Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TUNAHITAJI HISTORIA ITAKAYOSAIDIA UWEPO WA VIPAUMBELE VYA KITAIFA

E585b2c1cc8b1cbf7b3218d6df945861 TUNAHITAJI HISTORIA ITAKAYOSAIDIA UWEPO WA VIPAUMBELE VYA KITAIFA

Wed, 11 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

NDUGU msomaji wewe na mimi tunakubaliana kwamba historia ina maana sana katika dhana nzima ya maisha ya mwanadamu. Kupitita historia, mtu huweza kutambua jana ilikuaje, leo ikoje na kundaa kesho yake vizuri zaidi.

Kitendo cha kusoma na kuishi kwa historia iliyoandikwa na mkoloni ni kuendelea kuuishi ukoloni na viashiria vyake vyenye lengo la kuendelea kumuonyesha mwafrika kama kiumbe dhaifu kilichojaa unafiki, ulaghai na usaliti.

Historia hii iliyopo, inaonesha watawala wa awali yaani machifu/watemi waliwasaliti waafrika wenzao kwa kuwauza utumwani kwa lengo la kupewa shanga na vitu vingine vidogo vidogo.

Swali langu ni kwa kiwango gani dhana hii ina ukweli? Ukiachilia mbali ukweli kwamba utumwa ulikuwepo hata kabla ya kuja kwa mkoloni, lakini je, ni kweli wazee wetu hawa waliopigania uhuru walikuwa wanawauza wenzao kwa kupewa shanga na vipande vidogo vya nguo? Ni nani awezaye kuthibitisha hili?

Nimepata bahati ya kutembelea vituo vya makumbusho ndani ya nchi yetu karibia mikoa yote, kinachoshangaza na kusikitisha, makumbusho haya yamejaa kuutukuza ubeberu zaidi kuliko uafrika!

Jinsi wanahistoria hawa wanavyoeleza, huelekeza nguvu zao zaidi katika kuelezea mabeberu waliokuja kuharibu Afrika, kuliko kuelezea wazee wetu walivyooilinda Afrika kwa kila hali! Sasa huwa najiuliza vituo hivi vya makumbusho tumewaanzishia wakoloni au tumejianzishia sisi?

Kuna ukweli kwamba tawala za kichifu/kitemi zilizokuwepo kabla ya historia ya kibeberu tunayoisoma, inaonyesha kwamba wazee hawa walikuwa wamestaarabika sana na walikuwa na uwezo wa kuwasiliana na Mungu moja kwa moja katika utatuzi wa mambo. Kuja kwa mkoloni kumebadilisha hali hii. Ni bahati mbaya sana hata sisi wenyewe hatuko tayari kuijua kweli ya asili yetu kama waafrika ili kutambua vipaumbele vyetu.

Mfano ni rahisi sana Mnyaturu kujua historia ya mkoloni kuliko historia ya Mama Liti aliyekuwa na uwezo wa kukaa juu ya mkuki na kutumia nyuki kuwatimua wavamizi kwenye eneo lake!

Historia inaonyesha kwamba mwana mama huyu shujaa – Liti aliwatimua wakoloni wote waliojaribu kuingia kwenye ardhi ya Singida kwa kuwatumia nyuki. Maajabu yake ilikuwa ni kwamba nyuki hawa waliweza kuwang’ata wazungu tu na kuwaacha weusi salama! Kufanya hivi kuliiifanya tawala yake iwe salama! Swali ni wapi utakuta historia yake shujaa huyu? Ni lini vizazi hivi vitaijua hadithi hii?

Ndugu msomaji, ni wazi kwamba ukionyesha historia ya ushujaa wa wazee wetu hawa, kuna uwezekano wa kujenga taifa lenye dhana ya nguvu kitaifa na hivyo kutanguliza ulinzi wa taifa husika kama kipaumbele. Dhana hii itawafanya waafrika wasijione kama bara dhaifu bali bara lenye nguvu na lisilohitaji misaada ya kikoloni katika kuishi kwake bali bara la kuogopwa na kuheshimiwa na kila mtu. Kwani tunahofu gani kutumia mila na desturi zetu katika kulilinda bara letu? Tunaogopa nini kuiweka historia yetu hii wazi kwa vizazi vipya?

Ukisoma historia ya mkoloni inaonyesha kwamba wakina Livingstone walikuja kueneza dini Afrika japo ndani mwake walikuwa wapelelezi wa kibeberu waliokuwa na nia ya kuitawala Afrika kwa kila namna.

Kuna Ushahidi kwamba kabla kukaribisha ukoloni, mabeberu hawa waliandika mengi kuhusu maisha halisia ya uafrika na kuyatuma kwao. Swali langu ni waliandika nini? Maandishi yao haya tunaweza kuyapata wapi? Hatuoni umuhimu wa kuyahitaji ili kubadili historia za nchi zetu ndani ya bara la Afrika?

