Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TFF ya Malinzi, Yanga ya Manji zilipitia mengi

Mwesigwa Pic Data TFF ya Malinzi, Yanga ya Manji zilipitia mengi

Wed, 9 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Alifahamika zaidi kwa wadau wa soka alipoajiliwa kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, baadaye akahamia TFF, akiwa katibu mkuu wa shirikisho hilo la soka nchini, Selestine Mwesigwa alipitia mikikimikiki iliyomuweka jela kwa miaka kadhaa.

Ilikuwa ni mwishoni mwa Juni, 2017 vuguvugu la Mwesigwa na aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi kukamatwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuai na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) lilianza kusikika.

Sekeseke hilo liliendelea kwa watuhumiwa hao kukaa mahabusu hadi Desemba 11, 2019 walipohukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini. Mwesigwa alitakiwa kulipa Sh1 milioni na Malinzi aliyetiwa hatiani kwa shtaka moja la kutengeneza nyaraka za uongo akitakiwa kulipa Sh 500,000, walilipa faini na kuachiwa huru asubuhi ya Desemba 12 pale kwenye Gereza la Keko.

Katika kesi ya jinai namba 213/2017, washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka 20 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha ambazo ni Dola 173, 335 za Marekani.

“Sikuwahi kuwaza kuwa ipo siku nitakaa jela, japo sitaki kuyakumbuka yale maisha, lakini huwa naamini kila kitu kinatokea kwa sababu,” anasema Mwesigwa ambaye safari yake ya soka ilianzia shule ya msingi, sekondari kisha chuo kikuu kabla ya kutua Yanga.

HARAKATI ZA YANGA

Mwesigwa aliyefanya kazi na Yusuf Manji akiwa mfadhili na mdhamini kisha mwenyekiti wa klabu ya Yanga, anasema; “Nilicheza hadi Ligi Daraja la Pili nikiwa mkoani, baada ya hapo nikawa na majukumu mengine, masomo ndiyo yaliniondoa kwenye maendeleo ya kipaji changu, wazazi wengi wa Kiafrika wakati ule hawakuwa na mapenzi na mpira, nakumbuka hata baadhi ya walimu walikuwa wakiwambia wazazi wangu, kijana wenu ana akili lakini anapaswa kujiepusha sana na masuala ya mpira.

“Ila kilikuwa ni kitu ambacho kiko kwenye damu yangu, sikuacha hadi nilipokuwa chuo kikuu, nilifanya kazi kwenye mashirika ya kimataifa ya kiraia niliendelea kufanya kazi ya kusapoti watoto kupata vifaa na maeneo ya kuchezea.

“Nakumbuka kuna mradi ulipita mikononi mwetu na ndiyo ulijenga Uwanja wa Ruvu Mlandizi nikiwa kwenye shirika la Plan International, lengo lilikuwa kuwasaidia watoto wa shule ya msingi lakini baadaye jeshi kwa kuwa tulikuwa na ushirikiano nao ukabadilika na kutumika kwenye Ligi Kuu, ingawa watoto pia walikuwa na fursa ya kuutumia,” anasema.

Anasema akiwa anafanya kazi hizo, alishawishiwa na watu wengi wa mpira kujiunga nao, akimtaja miongoni mwao kuwa ni Kocha Syllersaid Mziray (sasa ni marehemu).

“Sikuwa na mapngo huo kabisa, na sikuwahi kuwaza kama ipo siku nitahusika katika uongozi wa mpira moja kwa moja, japo nikiwa chuo kikuu Yanga iliwahi kunitumia ili kuanzisha matawi Kanda ya Ziwa, sikuwa mwajiriwa.

“Hadi kuwa katibu mkuu wa Yanga kuna watu wengi walihusika, japo kuna kazi moja ya maendeleo tulifanya nikiwa na Mzee Mwinyi (Ali Hassan, Rais wa Pili wa Tanzania) kuna watu iliwavutia, ingawa kabla ya hapo Imani Madega akiwa Yanga lakini pia alikuwa mwenyekiti wa Soka Mkoa wa Pwani aliwahi kunishawishi nijiunge nao,” anasema.

