rasmi kuwa endapo mwanaume anakuwa mwenyekiti wa chama katika ngazi yoyote ya uongozi, basi katibu mkuu wa chama hicho awe mwanamke na kinyume chake.

Hii inalenga kugawanya nafasi za utendaji kwa jinsi hizi mbili na uzoefu unaonesha kwamba nchi ambazo zimepiga hatua ya usawa wa kijinsia katika masuala mbalimbali ikiwemo uongozi, zimepiga pia hatua kubwa ya maendeleo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben, katika moja ya mafunzo kwa wandishi wa habari anasema umefika wakati vyombo vya habari viwe chachu halisi katika mabadiliko ya kimtazamo katika jamii kwa kuchora taswira na uwezo chanya wa mwanamke katika uongozi, badala ya kumwona na kumwonesha kama msindikizaji katika kampeni.

Tamwa inaendesha mradi wa ‘Wanawake Wanaweza’ unaofadhiliwa na shirika la kimataifa la UN- Women (Tanzania) kwa kushirikiana na AWLN, TGNP, TCD na WilDAF.

Watu mbalimbali wanasema ushiriki wa siasa aliokuwa nao Samia hata kabla hajateuliwa kuwa Mgombea Mwenza katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 ambao mgombea wa CCM alikuwa John Magufuli aliyechaguliwa kuwa rais (alifariki dunia Machi 17, 2021), hatimaye Samia kuwa Makamu wa Rais na namna alivyotumikia wadhifa huo kiasi cha kuteuliwa tena kwa muhula wa pili na hata kuaminika na katiba hadi kuapishwa kuwa Rais wa Sita wa Tanzania akiwa mwanamke wa kwanza katika wadhifa huo nchini na hata Afrika mashariki, ni ishara wazi kuwa ‘wanawake wanaweza.’

Ndiyo maana Rose amekuwa akisititiza kuwa, katika uchaguzi mwingine wowote ujao na kwa ngazi yoyote, wanawake wanapaswa kushirikishwa mapema na kikamilifu katika mchakato wote ili wajiamini zaidi huku wakijengewa utayari zaidi kukabili changamoto zinazolenga kuwakatisha tama.

Anasema changamoto hizo zinaweza kuwa za kiuchumi na kijamii kama lugha chafu zinazolenga kutweza utu na uwezo wao.

Anasema: “Kwa kutumia kalamu zetu, waandishi wa habari tuna wajibu katika jamii kuonesha taswira chanya na uwezo wa mwanamke katika uongozi, hasa kwa kupuuza kauli za kuwabeza, kuwakejeli na kushusha uwezo wao eti kwa kuwa ni wanawake.”

Mtendaji huyo mkuu wa Tamwa anasema hata wanawake wengine waliopata nafasi za uongozi, hawana budi kupanga mikakati madhubuti mintarafu kuendelea kuwepo na kuongezeka kwa wanawake katika ushiriki kamilifu wa siasa na uongozi.

Anawataka waoneshe wigo mpana wa uongozi, ujasiri, uwezo na kujitokeza kuzungumzia masuala ya wanawake nafasi mbalimbali zikiwamo za vyombo vya habari ambavyo ni fursa nzuri kwa kupaza sauti.

“Katika chaguzi zote wanawake washirikishwe mapema na kikamilifu katika mchakato wote ili wajiamini zaidi huku wakijengewa utayari kukabili changamoto zinazolenga kuwakatisha tamaa, nasi tutumie kalamu zetu kuwaunga mkono kwa kuzingatia uwezo na uadilifu wao, badala ya kuwakatisha tamaa,” anasema Rose.

Mradi wa Wanawake Wanaweza unatoa mafunzo kwa wanahabari ukilenga kuibua changamoto zinazowakumba wanawake katika harakati za kushiriki siasa na uongozi.

Mradi unalenga pia kuwawezesha wanahabari kujua namna ya kuzibaini, kuzikabili changamoto za ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, kuhamashisha na kuwaelimisha wanawake ili wajitokeze kuwania nafasi za uongozi ama wa kuchaguliwa, au kuteuliwa katika kada mbalimbali kadiri ya sifa na uwezo wao halisi.

