Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Tiba asili zinaimarisha sekta ya tiba, uchumi’

D169d120a7b559f6bd74a6a212275b73 ‘Tiba asili zinaimarisha sekta ya tiba, uchumi’

Thu, 4 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KWA kipindi kirefu, sekta ya afya nchini imekuwa ikitegemea tiba rasmi, tiba asili na tiba mbadala katika kusimamia afya za Watanzania.

Hata hivyo, tiba asili imekuwa ikionekana kutopewa kipaumbele inachostahili licha ya ukweli kwamba imekuwepo siku zote ikiwasaidia Watanzania hata kabla ya ujio wa tiba za kisasa baada ya ukoloni.

Ni jambo la kupongeza kwamba katika siku za hivi karibuni upepo unaonekana kubadilika kwa asilimia kubwa kwa Watanzania kuanza kuamini tiba hii na hata kuanza kuonekana kwenye maduka ya dawa.

Lakini wakati tiba asili ya Tanzania ilikuwa ikidharauliwa na baadhi ya wananchi, tiba asili kutoka mataifa kama India na China zilikuwa zinaonekana kupewa kipaumbele na Watanzania hao hao!

Hali ilikuwa hivyo, licha ya kuwepo kwa taasisi mbalimbali nchini ambazo zimekuwa zikifanya tafiti za kisayansi kuhusu tiba asili.

Shukrani za pekee zimwendee Rais John Magufuli, ambaye amechangia sana katika kuhuisha tiba za asili, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na ugonjwa wa corona ambao mpaka sasa haujapatiwa tiba rasmi na tiba za kisasa.

Kupitia tafiti hizo za tiba asili, mintarafu suala zima la mapambano ya ugonjwa hatari wa corona, serikali imekubali kurasimisha dawa zinazoonekana kuwa na tija katika sekta ya tiba, ikiwa ni pamoja na kupitia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba (NIMR).

Kwa upande wa tiba asili zinazosaidia wagonjwa wa corona, tayari serikali imepitisha dawa tano na mafuta tete ya aina mbili.

Dk Paul Kazyoba kutoka NIMR anaipongeza serikali ya awamu ya tano kwa namna ilivyoamua kutoa kipaumbele katika kuhakikisha tiba asili inatoa mchango wake adhimu katika kada ya tiba rasmi.

"Hili ni jambo la kihistoria, tangu mwaka 1970 wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, kabla ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, serikali iliona umuhimu wa tiba asili katika kusaidia tiba rasmi na hivyo kuanzisha taasisi ya utafiti wa tiba asili ikiwa chini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili," anasema.

Anaongeza: "Mwaka 79 baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Utafiti wa Tiba la Jumuiya hiyo lilivunjika na nchi husika zikagawana vituo."

Anasema huo ndio ulikuwa mwanzo wa kuanzishwa kwa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba (NIMR) kwa mujibu wa sheria namba 23 ya Bunge ya mwaka 1979.

Anasema taasisi hiyo ilipewa jumla ya majukumu 10, jukumu la pili likiwa ni kusimamia na kusaidia utafiti wa tiba asili pamoja kurasimisha dawa zinazopatikana na kuthibitishwa katika tafiti hizo.

Dk Kazyoba anasema ilipofika mwaka 2000 idara ya utafiti wa tiba asili ilianza rasmi chini ya taasisi ya NIMR, serikali ikiwa na mchango mkubwa wa kuhakikisha inadhamini tafiti mbalimbali katika kada hiyo kwa kutoa fedha na kuanzisha kiwanda cha kutengeneza dawa za asili.

"Nayasema haya kwa sababu nataka kukuthibitishia jinsi serikali inavyothamini tiba asili na kuipa kipaumbele. Katika kuthibitisha umuhimu wa tiba asili sheria ya tiba asili na tiba mbadala ilianzishwa mwama 2002 ikifuatiwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ili kurasimisha na kudhibiti kada hiyo," anasema Dk Kazyoba.

"Mwaka 2007 hadi 2017 serikali iliendelea kufanya maboresho katika kada hiyo na mwaka 2017 serikali ilitoa Sh milioni 18 ili kuimarisha na kuendeleza kiwanda cha kuchakata dawa za asili kilichoanzisha mwaka 2010.

"Kupitia uwezeshaji huo tumeweza kuingia moja kwa moja katika kusaidia tiba rasmi na kwa sasa tuna mitambo ya kisasa kutoka China na tumeshaandaa jengo jipya kwa ajili ya kuzalisha dawa zinazotokana na mimea asili," anasema.

Anasema NIMR pia wamepokea Sh milioni 400 kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya ndani ya jengo la kiwanda na kukamilisha mahitaji kwa ajili ya utafiti wa tiba asili na kwamba hizo ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha tiba asili inatoa mchango mkubwa katika sekta ya matibabu.

"Toka mwaka 2017 tulipoanza kupokea fedha kutoka serikalini kwa ajili ya tiba asili mpaka sasa tumeshapokea takribani Sh bilioni moja na mchakato wa kukamilisha kiwanda cha tiba asili uko katika hatua nzuri," anasema Dk Kazyoba.

Anaongeza kuwa kada hiyo katika siku za usoni itachangia kuimarisha sekta ya tiba na uchumi kwa ujumla kwani dawa zitakazozalishwa zitauzwa.

Katika kuthibitisha na kuonesha kuwa anathamini mchango wa tiba asili, Rais John Magufuli wakati huu ambao dunia imeingia katika janga la corona anahimiza Watanzania kuwa pamoja na kuchukua tahadhari katika kujikinga na ugonjwa huo.

Amekuwa pia akiwahimiza Watanzania kutumia dawa za asili alimradi ziwe zimethibitihwa na Mkemia Mkuu.

Baadhi ya dawa hizo zinazotengenezwa nchini ambazo Rais Magufuli amewataka Watanzania kunywa ni pamoja na Nimrcaf na Covidol.

Amewataka pia watanzania kutodharau tiba ya kujifukiza kulingana na mwongozo unaotolewa na NIMR ili kupambana na janga hili la corona.

Pia Waziri wa Afya, Dk Doroth Gwajima ameungana na Rais Magufuli kwa kutembelea NIMR na kunywa dawa ya Nimrcaf, kisha anawasisitiza Watanzania kujitokeza kutumia dawa hiyo kwa kununua au kutengeneza wenyewe kwa kufuata mwongozo wa NIMR.

Mbali na Nimricaf na Covidol, dawa zingine zinazosaidia tiba ya corona zilizopitishwa na serikali ni Bingwa, Planet++, Covotanza huku zile za mafuta tete zikiwa Bupiji na Uzima.

Columnist: www.habarileo.co.tz