Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuchague amani, tuchague maendeleo

158414fb6402a8fa5ca9d8b14f23fafa Tuchague amani, tuchague maendeleo

Fri, 23 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ZIMEBAKI siku nne kufi kia siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Jumatano ijayo nchini kote. Uchaguzi huu utawezesha kupatikana viongozi watakaowatumikia Watanzania kwa miaka mitano ijayo.

Watanzania sasa wanao wajibu wa kuzingatia kuwa amani ni tunu ya maisha na ndio msingi mkuu wa maendeleo, hivyo wailinde amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi wakizingatia kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.

Kimsingi, hiki ni kipindi cha kila mmoja kujitathmini namna anavyojua thamani ya amani kwa jamii na gharama za kuitafuta inapoponyoka au kutoweka.

Lakini pia, kila mmoja wetu atumie nchi nyingine zilizochezea na hatimaye kuipoteza, kama kioo cha kujitazama na kujitathmini.

Ikumbukwe kuwa amani ni msingi imara wa maendeleo yoyote kwa binadamu, yawe maendeleo ya kiroho, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni tangu ngazi ya familia hadi taifa.

Tunapokaribia kuifikia siku ya uchaguzi, tukumbuke kuwa tukijisahau tukatumia uchaguzi kama bei ya amani, basi tujue watakaoangamia ni ndugu zetu yaani watoto, mama, baba, kaka, dada, shangazi, wajomba, marafiki, majirani, waumini katika dini zetu na wanachama wenzetu katika vyama na taasisi mbalimbali.

Ubaya wa ukosefu wa amani ni kwamba hao ndio watageukana na kumwagiana damu mithili wanyama waliolaaniwa.

Ninajua Watanzania karibu wote ni wacha Mungu, hivyo hakuna atakayekubali kupumbazika na kufungua geti la machafuko ili amani ipotee, eti kwa ajili ya uchaguzi na hasa kutaka kulazimisha watu fulani kuingia madarakani, japo hatujui wataingia kufanya nini wakiwa madarakani.

Twende katika uchaguzi tukijua kuwa kama tutakubali kudanganywa na kupumbazika kupoteza amani, waathirika wakubwa watakuwa ni watoto wetu, wagonjwa wetu, wazee wetu, wajawazito, watu wenye ulemavu na hata waungwana, maana mtego wa panya hukumba waliomo na wasiokuwamo.

Huo ndio ubaya wa kosa la kupoteza amani. Twende kupiga kura kuchagua viongozi huku tukikumbuka kuwa tukilewa mihemuko ya kisiasa na kuchezea amani, tunafungulia mataifa mengine milango ili waje kuturudisha katika zama za ukoloni; ukoloni wa kunyonywa na hata kurudishwa katika utumwa.

Tukumbuke mchezea zuri, baya humfika na ng’ombe hajui umuhimu wa mkia wake (amani) hadi unapokatika. Kwamba kwa kuzoea amani iliyodumu nchini, wengi wanaweza wasiithamini wala kujua thamani yake.

Lakini ikitoweka, ndipo kila mmoja ataitambua na wakati huo wale wasababishi wa upotevu huo wa amani na familia zao, watakuwa tayari wamekimbia kwenda wajuako.

Kukengeuka hadi kuruhusu amani ipotee, kutatufanya tujute kuona uchumi ukiporomoka na wengine kuja kuchuma utajiri na rasilimali zetu,hivyo kuangusha uchumi tulioujenga kwa miaka mingi na badala yake tutajikuae kwenye makucha ya watu.

Hilo, Watanzania hatulitaki na tusiliruhusu. Huu ni wakati muhimu kuliko mwingine wowote. Viongozi wa dini wazidi kuombea amani na Watanzania wasikie viongozi hao wa dini, jamii, serikali na wenye mapenzi mema wanaadilisha nini na kufuata.

Tunapoelekea uchaguzi, tukiona mtu wa kada yoyote anahamasisha au kushawishi vurugu, kila mmoja ageuke na kuitazama familia yake; amtazame mwanaye, mama yake, baba yake, mke wake, mume wake, mjomba au shangazi yake atakuwa wapi; hadi lini na kwanini.

Ndiyo maana ninasema twende kwenye uchaguzi tuchague amani, tuchague maendeleo

Columnist: habarileo.co.tz