Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuache kumjaza upepo clement mzize

Clement Mzize Tinhoooo Straika wa Yanga, Clement Mzize

Thu, 12 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Naona Tanzania tumeanza ule mchezo wa Waingereza. Mchezo wa kuongeza sifuri mbele. Mchezo wa kumjaza mtu upepo. Mchezo wa kumpa mtu ukubwa ambao bado hauonekani.

Mchezo huo ndiyo uliifanya Manchester United watumie pesa nyingi kumsajili Harry Maguire wakidhani ni Rio Ferdinand.

Ni mchezo huo huo ndiyo ulifanya Jadon Sancho aonekane ni kama Kyllian Mbappe!

Clement Mzize ni mchezaji wetu mzawa. Mzize wote tunamjua vizuri bado ni mbichi kwenye soka letu. Bado ni mchezaji anayepaswa kuwa namba mbili kwenye idara ya ushambuliaji.

Hata Yanga wenyewe hawaamini kama Mzize ameshakomaa kiasi cha kutegemewa sana na timu, ndiyo maana wamemleta Prince Dube.

Nikisikiliza tetesi anazohusishwa Mzize na uwezo wake, nabaki mdomo wazi. Nahisi kuna mahali tunaongeza sifuri mbele. Nahisi tumeanza mchezo wa kuwajaza wachezaji wetu kama Waingereza wanavyofanya.

Siku za karibuni kumekuwa na tetesi nyingi sana za Usajili zikimihusisha na klabu kubwa Afrika. Ni kweli ni mchezaji mzuri lakini tupunguze basi kuongeza sifuri.

Ukifika leo nchini, unaweza kusema Mzize ndiye mshambuliaji bora. Nadhani tumeanza michezo ya Waingereza. Nadhani tumeamua sasa kuanza kuongeza sifuri kwa wachezaji wetu.

Huu ni msimu wa tatu tunamshuhudia Mzize. Ni mchezaji mzuri sana lakini hajawahi kufunga hata mabao 10 ya ligi, hajawahi kufunga mabao ya kuibeba timu kwenye mazingira magumu na hana mabao mengi yanayokumbukwa na wengi.

Natamani tungeacha mchezo wa kuongeza sifuri. Natamani tungeacha mchezo wa Waingereza. Mzize bado ni mchezaji ambaye kwenye nafasi tano, anaweza kufunga bao moja. Bado anakua.

Kuna watu wameanza kumpa jina la Drogba. Ni vizuri mtu kuwa na ndoto kubwa, lakini ni vizuri zaidi kuwa na ndoto zenye uhalisia. Tuna kijana anaitwa Kelvin John. Ni Mtanzania mwenzetu. Ni kijana wetu na anacheza ligi kuu Denmark.

Wakati anaanza kuchipukia, alipewa jina la Mbappe. Hadi leo hakuna mfanano wowote.

Kuna kijana anaitwa Geofrey Mwashiuya. Aliwahi kusajiliwa na Yanga na akapewa jina la Lunyamila, hadi amepotea hajawahi kufanania na Edibily Lunyamila mwenyewe.

Hakuna urahisi kwenye kufanikiwa. Mafanikio ni mchakato. Wote tunatamani kuona Mzize anacheza klabu kubwa Afrika na dunia, lakini ni suala la muda. Kwa sasa anapaswa kuendelea kupewa nafasi ya kucheza ili azidi kukua.

Bado ukimtazama kwenye ligi na mchnago wake kwenye timu yetu ya Taifa, Taifa Stars huoni ukubwa wake. Ni kijana mdogo wa kutegemewe baadaye.

Tuache kumjaza Mzize. Bado hajafanya chochote cha kukumbukwa kwenye klabu yake ya Yanga na timu ya Taifa, Taifa Stars. Mshambuliaji wa aina yake,

walau anapaswa kufikisha mabao kuanzia 10 kwa msimu na kuisaidia Taifa Stars kufuzu kwa fainali za Afcon akiwa kinara wa mabao. Lakini kwa huu ukubwa tunaompa nje ya uwanja, hausaidii chochote.

Natamani angebakia tu kuitwa Clement Mzize hadi atakapofanya makubwa ndiyo mtandao wa Drogba uje wenyewe. Kila nikimkumbuka Didier Drogba Shughuli yake na Mzize, sioni mfanano kabisa. Kuanzia kwenye mwonekano hadi uwezo uwanjani. Ni mbingu na ardhi.

Msimu uliopita Yanga ililazimika kumtumia zaidi Stephen Aziz Kİ kama mshambuliaji wa mwisho kwa sababu Mzize alikuwa hatoshi. Msimu huu wamekuja na Jean Baleke na Prince Dube kuongeza nguvu kwenye eneo hilo hilo. Sio kwa bahati mbaya.

Huko nyuma tumewahi kuwa na tetesi nyingi sana za uongo na hazikusaidia soka letu. Nadhani Mzize bado hajakomaa vizuri.

Aendelee kupambana Yanga na awe na msimu mzuri wenye namba. Shida kubwa ya mshambuliaji, hata kama ana kıla şifa akikosa mabao inampunguzia thamani.

Bado mabao ya Mzize kulinganisha na nafasi anazotengenezewa ni machache mno. Bado anahitaji kukua. Bado anahitaji kuongeza namba za mabao yake.

Tuache kuongeza sifuri kwenye Ubora wa Mzize. Ni mtoto wetu wa Kitanzania lakini bado hajakomaa sawa sawa. Huu unapaswa kuwa msimu wake wa kukomaa akiwa na Yanga.

Huu unapaswa kuwa msimu wake wa kuonyesha maajabu akiwa na Taifa Stars maana Mbwana Samatta na Simon Msuva hawapo kikosini. Kama kuna kitu hakijawahi kudanganya, basi ni namba.

Tatizo la Simba na Yanga kwenye soka letu, zinaweza kukupa şifa hata usizokuwa nazo. Ni mabingwa wa propaganda. Nawaheshimu kwa hilo. Yanga inashiriki michuano mikubwa Afrika na Tanzania msimu huu. Ni muda wa kuona kiwango cha Mzize. Hizo Wydad Casablanca na Mamelod Sundowns hazina muda wa kupoteza. Hazitaki kuwa na mchezaji ambaye hajakomaa.

Tumeshuhudia wachezaji wengi kutoka Tanzania walivyoteseka walipokwenda kwenye timu kubwa Afrika. Tuache kumjaza upepo, Mzize bado sio mchezaji tishio. Mzize sio kabisa wa kumfananisha na Drogba.

Haya mambo ya Waingereza kuongeza sifuri hayatusaidii. Wachezaji wengi waliotamba kwenye ligi yetu, wamefulia walipoenda nje. Miaka ya hivi karibu labda ni Mbwana Samatta, Simon Msuva na Fiston Mayele ndiyo wameonekana kung’aa na klabu kubwa Afrika. Chama, Miquessone, Bwalya na wengine huko wanarukaruka tu.

Bado Mzize anapaswa kujijenga hapa hapa. Hizo tetesi za Kiingereza mimi sioni kama zina tija. Tümpende tu kama kijana wetu lakini tusimdanganye. Bado ana safari ndefu ya kukua.

Bado anahitaji kuwa chaguo la kwanza Yanga. Habari za kuona ni kama Drogba ajaye, tuache kumdanganya kijana wetu. Ana kazi ya kuibeba Yanga Kimataifa msimu huu. Ana kazi ya kuibeba Taifa Stars msimu huu kwenda Afcon.

Akamilishe kwanza hayo mawili ndipo turudi mezani kuzungumza.

Columnist: Mwanaspoti