Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tanzania ya Samia michezoni

Samia Suluhu Sports.jpeg Rais Samia Suluhu Hassan

Sat, 3 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Moja ya nyakati nitakazozikumbuka kwa muda mrefu katika utumishi wangu kwenye michezo ni Aprili 4, 2017.

Nina kila sababu za kuikumbuka siku hiyo iliyokuwa ni mara yangu ya kwanza kufika nyumbani kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na kuketi naye kwenye meza ya chakula alichokiandaa.

Kwangu mambo ya kukumbuka zaidi yalikuwa mawili; moja nilivutiwa kumuona Makamu wa Rais kwa upole akiwakaribisha mezani na kuwapakulia chakula vijana wa Timu ya Taifa ya soka ya umri chini ya miaka 17 waliokwenda kumuaga ili kwenda kambini Morocco kujiandaa na fainali za Afrika (Afcon U-17) zilizofanyika Gabon.

La pili ni tukio la kusikitisha la kuzuiliwa na madalali wa mamlaka ya mapato kwa basi lililokuwa linawapeleka Serengeti Boys kwenye chakula cha jioni kilichoandaliwa na Makamu wa Rais kuwaaga vijana hao katika kilichodaiwa kuwa shirikisho lilikuwa na deni la kodi.Pamoja na nasaha alizowapa vijana,Makamu wa Rais alizielekeza mamlaka husika kutumia busara katika kudai mapato na hivyo kesho yake basi hilo liliachiliwa. Matukio hayo nayakumbuka kama vile jana lakini pia nikiongea na baadhi ya vijana hao, ambao kwa sasa ndio wanatengeneza uti wa mgongo wa timu ya taifa ya wakubwa (Taifa Stars), bado wanaikumbuka siku hiyo.

Michezo ni sekta muhimu katika dunia ya sasa. Michezo inatoa ajira, huingiza kipato, huingiza kodi, hujenga afya ya jamii, hujenga mahusiano katika jamii, husaidia ukuaji kielimu kwa watoto na vijana na ni nyenzo muhimu sana katika diplomasia ya kimataifa.

Sekta ya michezo ni moja ya sekta za kiuchumi zinazokua kwa kasi sana duniani. Mathalani, katika nchi ya Marekani (USA) michezo huingiza takribani Dola 15 bilioni kwa mwaka kama pato la moja kwa moja kwa watu takribani 5, 000,000. Michezo inachangia karibu asilimia 2 katika pato ghafi la taifa (GDP) .

Nchi nyingi zinazoendelea, hasa za kiafrika, huichukulia michezo si shughuli yenye umuhimu wa pekee katika nyanja za maendeleo ya taifa. Mathalani hapa nchini tangu baada ya Uhuru Awamu ya Kwanza ya Serikali iliichukulia michezo kama burudani na wanamichezo walifanya kwa ridhaa wakitegemea zaidi vipaji. Michezo iligharimiwa zaidi na serikali pamoja na michango ya wanachama na wapenzi wa michezo. Katika miaka ya 1980 halikuwa jambo la ajabu nchi kujitoa au kutuma washiriki wachache kwenye mashindano ya kimataifa kwani lilipokuja suala la kubana matumizi michezo ilikuwa ni muanga namba moja. Hali ilikuwa siyo tofauti sana mpaka miaka ya karibuni.Hali hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na kutokuwepo na uelewa wa kutosha na pia utamaduni wa kuiona michezo kama suala la kupitisha muda tu. Hayo yote pamoja na sababu za kiuchumi yamechangia katika kukosekana kwa utashi wa kisiasa katika uongozi wetu.

Chini ya Samia

Rais Samia alichukua uongozi wa nchi wakati dunia ikiwa kwenye apambano dhidi ya Ugonjwa wa Uviko. Uchumi wa dunia ulikuwa katika hali mbaya na sekta ya michezo kimataifa na hapa nyumbani ilikuwa katika wakati mgumu. Mwaka mmoja baadaye tunaona sekta binafsi ikijiingiza kwa nguvu katika uwekezaji. Unaweza kuona mathalani katika soka namna makampuni binafsi kama GSM, METL, Azam Pay TV na mengine mengi yakishirikiana na yale ya umma kama CRDB, NMB n.k yanavyowekeza kwa nguvu katika mchezo huo. Hii ni kutokana na serikali kuviacha vyama vya michezo, klabu na makampuni kufanya shughuli zao kwa uhuru. Wote tu mashahidi namna wafanyabiashara waliojihusisha na udhamini wa michezo walivyopata misukosuko kidogo kiasi cha kupunguza udhamini au kujitoa kabisa.Chini ya Rais Samia nchi inasogea zaidi kutoka kwenye michezo kutegemea zaidi ufadhili kuelekea kwenye kuwa na udhamini na miradi ya kibiashara.

Fursa nyingine zinazoonekana chini ya Rais Samia ni kuondolewa kodi kwa vifaa vya miundombinu ya michezo kama nyasi bandia, mpango wa serikali kukarabati na kujenga viwanja na pia kutengeneza kumbi kubwa za Sanaa za maonyesho na filamu.