Ni mambo ya ajabu eti, tunamkaririsha mtanzania/mwafrika kwamba Livingstone alifia Zambia kisha kutolewa utumbo wake ukazikwa Zambia huku mwili wake ukipitishwa Bagamoyo kisha kwenda kwao kuzikwa! Wakati tungeweza kutumia muda mwingi kuonyesha ushujaa wa Mkwawa, Milambo, Liti, Mangi Sina, Mangi Mery, Kinjekitile Ngware, Ngoma ya Mwanamalundi n.k.

Nilifurahi sana kipindi fulani serikali ilipotangaza kufundishwa historia ya Tanzania inayoonyesha uhalisia wetu! Japo sijui kwa sasa kama jambo hili litapewa kipaumbele tena. Furaha yangu ilijikita kwenye ukweli kwamba pengine watanzania wangepata bahati ya kulijua taifa lao kwa undani zaidi kuliko kutegemea matango pori ya kikoloni yenye lengo la kudumaza ufikiri wetu.

Nilitegemea somo hili la Historia lingesaidia kuibua fikra mpya kwa kizazi kipya cha kitanzania dhidi ya historia ya ulimwengu.

Taifa lolote ulimwenguni linahitaji kuwa na historia yake halisia ili kuweza kutambua maeneo muhimu ya kupewa vipaumbele vyao vilivyokuwepo tangu enzi za mababu zetu.

Kwa mfano wangapi wanajua kuwa kumbukumbu inaonesha kwamba Tanzania ilianza kupokea Wakimbizi takribani miaka 60 iliyopita. Na wakati fulani taasisi inayojishughulisha na masuala ya wakimbizi na haki za binadamu ya Dignity Kwanza ilisema inaungana na wadau wengine kuandika historia ya kupokea wakimbizi katika nchi yetu. ( HYPERLINK "http://www.habarileo.co.tz/habari/2020-12-145fd7a719b2144.aspx" www.habarileo.co.tz/habari/2020-12-145fd7a719b2144.aspx)

Kukosekana kwa historia yetu halisia kunatufanya kama taifa tushindwe kuelewa ni vitu gani tunapaswa kusimamia kwa maslahi ya ulinzi wa tamaduni zetu na asili yetu.

Tunahitaji kufundishwa historia yetu kama Watanzania na kama Waafrika kwa lengo la kukuza uzalendo, na kufahamu hasa jinsi ya kulipigania na kulilinda taifa letu la Afrika.

Historia ni maisha ya mwanadamu; inayoweza kusaidia kila uzao ujitambue na kubainisha vipaumbele vya maisha kwa kulingana na mazingira husika. Ukiangalia mataifa mengi ya kiafrika, hayana vipaumbele endelevu vya kitaifa. Huendesha mataifa kwa maslahi ya watawala walio madarakani kwa wakati husika.

Hili husababisha kila mtawala kuwa na mawazo yake tofauti na mtangulizi wake. Hata baadhi ya miradi yenye kuwa na tija kwa taifa, inaweza kutupwa chini na utawala mpya kama hauna maslahi nayo. Hali hii imezidi kulitesa bara letu la Afrika kwa kiwango kikubwa sana.

Wakati nimetembelea makumbusho ya Kigoma kipindi fulani, nilimuuliza mhabarishaji wa kituo hicho, iwapo angekuwa tayari kujifunza historia mpya inayowaonyesha mababu zetu kiasili ni watu mashujaa pasipo kumuonyesha mkoloni kama mtu mwenye nguvu zaidi?

Majibu yake yaliniumiza sana kwa kuwa alichokiwaza na jinsi gani atapata fedha na siyo historia halisia! Kwake fedha ni muhimu kuliko asili yake. Hofu yangu ni je, wako wangapi waliotayari kuuza utu wao kwa lengo tu la kupata fedha? Ni wangapi wako tayari kuuza asili yao, miiko yao kwa lengo tu la kupata fedha? Ingekuwaje kama wazee wetu nao wangetuuza kwa maslahi yao binafsi ingekuwaje?

Mrisho Mpoto katika moja ya wimbo wake alisema ‘kuanza upya si ujinga’. Nafikiri umefika wakati tuitafute historia yetu halisia na kuwafundisha watu wetu kwa maslahi mapana ya kitaifa kama waafrika. Kufanya hivi kutasaidia vizazi vijavyo kujua jinsi ya kujitenga na mkoloni mwenye lengo kututawala milele yote. Mungu atusaidie.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni 0712246001; [email protected]

Columnist: www.habarileo.co.tz