Anasema katika shughuli ya Mzee Mwinyi, Mwesigwa akiwa na Shirika la Plan International ndipo alikutana na Davis Mosha, kisha Manji na Llyoid Nchunga.

“Hawa watu kwa pamoja walichangia mimi kwenda Yanga, japo sitaki kuingia kwa undani ni vipi Mzee Mwinyi alihusika, lakini bila yeye hawa wasingenifahamu hadi kuwa katibu mkuu wa klabu hiyo.”

MAISHA YA YANGA

“Lazima niwe mkweli Organisation ya mpira miaka ya nyuma ilikuwa kujitolea, pia kulikuwa na vurugu nyingi, mara mahakamani, mara mpasuko na vurugu mbalimbali, wakati naingia Yanga, hali ya soka letu haikuwa ya utulivu lakini mwishowe mapenzi yangu kwenye mpira ndiyo yalibreki changamoto hizo zote.

“Nilisema wacha niingie, vingine vitabadilika nikiwa humo humo, nimeanza kazi Yanga jambo lililonishangaza na sikutarajia nilikuta ni klabu iliyokuwa inakwenda kuchapisha barua stationary, halafu kesho yake mnashikana uchawi kuwa kuna mtu ametoa siri za klabu.

“Hata vitengo mfano ofisa habari kulikuwa na kitengo lakini hakijawezeshwa, kama katibu mkuu majukumu ya ofisi ndiyo yalikuwa yangu zaidi, nilihakikisha nawezesha watu, kitengo cha habari alikuwepo Sendeu (Luis) nikamuongezea vijana wa kujitolea, Baraka Kizuguto, Dismas Ten na Rose Msamira ili kuimarisha masuala ya mawasiliano sababu kitengo hicho ni suala nyeti.”

Anasema waliweka mfumo wa WiFi ambayo haikuwepo klabuni, wala haikuwa na email adress na kuboresha mifumo mingine ya mawasiliano ofisini.

WAZEE WAMBADILIKIA

Mwesigwa anasema; “Nilishawishi watu kubomoa pale nje, ilileta shida sana, wazee walilalamika, inakuwaje jengo libomolewe, lilipokelewa kwa mtizamo hasi, lakini mimi niliamini kwa kufanya hivyo klabu itakuja kufaidika na wazo hilo nilijifunza kwa timu ya Birmingham City ya Uingereza ambako huko nilikutana na Stewart Hall akiwa kocha wa timu yao ya vijana.

“Niliwahi kufanya kazi ya kujitolea kwenye klabu hiyo, hivyo kuna vitu vingi vya maendeleo ya soka nilijifunza kule, pia nilikuwa nikitembelea timu ya Aston Villa kwa kuwa walikuwa jirani, nakumbuka kipindi cha nyuma kupitia masuala ya Jumuiya ya Madola tulikuwa na ushirikiano na timu za kule.

“Wazee wa Yanga zamani wakiulizwa watakuwa wanafahamu, kuna timu kama sio West Bromwich iliahi kuja nchini na kulala klabuni Yanga, ilikuwa ni kama kubadilisha utamaduni, serikali ilikuwa na nguvu kwenye soka, klabu kubwa zilikuja hapa na timu zetu kwenda baada ya miaka ya 1990 pesa za televisheni zilipoingia kwenye soka nguvu ya serikali kidogo ikapungua.

“Hivyo na mimi muda niliofanya kazi Birmingham ulinisaidia sana na ndicho kilinihamasisha kuanzisha duka la klabu pale Yanga, wazee waliona jengo ni kama linabomolewa linatoka kwenye asili, ilileta shida sana, lakini hilo likafanyika na nashukuru mengi tuliyoanzisha wenzetu wanayaendeleza kwa kiwango zaidi,” anasema.

