Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tafiti, teknolojia kuvutia vijana kupenda kilimo

12fb89042a37545b38e0b34479d0dee6 Tafiti, teknolojia kuvutia vijana kupenda kilimo

Tue, 10 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JIMMY Godfrey, anatua furushi lake la nguo anazotembeza mitaani katika kiti kilicho wazi mbele ya duka la Mama Salha, Temeke Maganga, Dar es Salaam, saa 11 na ushei jioni ya Agosti 8 mwaka huu.

Akionekana amechoka, Jimmy, mkazi wa Tandika Davis Corner, ananunua chupa kubwa ya maji, na kuketi kwenye msingi mbele ya duka hiko akiwa na begi mgongoni ili kunywa maji na kupumzika kidogo, kabla ya kuendelea na biashara yake ya kutembeza nguo mitaani.

Katika mahojiano kuhusu biashara yake, Jimmy ambaye asili yake ni Kata ya Nanjirinji, Kilwa, mkoani Lindi, anakiri kwamba biashara ni ngumu na yeye ana familia ya mke na watoto wawili.

Sehemu kubwa ya nguo takribani 15 alizoshikilia mkononi huku chache zikiwa kwenye begi ni nguo za mitumba za watoto zinazofaa kwa majira ya baridi na michezo, yaani sweta, suruali na kaptura za michezo.

"Hizi nguo nimechukua 'mbegu' (malikauli) kutoka kwa tajiri wangu anayefungua marobota baada ya mtaji wangu kukata. Kwa hiyo ninauza ili siku mbili hizi nimrudishie pesa yake, mimi nibaki na faida."

Kijana huyo aliyeanza biashara hiyo takribani miaka 10 iliyopita, anakiri kwamba hajapata mafanikio makubwa katika shughuli hiyo zaidi ya pesa ya kujikimu.

"Kuna siku unatembea kidogo tu unabakiza nguo chache. Lakini kuna siku kama leo, unatembea lakini hakuna kitu. Kwa mfano, jana nilipanda gari nikashuka Mbezi. Nikaanza mdogomdogo hadi giza linanikuta nakaribia Majumba Sita, Ukonga. Ndipo nikapanda gari kurudi nyumbani kupumzika," anasema.

Anapoulizwa kuhusu mashamba kwenye kijiji chao cha Nanjirinji, eneo linaloongoza kwa kilimo cha ufuta mkoani Lindi huku pia likisikfika kwa kuwa na ardhi nzuri kwa kilimo cha mahindi na mpunga sambamba na uvunaji wa mazao ya misitu, Jimmy anakiri kwamba kuna aliowaacha kijijini wana maendeleo makubwa kwenye kilimo lakini yeye kilimshinda.

"Maisha ya kilimo ni mazuri, hasa wakati wa msimu. Lakini mjini unaweza kupata shida kama hivi biashara inapokuwa mbaya, baadaye mambo yanakuwa mazuri," anasema.

Wakati Jimmy akisema hayo, Farida Moshi, mkazi wa Mkoa wa Arusha, yeye ni miongoni mwa vijana ambao wameamua kuendesha maisha yao kwa kujiunga kwenye kilimo biashara, dhana inayohusisha kilimo na biashara zinazohusiana na kilimo.

Yeye amejikita zaidi kwenye biashara ya mazao mbalimbali ambayo anayachukua toka kwa wakulima na kuuza moja kwa moja kwa mtu mmoja mmoja ama wale wanaotuma kwake maombi maalumu.

Shughuli kama hii, endapo Jimmy atatunza akiba kutokana na kipato chake kidogo, anaweza kuifanya pia.

Farida anasema anafanya biashara hiyo huku akijua kuna faida na hasara kama zilivyo biashara nyingine, hivyo inabidi kupambana ili kutoka kimaisha.

Anasema kama mfanyabiashara wa nafaka mbalimbali ananufaika pia na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kupitia semina mbalimbali juu ya kilimo biashara pamoja na namna ambavyo wanafanya utafiti wa mbegu bora kwa ajili ya kilimo.

Anafafanua kwamba ingawa yeye haiingii shambani kulima lakini hutumia elimu hiyo kuwaelimisha wengine na pia humsaidia kujua mazao yanayotokana na mbegu bora na yaliyolimwa kisasa.

Anasema vijana wengi wanapata changamoto ya kufanya biashara kutokana na kukosa mitaji.

“Biashara sasa imekuwa ni ngumu ila ni kukaza moyo na kutokukata tamaa. Hivyo kwa vijana ambao hawajishughulishi na wanaogopa kilimo kabisa waingie kwenye biashara kama yangu na kujaribu,” anasema.

Farida anasema anauza nafaka za mahindi, maharage, mbaazi, choroko, ngwara, mtama mweupe na ufuta.

Anasema amekuwa akifanya biashara yake zaidi kwa kupokea maombi maalumu kutoka kwa wateja na pia kwa fedha taslimu kwa anayetaka.

“Unaweza ukaagizwa tani 30 na mteja ukauza kwa kumtumia mzigo moja kwa moja, unaweza ukauza reja reja ukajikuta umeuza gunia moja kwa siku ama unaweza kwa siku usiuze kabisa,”anasema.

Anasema maisha ya sasa mtu hawezi kuishi bila kujishughulisha kwa kutegemea kutafutiwa, hivyo kwa wale ambao hawajaajiriwa wanapaswa kufikiria kufanya biashara ama kuingia kwenye kilimo kwani wahenga wanasema jembe halimtupi kabisa mkulima.

