Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tathmini ifanywe kuadhimisha Siku ya Wanawake

Bc7b4e82df15983afe3b2640beed4801.png Tathmini ifanywe kuadhimisha Siku ya Wanawake

Mon, 1 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MACHI 8 kila mwaka ni maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Wanawake Duniani.

Maadhimisho haya hufanywa, kwa lengo la kuhimiza na kupiga vita vitendo vyote vya kikatili dhidi ya wanawake na kuhimiza masuala ya usawa wa jinsia.

Katika kuadhimisha siku hii hapa nchini, serikali miaka kadhaa iliyopita iliamua iwe inasheherekewa kitaifa kila baada ya miaka mitano ; na katika ngazi ya mikoa, iwe inaadhimishwa kila mwaka.

Hatua hiyo ilifikiwa ili kutoa nafasi kwa serikali kufanya tathmini ya hatua zilizochukuliwa kuhakikisha ukatili unakomeshwa na jitihada zinafanywa kuwawezesha wanawake na kulinda haki na usawa.

Hayo na mengine mengi yahusuyo haki za wanawake na watoto ni mambo ya msingi ya kuangalia wakati huu dunia inapopambana na vita dhidi ya ukandamizaji, si tu wa wanawake, bali pia makundi yote katika jamii hasa yale ambayo sauti zao hazisikiki.

Tukiangalia hapa nchini, tumeshuhudia jitihada mbalimbali za serikali zikiendelea kuboresha ustawi wa makundi hayo yaliyoachwa nyuma na hasa kundi la wanawake, ambao walidharaulika na kuonewa na kunyimwa haki za msingi kama elimu, lakini kwa sasa wanapata, kutokana na sheria na sera kuendelea kuboreshwa.

Kwa mfano, Serikali hivi sasa inatoa elimu bila malipo, hatua ambayo imetoa nafasi pia kwa watoto wa kike hasa kutoka familia masikini kupata elimu.

Hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa wilayani Ruangwa, alisisitiza kuhusu ujenzi wa shule za bweni za wasichana nchini ili kuwezesha kundi hilo, kusoma bila vikwazo.

Hakuna asiyefahamu katika familia, jamii na hata Taifa, nguzo kuu ya maendeleo ni mwanamke na hiyo inatokana na ukweli kwamba mwanamke anabeba mambo mengi, kwani ndiye mlezi na mwangalizi wa familia, hivyo kama atakandamizwa ni wazi kwamba hakutakuwa na maendeleo.

Tumeshuhudia serikali za awamu zote hapa nchini, zikipiga vita unyanyasaji wa wanawake na watoto, kwa kufuta ama kuboresha sheria zilizokuwa kandamizi ili kuhakikisha haki za wanawake zinalindwa ikiwamo maboresho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, iliyokuwa ikitoa nafasi kwa mtoto wa kike wa miaka 14 na 15 kuolewa.

Aidha, tumeshuhudia wanawake wakiwezeshwa na wengi wakipewa nafasi katika serikali. Hili ni jambo jema. Tumeona nafasi kubwa za utawala wakipewa wanawake, si kwa kupendelewa, la hasha! bali ni kutokana na kuwa na uwezo wa kufanya kazi hizo. Na waliopewa nafasi, wengi walizitendea haki.

Mfano mzuri ni Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, mwanamke shupavu anayedhihirisha kwa vitendo kuwa wanawake wanaweza. Pia Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Zena Said ni mfano wa hili.

Tumeshuhudia mengi yakifanywa na wanawake wenye nafasi na hayo ni machache tu yamedhihirisha kuwa hakuna linaloshindikana, kama kundi hilo wakiwezeshwa.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, tathmini ifanywe kuangalia hatua zilizofikiwa katika kuondoa aina zote za ukatili, ubaguzi na kuhakikisha haki zao zinalindwa.

Maadhimisho haya yawe na matokeo chanya. Tathmini iliyofanywa miaka iliyopita, itolewe ili iainishe maeneo yanayohitaji kuboreshwa ili kuhakikisha haki na maslahi ya wanawake yanalindwa.

Columnist: habarileo.co.tz