Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tembo hutumia kucha kuweka kumbukumbu

33a48b821e7d438b78ba173ad4f32ee9 Tembo hutumia kucha kuweka kumbukumbu

Thu, 27 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TEMBO ni mnyama anayetambulika kwa ukubwa wa umbo hivyo kuwa na maadui wachache porini. Hutumia umbo lake kuwatisha wanyama wengine na kuogopwa.

Tembo wanatajwa kuwa miongoni mwa wanyama wachache wenye ukaribu na familia na marafiki wanaweza kuwatambua mama zao, shangazi, bibi, binamu na watoto wa dada na wakati mwingine hata baba zao. Wana uwezo wa kujenga urafiki na tembo wasiohusiana nao.

Kwa kawaida, tembo dume wanaishi peke yao na wanakutana na tembo jike wanapojamiiana au kukaa nao kwa muda mfupi, baadaye wanatengana tena. Wasio na wenza huishi kwenye kundi peke yao na kujitenga na wengine.

Tembo wana uwezo wa kuonesha hisia za mapenzi kwa wenza wao wa zamani ingawa si rahisi baba kutambua watoto, isipokuwa kama baba ataonesha tabia fulani ya zamani.

Hawasikii vizuri, lakini ni wataalamu wa kunusa. Macho yao hayaoni vizuri wakati wa kula na badala yake, hutumia mkonga wao kunusa majani kama yanafaa kula au la.

Tembo ni miongoni mwa wanyama wanaoweza kuhuzunika pindi mwenzao anapokufa. Huweka kumbukumbu. Inapotokea siku wamepita alipofia mwenzao, hutulia kwa muda kumkumbuka.

Hupendelea kutembea kwa makundi kama familia, wa nyuma hushika mkia wa mbele yake ili wasipoteane.

Pamoja na ukubwa wake, tembo akitembea ananyata haweki vishindo, pia kwenye mguu wake kuna kucha inayotunza kumbukumbu juu ya sehemu au njia alizopita.

Wanyama hawa hawapendi kelele ndiyo maana watu wanapokwenda mbugani kutazama wanyama, huambiwa wasipige kelele wanapokaribia wanyama hawa. Kutokana na kuchukia kelele, wawindaji hutumia hasira zake pindi apigiwapo kelele na kuchimbiwa mashimo ili aingie.

Tofauti na wanyama wengine, tembo huwasiliana kwa kutumia vishindo vya miguu yao ambavyo kwa masikio ya mwanadamu, havisikiki lakini wenyewe huwa na uwezo wa kuvihisi na mawimbi yake husafiri umbali mrefu zaidi ambapo kuna namna huvitoa kulingana na tukio husika, mfano hali ya hatari ama upatikanaji wa maji.

Kama tembo mmoja ataonekana anakaribia kupoteza maisha, tembo wote wataacha kutembea, watakaa sehemu moja kwa muda fulani.

Iwapo tembo huyo mgonjwa au mzee atapoteza uhai, watakaa kwenye eneo hilo kwa siku kadhaa wakizunguka maiti na kuonekana wakimpa heshima za mwisho marehemu.

Wakiwa kwenye safari yao wakakuta tembo mwenzao kafa, watakusanyika hapo na kukaa naye kwa siku kadhaa. Watafanya hivyo hata kama hawamfahamu. Watakaa hapo kimya na kuugusa mwili kwa mkonga wao kama vile wanatoa heshima zao.

Imeandikwa na MAULID AHMED kwa msaada wa mtandao wa intaneti.

Columnist: habarileo.co.tz