UCHAKACHUAJI JEZI

Mwesigwa anasema kingine ambacho kilikuwa ni tatizo sugu Yanga ilikuwa ni uchakachuaji wa jezi za klabu hiyo, hivyo akashauri watafute kampuni ambayo itasimamia hilo.

“Kuna muda tulikamata jezi feki nyingi sana, hadi kontena zima lakini kinachotokea hata zile zilizokamatwa uongozi mnakuwa hamjui zimekwenda wapi.

“Lilikuwa ni suala geni, baadhi ya viongozi waliona kama ni jambo ambalo halieleweki, walinishangaa, huyu anatuletea mambo gani? suala la jezi feki lilikuwa tatizo sugu, sasa hivi mambo yamebadilika, klabu zinafanya biashara ya jezi na kupata mapato ambayo nyuma yalikuwa yakipotea.”

KAMATI KUTOINGILIA MAMLAKA

Anasema jingine ambalo lilikuwa ni mfupa sugu ni zile kamati ambazo zilikuwa kwenye mfumo wa utaratibu wa klabu kuishia kwenye mipaka yao.

“Mabosi wangu, Nchunga na Manji tuliweka mambo vizuri kwenye hili, zile kamati ambazo si waajiriwa wa kudumu utendaji wao ulibaki kwenye mipaka yao na kuwa washauri zaidi, tofauti na nilivyokuta wengi wao walikuwa wakiamkia klabuni.”

VUGUVUGU LA UASI TFF

Akiwa katibu mkuu wa Yanga, Mwesigwa anasema alionekana kushiriki katika vuguvugu la uasi akishirikiana na Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na harakati ya kuanzishwa kwa Bodi ya Ligi ambayo wakati huo Ligi ilikuwa ikisimamiwa na Kamati ya Ligi.

“Mimi na Kaburu tulianzisha kamati ambayo haikuwa rasmi, TFF walilichukulia suala hilo kwa namna fulani ya uasi, lengo letu lilikuwa ni kuisukuma TFF kuanzishwa kwa Bodi ya Ligi ili itoke kusimamiwa na kamati ya ligi, ambayo ni kamati ndani ya TFF iliyokuwa kama kamati nyinginezo za shirikisho hilo.

“Nje ya soka, tulikuwa na watu wenye maono, tulifanya jaribio ambalo lilizaa matunda kwa kushirikiana na wenzetu wa Simba, tulikaa pamoja na kutengeneza hiki kitu, japo nayo ilichukuliwa kwa mtizamo hasi kwa baadhi ya watu ambao waliamini Simba na Yanga haziwezi kukaa pamoja na kuwa na uamuzi wa pamoja.”

Anasema waliendelea kufanya harakati hizo, akimtaja Kaburu kujitoa sana na kuna wakati alifanya kampeni kwa kumfuata kiongozi mmoja mmoja ili kufanikisha hilo hadi walipofanikiwa kupata fursa ya kukaa mezani na Rais wa TFF, Leodgar Tenga .

“Mpango wetu ulimshtua sana, lakini tulimhakikishia huo sio uasi kama lilivyopokelewa na baadhi ya watu, lakini tunalenga kuupeleka mpira wetu mbali zaidi.

“Nakumbuka Karia (Wallace ambaye sasa ni rais wa TFF) alikuwa katika kamati ya ligi na wengine baadaye walituunga mkono na ilipoundwa Bodi ya Ligi wao ndiyo walikuja kuwa viongozi wake, ila kabla ilikuwa ni kama vita, tunaamka usiku usiku kulipambani hili.

“Katika harakati hizo tulipendekeza vitu vingi, vingine vilifanyiwa kazi na vingine havikufanyika, lakini nikiangalia bodi ilipo sasa na tulipotoka naona kuna msingi na huko mbeleni itafanya vizuri.”

YANGA YAENDESHWA KITAJIRI

Anasema alipokuwa Yanga, ndiyo ilikuwa timu ambayo ilionekana kuendeshwa kitajiri nchini, lakini ilikuwa na mengi nyuma ya pazia inapitia.

