Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Takwimu haziongopi, JPM atashinda kwa kishindo

0a8a3aa529a601960f696d26e56eb31c Takwimu haziongopi, JPM atashinda kwa kishindo

Wed, 28 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MWANAHARAKATI mmoja anayejiita Mimi Mwanakijiji, jana ‘alitupia’kwenye mtandao wa Jamii Forum kwamba: “Naamini kuwa Rais John Magufuli anastahili kupewa nafasi nyingine ya kuliongoza Taifa letu kwa miaka mingine mitano. Hoja zinazotolewa hazijatosha kuwafanya Watanzania wengi kutokumuunga mkono. Ushindi wake utakaribia asilimia 80.”

Mwanakijiji ambaye ni dhahiri kabla ya kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tatu alikuwa akiunga mkono upinzani akaendelea kusema: Lissu atapigiwa kura na watu wengi vilevile ana kazi kubwa zaidi ya kuuelekeza upinzani kuelekea 2025. Hadi hivi sasa hajajaribiwa kama kiongozi mkuu wa upinzani, anaenda kujaribiwa sasa.”

Anachosema Mwanakijiji ni kweli kabisa kwani uchaguzi ni hesabu na hizo hesabu ndiyo ushindi wa chama chochote kwenye uchaguzi. Kihesabu, Magufuli atashinda zaidi ya asilimia 80 na kama utafuatilia makala haya hadi mwisho utaliona hilo dhahiri.

Hesabu na namba hazidanganyi. Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jumla ya Watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura ni 29,188,347 ambao hawa wataweza kupiga kura siku ya Jumatano Oktoba 28.

Kwenye idadi hiyo ya wapigakura, CCM ina jumla ya wanachama 17,000,000 ambao takribani wote wamejiandikisha na wako tayari kupiga kura Oktoba 28.

Ni rahisi kuamini kwamba wale wachache wa upinzani tunaowaona hata kwenye mikutano na mitandao hawakujiandikisha na hasa kuboresha majina yao kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kutokana na kosa walilolifanya wapinzani Novemba mwaka jana kwa kukususa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Wafuasi wengi wa upande huo walikata tamaa na wengi wamedhihirisha waliamini hata uchaguzi mkuu wa mwaka huu upinzani utasusa pia na hivyo hawakuona sababu za kujiandikisha!

Lakini ukiachana na hao milioni 17, CCM ina mtaji wa wafuasi wapya ambao wamejiandikisha hivi karibuni wapatao milioni tano.

Ukipiga hesabu hapo unaona chama tawala kina wapigakura milioni 22 tayari ambao ni wana CCM na hapo unagundua kabla hata ya CCM kuingia kwenye kampeni ilishashika ushindi mkononi wa zaidi ya asilimia 78.

CCM inaingia kwenye ulingo huu kwenda kuzitafuta kura za watu milioni saba pekee. Hii pia inadhihirishwa na ukweli kwamba CCM ndicho chama pekee kilichoweka madiwani kila kata na wagombea ubunge kila jimbo.

Hata ukiondoa wagombea wa upinzani walioenguliwa kwa kukosea masharti, bado vyama vya upinzani, kikiwemo Chadema havikuwa na uwezo wa kusimamisha madiwani nchi nzima wala wagombea ubunge nchi nzima.

Taarifa zinaonesha kwamba kabla ya baadhi ya wagombea ubunge wake kupingwa, Chadema ilikuwa na wagombea 211. Jumla ya majimbo ya uchaguzi ni 264 na hivyo Chadema ilipotoa orodha yake ya tatu inayoonekana kwamba ndio ilikuwa ya mwisho, ilikuwa imeshindwa kusimamisha wagombea ubunge 53!

Sasa angalia hizo kura milioni saba zinavyotafutwa kihesabu na kisayansi. Piga hesabu utekelezaji mkubwa wa Ilani ya CCM na ahadi zote ambazo Dk John Magufuli alizotoa mwaka 2015, weka kampeni za kistaarabu na kisayansi zilizojaa hoja, ushawishi na uhudhuriaji wa watu wengi ambazo zimepigwa na CCM kwa kuhusisha vinara watatu wakuu, Mgombea wake wa urais Dk Magufuli, mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan na mjumbe wa kamati kuu, Kassim Majaliwa.

Hawa waligawana nchi kwa kila mmoja kushambulia maeneo tofauti tofauti ya nchi ambako kote kumepigwa kampeni kubwa sana.

Hapo ongeza na timu nyingine ya viongozi wastaafu na waandamizi wa CCM ambao nao wamepita kila kona kusaka kura. Wamepita kila sehemu kusaka kura ukilinganisha na vyama vingine ambao walikuwa wanashinda mitandaoni tu kupotosha na kusema watu.

