Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Taifa Stars ni mali ya mtu binafsi?

Taifa Stars Training Taifa Stars ni mali ya mtu binafsi?

Fri, 20 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ siku hizi inaendeshwaje?. Ni kama duka la mtu pale Kariakoo? Ni kama chombo cha familia? Haipaswi kuwa hivyo. Haipendezi kufanywa hivyo na haitakiwi kuachwa iendelee.

Hii ni mara ya pili mfululizo timu inaitwa kambini kimya kimya. Hii ni mara ya pili Watanzania wanajulishwa wachezaji walioitwa kwenye kikosi kupitia akaunti ya TFF ya Instagram. Sidhani kama ni jambo sahihi. Sidhani kama ni kuwatendea haki Watanzania.

Bado Tanzania haijafika hata asilimia 50 ya watu wake kutumia mitandao ya kijamii. Kuamini kuwa kila mtu yuko mtandaoni ni kujidanganya. Timu ya Taifa inapoitwa ni kama Baraza la Mawaziri linapotangazwa. Ni shauku ya kila mtu kujua nani ameitwa na nani ameachwa.

Ni jambo kubwa ambalo mpenzi yeyote wa soka atakuwa anataka kujua nani anaitwa kwa mara ya kwanza. Ni jambo kubwa mno la kitaifa. Ni tukio ambalo kila mpenzi wa soka atakuwa na shauku nalo.

Ni kutowatendea haki Watanzania kutotangaza kikosi hadi vyombo vya habari kuanza kupiga kelele. Taifa Stars sio mali ya TFF, ni mali ya Watanzania. TFF wanapaswa kuwaheshimu sana Watanzania.

Kocha wetu Adel Amrouche anapswa kuambiwa ukweli na mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo ambaye kimsingi ndiye bosi wa makocha wetu wote wa timu zetu za Taifa. Anapaswa kumwambia kuwa Watanzania wanaipenda timu yao ya Taifa baada ya hamasa kubwa sana.

Timu pekee wanazozipenda bila hamasa kubwa ni Simba na Yanga. Wanapaswa kuanza kujengewa utamaduni mpya juu ya timu yetu ya Taifa.

Kuanza kuita timu kimyakimya kama bangi inaweza kuanza kuwafanya waichukie timu yao. Waisusie timu yao. Tuwaweke karibu na timu. Wanapaswa kujua mapema na kwa uwazi sababu za wachezaji wapya walioitwa kwa mara ya kwanza. Wanapaswa kujua sababu za wachezaji Wakongwe wenye ushawishi walioachwa kikosini.

Ni kweli hakuna kocha anayeweza kuwaridhisha mashabiki kwa machaguo yake, lakini ni vyema kutoa sababu ili wananchi waelewe. Kuwaacha wachezaji wakongwe kwenye timu na wenye ushawishi bila kusema chochote ni kutowatendea haki mashabiki wa soka.

Mkurugenzi wa ufundi wa TFF ni lazima atusaidie katika hili. Ni lazima wamueleze kocha wetu ukweli. Kuna siku watu wanaweza kuja kususia mechi za timu ya Taifa. Ni suala la taarifa tu. Mambo ya kuita timu ya Taifa kimyakimya yana gharama kubwa kwenye mpira.

Watu wengi walianza kuzipenda kwanza Simba na Yanga kabla hata ya mpira wenyewe. Hii staili ya kimyakimya itawapoteza mashabiki wengi wa Stars. Itafika mahali Stars inahitaji mashabiki bila mafanikio. TFF watusaidie tusifike huko. Taifa Stars ni mali ya umma.

Kumekuwa na kelele nyingi ambazo kocha kwa maslahi ya umma anapaswa kuzitolea majibu. Feisal Salum akiwa hachezi kutokana na mgogoro na klabu yake ya zamani, Yanga alikuwa anaitwa kwenye timu kila siku.

Kumbuka alikuwa hachezi mechi kokote. Alikuwa nje ya dimba la ushindani kwa muda mrefu sana. Kwa sasa Feisal amejiunga na Azam FC. Anaupiga mwingi na anashika nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao msimu huu kwenye ligi yetu, lakini haitwi timu ya Taifa.

Kocha halazimishwi kumuita, lakini ni vyema kutoa sababu za kumuacha. Kama wakati hachezi alikuwa anaitwa sasa anacheza na kufanya vizuri, lakini haitwi inafikirisha kidogo.

Au ni kwa sababu zama zile alikuwa Yanga? Au kwa sababu zama hizi yuko Azam FC? Huwezi kupata jibu hadi kocha aongee.

Ni busara ya kawaida sana inapaswa kutumika hapa.

Pale Simba, Shomary Kapombe anaupiga mwingi sana. Ni miongoni mwa wachezaji watatu wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwezi pale Unyamani. Unapomuacha kwenye kikosi halafu ukamuita Israel Mwenda ambaye anatoka pia Simba na muda wote huwekwa benchi la Kapambe ni lazima utoe maelezo watu waelewe.

Kama Mwenda anawekwa benchi na Kapombe wakiwa klabuni kwao wewe kocha umemuona wapi? Umetumia kigezo gani kumuita? Taifa Stars sio mali ya mtu binafsi. Ni taasisi yenye maslahi mapana ya umma. Ni muhimu kuwaheshimu Watanzania kwa kuwapa taarifa sahihi na kwa wakati.

Juzi Taifa Stars ilikuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Sudan. Watanzania wengi hawakuwa na taarifa. Watanzania wengi hawakufuatilia hata mechi yenyewe. Hii njia waliyochagua TFF na kocha kupita itaigharimu timu. Taratibu watu wataanza kuichunia timu yao. Shauku ya kutaka kuitazama itaanza kupungua. Taifa Stars sio duka la mtu. Ni mali ya umma.

Pamoja na mafanikio mengi ya TFF hii ya Wallace Karia waliyoyapata, lakini wamekuwa waoga kukosolewa. Wamekuwa wanataka kusifiwa tu. Hata timu ya TFF ikikosolewa wao wanamaindi. Waache uoga. Wana mafanikio mengi tu, waache Watanzania wakosoe timu yao kwa uhuru.

Wanapaswa kumwambia kocha hii timu ni mali ya umma. Kukosoa ni kuzuri sana kwa mtu anayetaka kujifunza. Hatutaki kuwe na machawa wengi kwenye mpira wetu. Mambo ya kusifiana kila kitu yamepitwa na wakati.

Maelezo na ufafanuzi wa kocha huwa unasaidia kuondoka kelele za mashabiki. Ina maana kubwa kwa kocha kutangaza wachezaji mapema na kuzungumza na Watanzania juu ya uelekeo wa timu yetu. Mambo ya kuifanya Taifa Stars kama mali ya mtu binafsi haikubaliki hata kidogo.

Columnist: Mwanaspoti