“Nakumbuka kuna kipindi Yanga ilikuwa ikisafiri kwa basi kwenda kucheza Kampala, Uganda, ilikuwa ni shida, klabu zilikuwa zikiendeshwa na wafadhili na si Yanga tu hata Simba.

“Fedha za wakati ule zilikuwa za ufadhili, zilikuwa na shida, kuna msemo unasema amlipaye mpiga filimbi au mpiga zumari ndiye anayechagua wimbo, ndivyo ilikuwa kwenye klabu yetu, mnaweza kusema mnataka tununue mchezaji fulani, lakini kwa anayemlipa mpiga filimbi kama hajavutiwa naye hanunuliwi.

“Nakumbuka tulitoka kwenye ufadhili, tulipata mdhamini Quality Group, lakini ilikuwa ni ufadhili na udhamini kwa wakati mmoja, hivyo vitu vingi anaamua yeye, ilienda hadi akawa mwenyekiti, alitoa fedha nyingi Yanga, ndiyo ilikuwa timu inayojiendesha kitajiri wakati ule.

“Kwenye soka ili mfanye vizuri zaidi, mnahitaji fedha zaidi, Yanga tulikuwa na mdhamini mmoja, akitoa 25 milioni kwa mwezi, mkipata wadhamini wengine akisema hajaridhika na mkataba au hiyo fedha nyingine siitaki, basi mnatulia hivyo ikitokea anayowapa ikichelewa au haitoshi napo ni tatizo.”

Anasema pamoja na Yanga kuonekana ikijiendesha kitajiri, lakini mifumo haikuwa imekaa sawa sawa, japo Quality Group alitoa fedha nyingi sana na kuondoka kwa Manji kulichangia klabu hiyo kutetereka.

“Kuanzia 2016 hali ya uwekezaji katika mpira ikaanza kupungua nchini hadi alipoibuka Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ kuwekeza Simba kidogo mambo yakaanza kwenda vizuri, unafahamu wawekezaji ni wafanyabiashara ili kuwekeza anahitaji kutiwa moyo, ataangalia mifumo ya kodi, mifumo fedha ya nchi, utashi wa kiutawala wa nchi.

“Pia, kujitangaza, hivyo wanahitaji mazingira mazuri ya kisiasa pia, Yanga ilitetereka baada ya Manji kutoka, wakajiendesha kwa kutembeza bakuli, na pale ndipo umuhimu wa kuwa na mtaji wa kutosha wa mashabiki ulionekana na kipindi chote cha msoto haikuwa kutoka kwenye nafasi ya pili katika ligi.

“Waliishi katika mfumo wa ukiwa huna utasema matembele nayapenda sana, ila ukipata nakuanza kula vinono utahoji kama matembele nayo ni chakula, hivyo nao walikuja na lugha ya kujifariji kipindi chote cha msoto wao hadi wakaimarika.”

Anasema katika vitu ambavyo Yanga haipaswi kuvisahau ni uwepo wa Mwinyi Zahera, kwani hajawahi kumuona kocha wa aina ile ya Zahera raia wa DRC.

“Kabla ya Zahera walikuwa na kocha aliwakimbia kwa sababu ya ukata uliosababisha malimbikizo ya mshahara, lakini Zahera aliwaokoa, hali ilikuwa mbaya alikwenda nao hivyo hivyo, binafsi sijawahi kumuona kocha wa hivyo, hakujali kutetereka kwa Yanga.”

YANGA HADI TFF

Mwesigwa alipoacha ajira Yanga, ndani ya muda mfupi aliajiriwa TFF kwenye nafasi ile ile ya katibu mkuu, nafasi ambayo anasema ilikuwa ni makubaliano na Manji.

“Mwenyekiti aliniomba, aliniambia kuna mfumo anautengeneza, lakini wakati huo nilikuwa nimeomba ajira TFF na kufanya usaili nikapita, Manji akaniambia nikae siku 30 na Marehemu Mwalusako (Lawrance) ili kushirikiana naye kabla sijamkabidhi ofisi, japo alikuwa katibu mkuu kabla yangu, hivyo alikuwa akirudi kwa mara nyingine.

