Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tafiti za REPOA na matokeo ya uchumi wa wanawake

ACE Logos 640x400px REPOA Tafiti za REPOA na matokeo ya uchumi wa wanawake

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: Habarileo

UWEZESHAJI wa wanawake kiuchumi ni jambo muhimu zaidi katika dunia hii ambayo teknolojia inakua kwa kasi.

Hakuna anayepinga kwamba ukimwezesha mwanamke kiuchumi umewezesha familia na jamii nzima kutokana na nafsi ya malezi aliyonayo.

Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umasikini (REPOA) kwa muda mrefu imekuwa na msaada mkubwa kuwawezesha wanawake kutambua fursa za kiuchumi.

Kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995, Repoa imejitokeza kuwa taasisi mahiri ya utafiti iliyokuwa msaada kwa nchi.

Mtafiti Mwandamizi wa taasisi hiyo, Jane Mpapalika anasema upekee wa taasisi hiyo ni namna ilivyotoa mchango kwenye kujengea watafiti uwezo wa kufanya tafiti za kisera na pia kwa watumiaji mbalimbali wa tafiti.

“Repoa ni taasisi inayohusika na kutokomeza umasikini na kukuza uchumi kwa hiyo tunasaidia serikali kwa kutoa ushauri jinsi ya kutokomeza umaskini.

“Tunaangalia mambo tofauti tofauti kwa sekta zote nchini kwa kipindi cha miaka 25 tuliyofanya kazi za tafiti. Anasema hadi sasa wamefanya tafiti zaidi ya 10 zinazohusu wanawake.

JINSI INAVYOSAIDIA WANAWAKE

Anaeleza kuwa licha ya kufanya tafiti pia wanajihusisha kutoa mafunzo mbalimbali kwa jamii hasa wanawake ili kuweza kuwasaidia kutambua fursa zilizopo kiuchumi.

“Huwa tunafanya tafiti tofauti tofauti na pia tuna programu na mafunzo kwa ajili ya wanawake na hizi zinalenga kuwawezesha ili ziweze kuwasaidia kukua katika shughuli zao za aina mbalimbali.

“Mara nyingi tunafanya tafiti kama vile njia gani tutawawezesha wanawake kwa mazingira waliyopo miongoni mwa programu tuliyofanya inajulikana kama ‘Growth and Economical Opportunists for Women’ iliyodhaminiwa na International Development Research Center (IDRC).

Anaongeza: “Ndani ya hiyo programu tulikuwa tunashirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika mpango wake wa kunusuru kaya masikini katika kuwasaidia wanawake kwasababu tunaamini ukimwezesha mwanamke umewezesha jamii nzima.

Mpapalika anabainisha kuwa kupitia mradi huo wanawake walipewa hela kwa ajili ya kuendeleza familia zao ikiwa ni njia mojawapo ya kuwawezesha.

“Lakini pia tumefanya utafiti kuhusu watoto wa kike, tuliangalia watoto wanavyoolewa nini kinampata au anaathirika vipi katika makuzi yake, kujikwamua kimaisha maana yake kuolewa chini ya miaka 18 mtoto amenyimwa uhuru wake, haki yake ya msingi ya kuendelea na masomo yake.”

Anasema matokeo ya tafiti yalionesha watoto wa kike waliopata ujauzito waliingia katika mtiririko wa umasikini hivyo kusababisha nchi kurudi nyuma.

“Tafiti nyingine tuliyofanya inaitwa ‘women committing violence’, tumezoea sana kwenye jamii yetu tunasikia wanaume wananyanyasa wanawake lakini kuna ile wanawake tunanyanyasana wenyewe kwa wenyewe.

“Tumekuwa tukiwasaidia wanawake wajasiriamali kwa miaka mingi jinsi ya kujikwamua, tumekuwa tukishirikiana na baraza la uwezeshaji Tanzania katika kufanya tafiti jinsi ya kuwezesha wanawake wafanyabiashara watoke ngazi ndogo hadi kati na juu zaidi,” anafafanua Mpapalika.

Anasema tafiti nyingine waliyofanya ni kuhusu madini ambapo waliangalia ni namna gani wanawake wanavyoweza kunufaika na mradi wa gesi inayopatikana Mtwara.

“Hivyo tafiti zetu nyingi wanawake wanaingizwa ambao ni wazawa lengo ni kutaka wanawake wawezeshwe katika ule mradi kwasababu wanawake wana majukumu katika nyumba na tunafanya hivi ili wanawake wasiachwe nyuma.

“Pia tulifanya mafunzo maalumu Zanzibar kwa wanawake jinsi ya kulima mwani, mbogamboga na mradi ulifanikiwa kwa kuwawezesha wanawake,” anasema.

WAELEZA WALIVYONUFAIKA

Miongoni mwa wanawake walionufaika kiuchumi na mafunzo yanayotolewa na Repoa ni Fatuma Makame, mkazi wa Pemba, Zanzibar.

