Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tafiti za wasomi zitoe majibu ya matatizo yetu

C8b39c46b99c96d3fb809e2aae95127a Tafiti za wasomi zitoe majibu ya matatizo yetu

Thu, 24 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MATATIZO mengi kwenye jamii yanaweza kupata majibu kama wasomi wetu watajichimbia na kuja na majibu ya kisomi ya matatizo hayo kwa kufanya tafiti nyingi kwani hapo watakuwa wametumia elimu yao ipasavyo kuiokoa jamii.

Haitoshi tu kwa msomi kupata shahada ya kwanza, ya pili au ya uzamivu bali kinachotakiwa ni kwa wasomi wetu kufanya tafiti mbalimbali kuhusu shida zilizopo kwenye jamii na kuja na majibu yenye ufumbuzi badala ya kila kitu kutafuta wazungu.

Vyuo vikuu ni visima vya maarifa kwani kumejaa wasomi wa ngazi mbalimbali kuanzia wenye shahada ya kwanza, shahada ya uzamili, shahada ya uzamivu na maprofesa wa fani mbalimbali, hivyo ni eneo ambalo wakiamua kwa dhati kabisa wanaweza kuleta mabadiliko hapa nchini.

Chuo Kikuu Ardhi (ARU) kimekuwa mfano wa utekelezaji wa maono hayo kwa kufanya tafiti nyingi zenye manufaa kwa taifa na hivi karibuni kilibuni teknolojia ya kutengeneza mkaa mbadala unaotokana na taka ngumu kikisema kuwa kinalenga kuongeza ujuzi na ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu na wakulima wadogo.

Teknolojia hiyo inaweza kuwa mkombozi wa mazingira kwa maana ya kupunguza au kumaliza tabia ya ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa kama ambavyo imezoeleka kwenye jamii.

Kwa sasa matumizi ya mkaa hasa ambao unakatwa kwa njia ambazo siyo endelevu yamekuwa makubwa sana kiasi cha kutishia uhai wa misitu yetu, hivyo kama utafiti huu wa ARU utatiliwa maanani na kuendelezwa ni dhahiri tutaokoa misitu.

Ubunifu kama huu ni wa kuungwa mkono na kuendelezwa kwa ajili ya mustakabali wa nchi kwani ni kwa muda mrefu wadau wa mazingira duniani wamekuwa wakilalamikia ukataji miti kwa ajili ya mkaa kama janga linaloitesa dunia leo na kesho.

Teknolojia hiyo ni suala muhimu na ambalo serikali inapaswa kulitilia mkazo kwani litaliokoa taifa kuelekea kuwa jangwa kwani watu watahamia kwenye matumizi ya kuni mbadala na kuachana na ukataji wa miti ambayo ndiyo maisha ya sasa

Akizungumza kwenye mahafali ya 14 ya chuo hicho hivi karibuni, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa, alisema chuo hicho pia kimefanya utafiti wa kuboresha matumizi na mbinu mpya za umwagiliaji katika bonde la mto Rufiji ili kuleta tija na kuongeza uzalishaji katika Wilaya ya Iringa pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za matumizi ya maji katika mto Rufiji

Profesa Liwa anasema chini ya ufadhili wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), chuo kimefanya utafiti kuhusu teknolojia ya asili ya ujenzi wa nyumba zinazostahimili matetemeko ya ardhi katika mji wa Dodoma na utafiti huo utawezesha kutumia taaluma hiyo kwenye ubunifu wa majengo ya kisasa ya mkoa huo.

Utafiti kama huo una manufaa makubwa kwa Watanzania hasa ikizingatiwa kuwa utasaidia kuwakinga watu wengi na majanga ya asili ambayo iwapo yatatokea yatasababisha uharibifu mkubwa wa mali na wakati mwingine kugharimu maisha ya watu

Ingawa ni kwa nadra sana majanga ya asili kama matetemeko ya kiwango kikubwa kutokea kwa hapa nchini lakini ni vyema hatua kama hizo zinazochukuliwa na ARU zikaungwa mkono na kuendelezwa ili watu wakajenga kwa kuzingatia hilo hasa kwenye maeneo yenye uwezekano wa kutokea matetememo.

Nchi inapoelekea kwenye uchumi wa viwanda tafiti si jambo linalohitaji mjadala kwani ni suala muhimu linalohitaji kutiliwa mkazo na serikali, watu binafsi na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kufikia ndoto ya Tanzania ya viwanda.

Rais wa awamu ya tano, Dk John Magufuli amekuwa akisisitiza kuipaisha Tanzania kiviwanda hivyo moja ya nguzo kuu kufikia ndoto hizo ni kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitaweza kuwezesha ugunduzi wa teknolojia mbalimbali ambazo zinaweza kuuzwa hata nje ya nchi.

Imekuwa kawaida kwa nchi mbalimbali za Afrika kuagiza au kunakili teknolojia zilizobuniwa na mataifa ya Ulaya, Marekani na Asia lakini umefika wakati wasomi wetu waoneshe thamani ya usomi wao kwa kufanya tafiti nyingi na kugundua teknolojia.

Imekuwa kawaida kuona wataalamu wetu wakienda kwenye mataifa mbalimbali yaliyoendelea kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo teknolojia mpya lakini hatuwezi kujivunia sana hilo kwani ufike wakati na wao waje kujifunza Tanzania.

Elimu wanayopata wasomi wetu inatakiwa kuwa chachu ya kuwa wabunifu wa mambo mbalimbali ili kuwapa tamaa vijana wanaochipukia wanapoona wasomi wamebuni teknolojia mbalimbali ambazo mwishowe zinakuwa na manufaa kwa nchi.

Ndiyo sababu tafiti zinazofanywa na ARU ni muhimu kwa ustawi wa taifa na vyuo vikuu vyote ambavyo ndiyo visima vya maarifa, hivyo wafanye tafiti nyingi kadri ya uwezo wao ili waje na majibu ya matatizo mengi yanayosumbua kwenye jamii yetu.

Kwenye mahafali ya 14, Profesa Liwa alisema ARU imefanikiwa kuwa na matokeo ya utafiti yaliyohusu uhitaji wa utaratibu mpya wa upangaji wa miji na kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi chuo kimehuisha miongozo ya upangaji miji hapa nchini.

Hili ni eneo lingine muhimu la utafiti ambalo wasomi wanapaswa kuwekeza kwa nguvu kubwa kwani miji mingi hapa nchini imejengwa holela ni maeneo machache sana ambayo yamejengwa kwa mpangilio unaotambuliwa na serikali.

Wananchi wamevamia maeneo mengi kabla ya serikali kupanga hivyo wasomi wanapaswa waje na majibu ya suala hili kwa kutengeneza miongozo itakayosababisha miji mingi hapa nchini ipangiliwe upya kwa kuwekwa miundombinu itakayosababisha maeneo hayo yafikike.

Maeneo ambayo hayajafanywa makazi bado ni mengi nchini hivyo wasomi wakija na mpango mzuri wa namna ya kuyapanga maeneo hayo kabla ya kuvamiwa na wananchi ili yajulikane maeneo ya wazi, barabara na mitaa tofauti na ilivyo kwenye baadhi ya miji ambayo haifikiki kutokana na kutopangiliwa.

Hivyo basi kuna umuhimu mkubwa wasomi wetu badala ya kuishia kufundisha kwenye vyuo vya elimu ya juu wakajikita kufanya tafiti mbalimbali waisaidie nchi kufikia malengo yake ya kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa juu kwa kuja na tafiti nyingi zitakazotoa majibu ya matatizo yaliyopo.

Columnist: habarileo.co.tz