Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuchangieni damu kuokoa uhai wa wajawazito

ASFEQW Tuchangieni damu kuokoa uhai wa wajawazito

Fri, 25 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

LEO ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Uchangiaji Damu kwa vituo mbalimbali nchini.

Uchangiaji huu ni maalumu kwa ajili ya kuokoa uhai wa wagonjwa mbalimbali, pia kwa wajawazito, pindi wanapokuwa wanajifungua au baada ya hapo.

Hakuna asiyejua umuhimu wa damu katika mwili wa binadamu, hususani kwa yule ambaye yuko kwenye nafasi ya kuongeza kiumbe mwingine duniani.

Katika kuhakikisha kampeni hiyo inafikiwa, Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS), umeandaa utaratibu wa kila mmoja kujitokeza na kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya akina mama wajawazito.

Ikumbuke kuwa damu haijawahi kutosha katika vituo mbalimbali vya afya, kwa kuwa mbali na wajawazito bado yapo makundi mengine ambayo kwa namna moja au nyingine hujikuta wakihitaji damu.

Aidha, mbali ya kwamba uchangiaji damu unakuwa na kampeni maalumu, lakini ifikie wakati kila mmoja mwenye vigezo vinavyokidhi kujitokeza mara kwa mara kwa kuchangia damu ambayo ni katika kuokoa uhai wa wahitaji mbalimbali wakiwemo wajawazito.

Kwa mujibu wa NBTS, kila Mtanzania mwenye umri unaoanzia miaka 18 na kuendelea hadi kufikia miaka 60 anao uwezo au nafasi nzuri kwa kujitokeza na kuchangia damu, ilmradi awe na afya njema.

Ikumbukwe kuwa hatua ya uchangiaji damu ni ya hiari na kwa mantiki hiyo, hakuna anayelazimishwa hata mmoja, lakini katika kuokoa uhai wa wengine ni muhimu ikawepo kukumbushana ili kuokoa ya wahitaji wakiwemo wajawazito na wengine.

Hakuna asiyejua kuwa wagonjwa wa ajali mbalimbali, wapo wanaokuwa na uhitaji wa damu na hata watoto wanaokua chini ya umri wa miaka mitano.

Hata hivyo, wapo wale wanaokuwa tayari kuchangia damu, lakini wakiwa na hofu kuwa muda huo, ndio itakayotumika kupimwa afya zao, jambo ambalo sio la kweli kwa kuwa kwa anayejitokeza kwa ajili ya kuchangia damu anapata fursa pia ya kuifahamu afya yake.

Ni muhimu kwa wale wenye vigezo vinavyokidhi, kujitokeza kuchangia damu wakati wote wanapopata nafasi hiyo wakitambua kuwa kufanya hivyo siyo tu watakuwa wanaokoa maisha ya watu wenye mahitaji, bali pia kujiwekea wao binafsi akiba lakini pia kulinda afya zao.

Kimsingi jamii inapaswa kuamka na kuwa mstari wa mbele katika kujua umuhimu wa uchangiaji wa damu kwa hiari na bila kushurutishwa na mtu ili kuisaidia NBTS kuwa na akiba ya kutosha ili kuzisaidia hospitali lakini pia vituo vya afya kwa kuzifanya kuwa tayari wakati wote anapotokea mhitaji kwa kuwa hakuna kiwanda cha kuzalisha damu.

Tunatambua kuwa changamoto kubwa inazozikabili hospitali nyingi nchini kwa sasa ni upatikanaji wa damu ya kutosha ili kuwasaidia watu wenye mahitaji, ambapo tatizo kubwa linalosababisha uhaba huo ni kutokuwepo kwa elimu ya kutosha kwa wananchi hao juu ya umuhimu wa kuchangia damu.

Katika kuhakikisha tatizo hilo linamalizika imefika wakati wananchi wao wenyewe kujitambua na kutambua kuhusu faida za kuchangia damu kila wakati ili kukabiliana na uhaba uliopo jambo ambalo pamoja na mambo mengine litazisaidia hospitali zetu na Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Damu salama kuwa na akiba ya kutosha ya damu hiyo.

Hivyo ni muhimu kwa wananchi kuitumia siku ya leo kujitokeza kwa wingi na kuchangia damu ili kukoa maisha ya wagonjwa wetu hospitalii na wajawazito, lakini pia kujiwekea akiba wao wenyewe kwa kuwa unaweza ukawa si mwenye mahitaji leo lakini kesho ukawa mhitaji.

Columnist: habarileo.co.tz