Anahimizq vijana wenzake kujikita kwenye kilimo moja kwa moja kwa kulima ama kuuza mazao kama anavyofanya yeye.

Mkurugenzi Mkuu wa Tari, Dk Geofrey Mkamilo amekuwa akihimiza mara kwa mara kuwa sio lazima vijana kuchukua jembe na kulima bali wanaweza kufanya biashara ya mazao ya kilimo.

“Vijana wengi wanakiona kilimo kama ni adhabu lakini sisi tunakuja na teknolojia na ubunifu utakaowafanya vijana nao wawe sehemu ya kilimo.

“Kilimo si cha kuchukua jembe tu unalima hapana, unaweza wewe ukawa unakwenda kununua maharage kwa wakulima shambani ukachukua yale maharage wewe na kwenda kuyauza ukapata fedha.

"Vijana wanaweza wakaingia sehemu mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani sio lazima awe na shamba wengine wanasema mi sina shamba. Kimsingi sio lazima ushike jembe, unaweza ukafanya shughuli yoyote ya kilimo kwenye mnyororo wa thamani,” anasema.

Anatolea mfano mkoa wa Dodoma kuwa kwenye zao la zabibu wapo wakina mama lukuko ambao hawalimi bali wananunua zabibu kwa maana ya matunda na kuzipanga mezani kusubiri wateja.

“Mkakati wetu ni kuhamasisha vijana waondokane na zile fikra tofauti, kwamba vijana ambao ndio wana nguvu nyingi za kuzalisha, pia wawe ni sehemu ya kilimo kwenye mnyororo huu wa thamani,” anasema.

Anasema kilimo biashara sio cha kujikimu pekee kwa maana ya mkulima kuishia kupata chakula pekee bali pia kuuza mazao ili kukidhi mahitaji yake mengine kama kusomesha watoto, kununua mavazi, kununua aina mbalimbali za vyakula na mahitaji mengine.

“Ili ufanye hivyo lazima uwe na malengo unataka kulima nini. Sasa hivi tunaona zao la alizeti serikali imeshaweka mikoa mitatu ya kimkakati kwa ajili ya kusaidia wakulima wa maeneo ya pale ili uzalishaji wa mafuta ya kula hapa nchini uongezeke," anasema.

Anataja mikoa ya kimkakati katika kuzalisha alizeti kuwa ni Dodoma, Singinda na Simiyu.

Anasema kwa maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Kilimo, wakulima wa alizeti katika mikoa hiyo watapata huduma zote za ugani ili waweze kuzalisha kwa tija.

“Hicho ndicho kilimo biashara, unalima kwa lengo la kufanya biashara. Sisi kama Tari kila mwaka tunakuwa na maonesho ya wakulima lakini tunachoonyesha pale ni teknolojia zote tulizonazo na wadau wote wa kilimo wanakuwepo,” anasema.

Anasema maonesho hayo ni fursa kwa mkulima na watu wengine wenye nia ya kujiunga kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, kuona fursa zilizopo kwenye utafiti wa kilimo kuanzia mbegu pamoja na mbinu bora za kilimo, upandaji, uwekaji wa mbolea na utanzaji.

Ni sehemu ambayo mkulima anajifunza ili aondokane na kile kilimo cha mazoea, aje kwenye kilimo cha kisasa.

Hii ni njia itakayomfanya mkulima aweze kuongeza tija na uzalishaji katika yaleyale mazao anayolima lakini sasa anatakiwa alime kibiashara.

“Tunapolima mtu ajiulize analima kwa ajili ya soko gani? lazima uwe unajua unalima kwa ajili ya soko lipi,” anasema.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Tari-Selian mkoani Arusha, Dk Joseph Ndunguru anasema sekta ya kilimo ili iwe yenye tija ni lazima kuwepo na utafiti.

“Huwezi kuwa na kilimo chenye tija bila utafiti. Kwa kuwa utafiti ndio unatoa majibu ya tatizo lililopo, kwa kufanya utafiti tunaona kabisa sisi kama watafiti tutakuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa viwanda na wakulima pamoja wadau mbalimbali watajiongezea kipato.

“Lakini kama mnavyojua sekta ya kilimo inatoa ajira kwa watu wengi sasa, ili watu wavutike kwenye sekta za kilimo ni lazima tuwe na kilimo chenye tija ambacho ni kilimo kinachotumia teknolojia ya kisasa ambayo sisi kama watafiti ndio tunaifanya,” anasema Dk Ndunguru.

Katika maonesho ya kilimo biashara yaliyofanyika hivi karibuni katika Kituo cha Selian, Arusha, Katibu Tawala wa mkoa huo, Dk Athuman Kihamia alisema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kutosheleza masoko ya mazao duniani kutokana na kuwa na ardhi ya kutosha pamoja na hali nzuri ya hewa.

Alisema, hata hivyo kwamba hilo linakwama kutokana na Watanzania wengi kuendesha kilimo cha mazoea pamoja na kutotumia utaalamu wa kilimo bora.

Vilevile alisema uzalishaji mdogo kwa eneo, magonjwa na wadudu waharibifu, ukosefu wa soko la uhakika, mabadiliko ya tabianchi, gharama kubwa ya pembejeo ikilinganishwa na kipato cha wakulima ni baadhi ya vitu vinachangia uzalishaji wa mazao kuwa chini.

Columnist: www.habarileo.co.tz