Anasema mafunzo aliyoyapata yalimsaidia kuelewa jinsi ya kutumia zao la mwani kutengeneza bidhaa mbalimbali. “Awali tulikuwa tunauza mwani kilo moja Sh 600, lakini sasa tumefundishwa namna ya kutengeneza bidhaa zitokanazo na zao hilo kama sabuni za maji na mafuta mgando,” anasema Fatuma.

Anasema bidhaa hizo wanaziuza kuanzia Sh 1,000 hadi 2,500 na kuongeza kipato chake. “Sasa nimekuwa mjasiriamali kipato changu kimeongezeka, pesa zinanisaidia kuongezea katika mtaji na kuhudumia familia kama kusomesha watoto na kupata nguo za sikukuu,” anaeleza Fatuma.

Naye Meire Hamadi anasema baada ya kupewa mafunzo alifanyia kazi alichojifunza na sasa anafanya biashara za kusafirisha bidhaa kutoka Pemba hadi Dar es Salaam.

“Mwanzo tulikuwa hatujaanza kutengeneza bidhaa sasa tumepata soko zuri, ninatengeneza mafuta, scrabu, losheni na kuzisafirisha kwenda Dar es Salaam,” anasema Meire.

“Nimejua faida nyingi zinazotokana na zao hilo hasa bidhaa zake na kipato kimeongezeka ni msaada kwa familia, watoto wangu nimewapeleka skuli za kulipia,” anabainisha.

UTAFITI WA MAWASILIANO

Utafiti mwingine uliofanywa na Repoa mwaka jana ulihusu matumizi ya simu kwa makundi matatu ya wanawake na TASAF ilihusishwa.

“Kundi la kwanza lilipewa simu ambazo ni ‘smatphone’ na za kawaida, kundi lingine lilipewa fedha kwa ajili ya kununua simu na wengine walipewa laini bila simu.

“Waliopewa simu walipewa kiasi cha pesa ili kufanya matumizi ya simu, hapa tuliangalia mambo matatu hali yao ya matumizi ya simu, walivyokuwa awali na sasa,” anaeleza Cornel Jahari mmoja wa washiriki wa utafiti huo.

Anasema utafiti huo ulifanyika katika mikoa ya Mwanza, Geita, Tanga, Pwani (Kilwa), Ruvuma (Songea), Arusha na visiwani Zanzibar ukihusisha wanawake zaidi ya 1,800.

“Wanawake waliopewa simu wengine waliwapa watoto, waume zao na wengine walitumia kwa matumizi mengine, wapo waliozihifadhi tu na tulivyorudi tulizikuta,” anafafanua Jahari.

Anasema matumizi ya simu yalikuwa mengi kwa wale wa vikoba kuliko watu wa TASAF, mfumo wa kupokea fedha na kutuma ulikuwa mdogo kwa watu wa TASAF walikuwa hawatumii simu kupeleka fedha.

“Kwa wale waliopewa fedha wengine walinunua simu za bei nafuu na nyingine wakanunua vitu vingine kama mifugo mfano kuku ambao walikuwa wanapata kipato zaidi.”

Anaeleza kuwa wengine walikuwa wanatumia simu kujua bei za bidhaa mbalimbali. “Tafiti nyingi zinasaidia kufanya maamuzi mfano tulivyofanya na TASAF pia iliwasaidia, wengi waliweza kubadilika na kuanza miradi midogo midogo na zimesaidia watu masikini zaidi kutambua fursa za kiuchumi,” anabainisha Jahari.

MANUFAA YA TAFITI KWA SERIKALI

Jahari anasema tafiti wanazofanya zinasaidia serikali katika kutenga fedha na namna ya kuelekeza maendeleo katika jamii mfano kwenye miradi ya kimkakati ili kukuza uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla

“Zinashauri serikali mfano tafiti ya jinsi ya kukuza mapato inasaidia kujua nini kifanyike, kama ile ya vifo vya mama na kilimo ili wanapotunga sera wasitunge tu wajue kuwa kuna hiki na kile,” anasema.

Dk Mpapalika anasema hadi sasa wanajivunia kuwa ndani ya nafasi ya 10 ya taasisi za Afrika zinazofanya tafiti zenye manufaa. “Tunajivunia kusaidia kutokomeza umasikini katika tafiti zetu tunazofanya serikali inazitumia na pia wananchi wa kawaida wanafaidika katika kuboresha hali zao za uchumi.

“Hadi sasa tumefanikiwa kutoa mafunzo kwa wanawake zaidi ya 50 kwa mwaka huu na tunalenga maeneo tofautitofauti kwa wanawake wajasiriamali na wanaokaa nyumbani tunawawezesha kuona fursa za kiuchumi na kuzitumia,” anabainisha Mpapalika.

Anasema matarajio yao ni kuona Tanzania inakuwa na mafanikio na serikali kuchukua tafiti wanazofanya watumie ili kuweka sera za kusaidia wananchi.

Columnist: Habarileo