Katika moja ya mafunzo hayo, wanahabari walioshiriki waliazimia kuepuka lugha za kushusha hadhi ya wanawake wakiwamo wanaogombea nafasi za uongozi wa kisiasa sambamba na maswali yenye ladha ya ubaguzi wa kijinsia na badala yake, wawaibue na kuwahamasisha wanawake kujitokeza na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Aidha, wanahabari wanahimizwa kuwapa wanawake nafasi sawa katika vyombo vyao huku nao wakiweka msukumo kwa vyama vya siasa kutoa nafasi sawa za uongozi kwa wanawake.

Sera ya Jinsia Katika Vyombo vya Habari iliyotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) Novemba 2019, inavitaka vyombo vya habari kutoa haki na fursa sawa kwa wanawake na wanaume katika kuandika na kutangaza habari zao.

“Katika kuripoti masuala ya siasa, uchumi au vita, wanahabari watahakikisha sauti za wanawake zinasikika,” inasema sera hiyo na kuongeza: “Matumizi ya lugha inayoashiria ubaguzi au unyanyasaji wa kijinsia ni marufuku…”

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima anasema vyombo vya habari na hata viongozi wa dini, wanao wajibu mkubwa kubadili mitazamo hasi dhidi ya wanawake kuwa hawawezi na ni dhaifu katika uongozi.

Padri Kitima anasema: “Hii si kweli maana hata hapa nchini kuna ushahidi mwingi wa wanawake waliopata uongozi na kufanya vizuri katika nafasi zao akiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu (Sasa ni Rais wa Tanzania)…”

Katika moja ya warsha zilizowahusisha wanawahabari zilizoandaliwa na TEC na kufanyika Kurasini, Kitima anasema: “Wanawake ni watu wenye nguvu na uwezo wa uongozi na inawezekana kabisa kuwapo wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi, hivyo ni wakati sasa wa kuonesha umuhimu wa wanawake katika siasa na uongozi.”

Anaongeza: “Hata viongozi wa dini katika nchi na kati yao Wakristo na Waislam, wanao wajibu wa kukuza nafasi ya wanawake wenye uwezo na ujasiri.”

Ndiyo maana Tamwa na wadau mbalimbali wa usawa wa kijinsia katika mafunzo hayo wanasema vyama vya kisiasa havipaswi kuendeshwa na mfumo dume unaokandamiza, kubagua na kutoshirikisha wanawake katika siasa na uongozi wa umma kwa manufaa ya umma."

Washiriki wa mafunzo kwa wanahabari katika mradi wa Wanawake Wanaweza chini ya ufadhili wa UN-Women (Tanzania) wanahimizwa kuhakikisha mambo yanayowaweka wanawake nje ya siasa na uongozi yafanyiwe utafiti na kutatuliwa vizuri ndani ya vyama ili kufikia maendeleo ya kweli na usawa wa kijinsia.

Hayo ni pamoja na mazingira magumu katika kampeni kama kukosa uwezo wa mali na fedha.

Imebainika kuwa, mahali penye mizengwe dhidi ya wanawake, wengi hujikuta wanarudi nyuma na kusita kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki siasa. Lakini pale ambapo wanawake wanaungwa mkono kikamilifu hata na vyama vyao vya siasa, wamekuwa na nafasi kubwa ya kushirika na hatimaye kushinda katika uchaguzi katika kata na majimbo yao.

Ndiyo maana watu wengi wanataka tamaduni, mila, mitizamo, imani zinazodharau uwezo na ushiriki kamilifu wa wanawake katika siasa na uongozi ziepukwe hasa wakati wa uchaguzi.

Vyama viwaunge mkono wanawake na kuwasaidia kufanya kampeni, huku wanahabari nao wakitumia kalamu na kamera zao kuonesha taswira chanya na uwezo imara wa wanawake katika siasa na uongozi.

Columnist: www.habarileo.co.tz