CCM imeshawishi mamilioni kwa mamilioni ya Watanzania kuwachagua huku wakinufaika na mtaji wa kuwa na wanachama wengi, wasanii wa kizazi kipya wenye majina makubwa ambao wanawatumia hao kwenye mikutano yao, jambo lililowavuta watu wengi zaidi kuhudhuria mikutano yao na hapohapo CCM ikatumia upenyo huo kupenyeza sera zake nzuri na kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Kumbuka vyama vingi vya upinzani havina mwenyekiti hata mmoja wa kijiji wala mtaa au kitongoji anayeweza kuwasaidia kupiga kampeni huko chini ambako ndo kuna wapiga kura wenyewe.

CCM huko kote ina wenyeviti wake, viongozi wa chama wa mashina, matawi, kata, wilaya na mkoa ambao wanasaka kura kila kukicha. Hakuna anayelala.

Mpaka sasa CCM imeshapita bila kupingwa kwenye majimbo 28 kati ya zaidi majimbo 264 na kata 850 kati ya kata 3957 ambako kwa tafsiri hiyo tu, maeneo hayo hayana tena wagombea wa upinzani wanaoweza kuwanadi wagombea wao wa urais. Huko kote kumetawaliwa na CCM.

Kumbuka mwaka huu, CCM ilikuwa makini pia katika kuziba mwanya wa mtafuruku kiasi kwamba wale walioshindwa kwenye kura za maoni, kwanza hawakuwa na muda wa kukimbilia upinzani na pia imejitahidi kuhakikisha kwamba wale walioshindwa wanakuwa sehemu ya kuwanadi wale walioshinda.

Kwa kampeni hizi kubwa za CCM maana yake zimewafikia zaidi ya wale wapiga kura milioni saba ambao hawakuwa kwenye kanzidata yake huku ikijiimarishia kura zaidi kwa wapigakura wake milioni 22 waliopo kwenye kanzidata yake na walio tayari kuipigia CCM.

Takwimu za utekelezaji wa mambo makubwa ndani ya miaka mitano tu ziko wazi, udhaifu wa vyama vya upinzani unaonekana.

Baadhi ya mambo hayo ni kusambaza umeme vijijini na barabara za lami zilizounganisha maeneo mengi ya nchi kwa sasa unaweza kutoka Mtwara hadi Kagera kwa teksi.

Amerudisha nidhamu ya hali ya juu kwa watumishi wa umma, amekaribia kumaliza rushwa na ufisadi na sasa imekuwa siyo hoja tena, vituo vya afya kila kata na mikopo elimu ya juu pamoja na makazi ya wanafunzi yameboresha. Hebu tukumbuke shida walikuwa wakizipata vijana wetu UDSM.

Mengine aliyofanya ni kuongeza makusanyo ya kodi na sasa miradi mingi inaendeshwa kwa fedha za ndani, amekuwa mfano katika ubanaji wa matumizi kwa kupunguza safari za nje ambazo amewakilishwa na wajumbe aliowateua hivyo kupunguza gharama kama angeondoka na ujumbe wake mzima.

Kama hayo hayatoshi, kama kuna jambo lilikuwa linatuchafua ni la dawa za kulevya maana haikuwa ajabu kusikia Watanzania wakikamatwa na dawa kila sehemu duniani lakini kwa sasa hilo ni historia.

Mengine aliyofanya ni ujenzi wa miundombinu ya kisasa kama reli ya kisasa ambayo itaenda kuboresha usafiri wa reli, vivuko, kuimarisha bandari na kufufua reli ya kwenda Arusha.

Magufili pia ametekeleza sera ya elimu bure na pia ametisha dunia katika mapambano dhidi ya corona (Covid 19) kiasi kwamba nchi haikuwa na Habari ya kufungiana ndani.

Magufuli pia amekuwa msikivu na kusikiliza shida za wananchi na kuzitatua hapo hapo kila alipokuwa akipita njiani kuelekea katika ziara za kiazi, ameweza kusimamia na kuletwa sheria za madini ambazo zinawabana watu ambao wamekuwa wakitunyonya kwa kutupa gawio ambalo halikuwa sawa na kile wanachokichukua na amefufua shirika letu la ndege.

Hayo ni machache lakini kikubwa nilidhamiria kuwakumbusha tu wapinzani, wasije wakasema wameibiwa kura ushindi wa kishindo na wa kihistoria ambao haujawahi kutokea atakaoupata Rais katika uchaguzi wa leo.

Mwandishi wa mkala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni 0657475347

Columnist: habarileo.co.tz