1. Program za vijana

Taifa linatakiwa kuwa na programu nyingi za michezo na sanaa kadri inavyowezekana. Michezo mashuleni ni jambo la lazima kwa jamii yoyote iliyo makini na maendeleo ya michezo. Serikali na vyama vya michezo wanatakiwa kuwekeza kwa wataalamu wa ufundi na miundombinu ya michezo kama kweli tunataka kesho yenye furaha na fahari. Hakuna taifa lililofanikiwa katika michezo na Sanaa bila kuwa na programu nzuri na kubwa za vijana kuanzia ngazi za chini (grassroot) hadi professional.

2. Kimataifa

Si ajabu kusikia nchi za Uingereza na Marekani zilivyochukizwa na Fifa chini ya Rais wake Joseph Blatter baada yakupigwa vikumbo na Russia na Qatar katika kuandaa Kombe la Dunia 2018 na 2022.

Inawezekana chuki hiyo ina imechangia anguko la Sep Blatter Fifa. Afrika inamkumbuka Blatter kwa kuizawadia Kombe la Dunia 2010 ikiwa ni miaka mine tangu Afrika Kusini iporwe nafasi hiyo na Ujerumani. Vita ya kuandaa mashindano makubwa kama Olimpiki na Kombe la dunia haijawahi kuwa ya kitoto. Hii ni kwa sababu mataifa yanajua umuhimu wa mashindano kwa uchumi na diplomasia ya nchi.

Mwaka 2014 Caf ilihamisha mashindano ya Afcon ya 2015 kutoka Morocco baada ya kujitoa kwa ilichodai kuwa tishio la Ugonjwa wa Ebola hivyo alikuwa anatafutwa mwandaaji mbadala; Rais Jakaya Kikwete alitamani tuchukue nafasi hiyo na alitoa ruhusa kupelekwa maombi Cairo.Tulipokwenda CAF tuliambiwa kama nchi hatuna uzoefu wa kuandaa mashindano yoyote ya Bara la Afrika. Mashindano yakaenda Guinea ya Ikweta. Badala yake, tulipewa nafasi ya kuandaa Afcon ya vijana chini ya miaka 17 kwa mwaka 2019 ili tupate uzoefu wa kuandaa.Kimsingi sasa tunaweza kuandaa mashindano ya Afrika tukipita vigezo vingine kama viwanja, miundombinu ya usafiri na mahoteli. Mashindano ya kimataifa si tu yataitangaza nchi bali pia yatakuwa na athari chanya katika biashara na uchumi kwa ujumla.Pamoja na mashindano, bado nchi inaweza kutoa idhini na hata ardhi kwa vyama vya kimataifa vya michezo kuwa na makao makuu hapa nchini.Tunaweza pia kuanzisha mashindano kama Serengeti Open, Zanzibar Open kwa tenisi na gofu au hata marathoni za kimataifa ambazo pia zitachangia kukuza utalii.

3. Mashindano kimataifa

Rais wa nchi ni raia namba moja na kielelezo cha taifa. Hata hivyo hakuna Rais aliyewahi kuitangaza nchi kimataifa kufikia michezo inavyotangaza hata angetoa hotuba tamu kiasi gani pale kwenye majengo ya umoja wa Mataifa, New York. Kama nchi itawaandaa vijana wengi na kupata nafasi ya kushiriki mashindano na matamasha mengi kimataifa haitakuja kujutia gharama zilizotumika. Jiulize ni watu wangapi wanajali kumjua Rais wa Brazil, Senegal au Argentina? Lakini angalia wanasoka na timu zao za taifa zinavyotangaza mataifa hayo.Ni wakati mwafaka sasa kwa serikali kuongezea nguvu kazi zinazofanywa na vyama na mashirikisho ili vijana wetu walio katika sanaa na michezo waweze kujionyesha na kufanya vizuri kimataifa.

4. Michezo na utalii

Ni wakati mwafaka kwa serikali kuangalia upya muundo wa wizara ya utamaduni na michezo ili iweze kufanya kazi chini ya wizara inayoshughulika na utalii. Hakuna namna ambayo utalii unaweza kutenganishwa na michezo na utamaduni. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikiuweka utalii sambamba na michezo na utamaduni. Maliasili ingeweza kuunganishwa na mazingira na kufanya vizuri tu. Onyesho la Filamu ya Royal Tour ambayo Rais Samia pia ameshiriki linathibitisha utalii uko kwenye burudani zaidi kuliko shughuli za uhifadhi wa mazingira.

5.Utashi wa kisiasa

Utashi wa kisiasa huamua mkazo wa kisera uwekwe wapi na panapo utashi wa kisiasa serikali huziamsha hata sekta binafsi kuchangia maendeleo ya sekta husika. Kitendo cha Makamu wa Rais wa nchi kuwapakulia chakula Nickson Kibabage, Kibwana Shomari, Israel Mwenda, Dickson Job ni dalili ya utashi wa kisiasa. Na hata walipotolewa na Niger katika kufuzu Kombe la Dunia, vilio vilitawala kwenye chumba cha kuvalia wakikumbuka ahadi waliyotoa Makamu wa Rais.

Serikali ya Rais Samia imeonyesha mwanga na utashi wa kutosha katika kuleta maendeleo ya michezo, sanaa, utalii na utamaduni.

Columnist: Mwanaspoti