“Nilikubali kufanya kazi mwezi mmoja nikiwa na Mwalusako, ulipokwisha nilienda kwenye ajira yangu mpya TFF ambako sikupelekwa na mtu, niliomba mwenyewe baada ya ajira kutangazwa.”

KAZI UPYA

Anasema alipoanza kibarua pale TFF, moja ya vitu vilivyomshangaza ni kuwepo kwa makocha wawili pekee wenye Leseni A ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

“Tena wote walikuwa kwenye utawala, hakukuwa na kocha mzawa anayefundisha klabu mwenye leseni hiyo, akiachana na Sunday Kayuni na Salum Madadi ambao wote walikuwa TFF wakati huo.

“Kuna klabu za Ligi Kuu zilikuwa zikinolewa na makocha wenye uzoefu tu, labda alifundisha sekondari akashiriki kozi fupi na kupewa timu, tuliamua kuanza na club lincensing, tukasema kocha mwenye leseni kubwa basi aanzie B, ikafanyika kozi, walishiriki wengi akiwamo Kidao (Wilfred), Nsajigwa (Shedrack), Mecky (Maxime), Mzee Tenga na wengineo.

“Wengi walishiriki, hadi wakapata Leseni A, tuliwakuta wawili lakini hadi natoka walikuwa 22, pia kulifanyika kozi ya makocha wa makipa, kina Pondamali (Juma), Ivo Mapunda na wengine walishiriki.

“Pia, tulipata marefarii wengi wa renki ya FIFA, ambao walitokana na mafunzo, yalifanyika kwa ukubwa japo ilikuwa ni sehemu ya majukumu yetu kiutawala, pia kitengo cha habari tulikiimarisha na kuja na wazo la kuanzisha TFF TV na sasa wanakwenda kama tulivyofikiria.”

MAMBO MRAMA TFF

Anasema licha ya kuwepo kwa mazuri mengi, lakini changamoto pia zilikuwa ni nyingi, ikiwamo TFF kutopata fedha ya kuhudumia timu ya taifa kwa wakati.

“Umma unasikia mna wadhamini, lakini timu ya taifa hadi inaingia kambini fedha haijaja, hivyo mnaanza ‘kumlilia’ mtu mmoja mmoja, hata fedha za FIFA nazo zinaweza zisiwafike kwa wakati sababu nao wana utaratibu wao, lakini mnapambana hivyo hivyo.”

MADENI YA TFF

Anasema kwenye kodi pia kulikuwa na mifumo isiyoeleweka, TFF iliwahi kubambikiwa kodi na mamlaka, ofisi ikapigwa kufuli na watumishi kuzuiliwa kuendelea na majukumu.

“Tumefika ofisini, getini kuna kufuli, kulikuwa na kitu kinaitwa ‘task force’ ambacho ni chombo kingine zaidi ya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kuna mahali mtu anakubana lazima kutoa fedha, hata TFF ililazimika kutoa fedha ambazo hazikuwa halali, siwezi kuzitaja zilikuwa kiasi gani, lakini waliopo ofisini sasa wanalielewa hilo.

“Ambacho kilituchanganya, TFF na TRA tulikuwa tunafanya mazungumzo, madeni yetu yanajulikana na tunalipa, lakini ghafla tunaletewa deni ambalo hatulijui, lilituathiri na ilifikia hatua wenzetu wa TRA hawakuwa na mamlaka ya mwisho kwenye deni hilo.

“Sijui kama ilikuwa ni profesheno au uamuzi wa kisiasa, lakini kwa kuwa TRA ilishikiria makali, inabidi mkubali na kulipa ili mambo mengine yaendelee

“Haikuishia hapo, wachezaji wa timu vijana walishushwa kwenye basi wakienda kwenye chakula cha jioni ambacho waliandaliwa na Makamu wa Rais kwa ajili ya kuwaaga wakienda Afcon, kisa ni madeni hayo hayo ya kodi.

Columnist: Mwanaspoti