Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TRA wajifunze kwa Zakayo

Fa9984de2bb84f17a67a5939f129719e TRA wajifunze kwa Zakayo

Tue, 6 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“ Yule Zakayo ni mtu mfupi, alitaka kumuona Yesu, alipanda juu ya mkuyu, Yesu akamwiita, Zakayoo njoo Zakaayo njoo, shuka juu ya mti.” Huu ni wimbo wa kwaya niliusikia utotoni mwangu. Nilijiuliza sana kuhusu kisa cha Zakayo na Yesu.

Kwenye Biblia inaandikwa kuwa, Zakayo alikuwa mkusanya kodi. Alikuwa dhalimu kwa watu, aliwanyanyasa katika kukusanya kwake kodi. Siku Yesu alipofika kwenye mji wao, umati wa watu ulikusanyika. Zakayo naye alitaka kumwona Yesu.

Kwa vile alikuwa mfupi alipanda juu ya mti wa mkuyu. Yesu akamwona, akamwita: “Ewe Zakayo shuka juu ya mti.” Yesu akaenda hadi nyumbani kwa Zakayo. Tendo hilo lilimstaajabisha Zakayo.

Wanazuoni wa kikristo huenda wanaweza kukifafanua zaidi kisa hiki. Lakini, tukirudi kwenye swali; je, TRA wana cha kujifunza kutoka kwa Zakayo? Jibu: Ndio, yumkini katika kutekeleza majukumu yao, kuna watu walikanyagwa na Zakayo.

Hata hivyo tuamini kuwa Zakayo alikuwa na nia njema ya kuongeza mapato ya kodi ya dola. Zakayo alihitaji tu kuelimishwa kuwa walipa kodi wale ni sawa na kuku wa mayai.

Tunahitaji mayai yao, lakini itakuwa ni ujinga tukiwachinja kutoa mayai tumboni. Maana kwa kila kuku tutapata yai moja tu na mengi tutayakosa, ni hasara. Nini Zakayo alipaswa kufanya?

Jibu: Zakayo alipaswa kufanya mawili; Mosi, kuhakikisha kuku wale wa mayai wanaishi na kila kuku atage mayai. Hata kama kwa kuchelewa kutaga lakini mwisho wa siku atage tu, vinginevyo, kuku huyo atakuwa anatumalizia chakula chetu, achinjwe tu, hakuna namna.

Pili, Zakayo alipaswa kuhakikisha anaongeza vifaranga wapya. Hivyo, kuku wengine wengi zaidi wa kutaga mayai kupatikana. Hivyo, kupanua wigo wa kukusanya kodi.

TRA wana cha kujifunza kutoka kwa Zakayo. Vinginevyo lengo la kukusanya Sh trilioni tatu kwa mwezi litakuwa gumu kulifikia. Nini adili ya yote haya? Ni imani ya wengi kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan ataendelea kuimarisha nidhamu ya kitaifa ikiwamo tabia ya kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi.

Kutuondoa pia katika kuthamini vya kigeni tu. Ni ile hulka ya kuona kila kitokacho nje ni bora kuliko vya kwetu. Kwamba tuendelee kuwaelimisha watu wetu kutumia fursa na rasilimali zao.

Kwamba kuamini kuwa elimu ni ufunguo wa maisha. Hayati Baba wa Taifa pia aliwahi kulisema hili kuwa tunabadilishiwa dhahabu na kipande cha chupa halafu tunachekelea kama Zuzu.

Ni wazi machungwa yetu yataendelea kuchezewa ‘mdako’ hadi tutakapo funguka macho. Ni hivi, Jamhuri yetu na ikope pesa popote, iombe misaada kokote ili mradi watu wapate elimu bora kuanzia shule za msingi, sekondari, elimu ya watu wazima, ufundi na vyuo vikuu.

Leo kuna mbumbumbu wanaoshikilia ofisi za umma hawatofautishi soko huria na maslahi ya taifa. Kwao soko huria maana yake hata kazi ya uratibu ‘regulatory’ ya serikali haipo tena.

Hawa ni mzigo mkubwa sana kwa taifa, maana tunawalipa mishahara kwa kodi zetu. Wizara za Viwanda na Biashara iwe na msaada kwa mwananchi wa kawaida, ihimize ubunifu, itafute masoko kwa kushirikiana na wizara nyingine.

Tunaposema tunawekeza kwenye sayansi na teknolojia isiwe na maana ya simu za mikononi. Tuwe na mipango ya kubuni kwenye zana za kilimo, tekinolojia ya mnyama-kazi kama punda ili kumpunguzia kazi mkulima.

Tuwe na matumizi endelevu ya nishati ili kupunguza ukataji miti hovyo. , tuboreshe mazingira “ya uwekezaji” na kuongeza “pato la taifa” kupitia TRA

Columnist: www.habarileo.co.tz