Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TUONGEE KISHKAJI: Diamond anaimba na kutafuta wateja

Diamond Pic Diamond Platnumz

Mon, 14 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Alhamisi hadi saa sita usiku nilikuwa macho nasubiri kusikiliza EP ya Diamond. Kuwa macho hadi saa sita usiku haishangazi, ila kuwa macho hadi muda huo kwa ajili tu ya kusikiliza EP imekaa kiboyaboya sana, huwezi hata kuisema mbele ya washkaji wakakuelewa. Eti, “Dah! Jana nimelala saa saba usiku”. “Kwa nini?” washkaji wanakuuliza. “Nilikuwa nasubiri kusikiliza EP ya Diamond.” Huwezi kusema hayo mambo.

Lakini kwa upande wangu nilikuwa na cha kujitetea, nasikiliza ili nipate cha kuchambua, ndo kazi inayoniweka mjini.

Kwanza unajua mwanzo nilitegemea atatoa albamu kwa sababu Diamond na timu yake walitumbia watatoa albamu tangu mwaka jana. Na hata harakati zake zilikuwa zimekaa kialbamu tena albamu ya kimataifa. Alikuwa anaijaza Instagram yake na picha akiwa Marekani studio na wasanii wakubwa wa huko, kina Snoopy Doggy, Wiz Khalifa, Alicia, Swizz Beatz mpaka wasanii wa India.

Lakini kwa sababu wasanii wote hao hawajasikika kwenye EP yake maana yake inawezekana kabisa kuna albamu inakuja.

EP ambayo inaitwa FOA (First of All) ni nzuri lakini haifiki kwenye ‘level’ za kuitwa moja ya kazi bora za Diamond. Kati ya nyimbo 10 kuna nyimbo kama tatu tu ambazo zina ladha ya kibongo, nyingine zilizobaki ni kama vile Diamond alikuwa anajaribu kuwaambia wanaijeria hata mimi naweza kuimba muziki kama wenu, na sio kuimba muziki huo tu, na hata kuandika mashairi kama yenu. Sio mara moja, Diamond anasikika akiimba kwa kutumia maneno ya kinageria kabisa.

Lakini sitaki kujikita sana huko, najua Diamond alipofikia sasa hivi hata akitoa albamu au EP mbaya kuliko zote alizowahi kutoa tangu aanze muziki hakuna namna atakosa wasikilizaji.

Hiko ndio kitu natamani kukiongelea leo. Inakuwaje huyu jamaa muda wote anakuwa na watu wa kumsikiliza?

Moja ya sababu rahisi ni jamaa tayari ni staa mkubwa zaidi wa muziki Tanzania kwa hiyo tayari ana ‘attention’ ya watu, lakini sababu nyingine ambayo labda watu hawaitazamani sana ni timu yake ya matangazo inavyojua kumtafutia wateja.

Fikiria usiku ule ule, baada ya EP kutoka, watu walishaisikiliza na kuifanya mjadala kwenye mitandao ya kijamii.

Usiku ule ule ilikuwa ukiingia Instagram na Twitter unakuta watu wanabishana Albamu mbaya au nzuri mpaka unajiuliza hawa watu wanafanya kazi ‘shifti’ za usiku kwahiyo albamu imewakuta wakiwa kazini au ni watu ambao waligoma kulala ili tu wasikilize EP ya Diamond?

Lakini yote hiyo ni kwa sababu timu ya Diamond ilianza kutengeneza wasikilizaji kabla hata kazi haijatoka. Walitengeneza kutumia njia ambazo hazitumiki sana na wasanii wa Bongo. Wasanii wengi wa Bongo wanaimba halafu wanaacha muziki wao uwatafutie wateja, kwa hiyo hata wakifanya matangazo ni ya kawaida sana. Wataenda kwenye vyombo vya habari kufanya intavyuu mbili tatu kisha basi.

Lakini timu ya Diamond ilianza na kupost vitu vya kuamsha mchecheto, yaani wanaposti hashtag ya #FOA na picha ya rangi ya ‘orange’ tu na kuandika tarehe. Hujui nini kinakuja kutokea.

Na mwendo huo wakauhamishia kwenye mabango ya barabarani. Nambie uliona wasanii wangapi Bongo wakiweka mabango ya EP zao au hata albamu zao kabla hazijatoka?

Wakaanza ‘kuwalazimisha’ mastaa wote wa bongo kuvaa fulana zilizoandikwa #FOA zenye rangi ya ‘orange’ au ‘nyeupe’ na kila staa akawa anaposti kwenye page yake ya mtandao wa kijamii. Ikawa kila ukiingia Instagram, kila msanii unamuona yuko na fulana ya #FOA, nambie nani aliwahi kufanya hivyo?

Mpaka siku anakuja kusema kuwa ni EP watu wakabaki na swali moja? Hiyo FOA maana yake nini? Ambapo alikuja kuwajibu mwishoni alipotoa ratiba kamili ya uzinduzi wa EP.

Inawezekana ikaonekana ni mambo madogo sana lakini amini kwamba sio kila msanii Tanzania, hata wasanii wakubwa wamebahatika kuwa na timu ya matangazo kama aliyokuwa nayo Diamond. Jamaa anaimba na kutafuta wateja wakumsikiliza.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz