Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TFF izisaidie klabu CAF kwa Ligi Kuu kuanza mapema

Simba Yanga.png Wawakilishi wa Tanzania Ligi ya Mabingwa Afrika

Tue, 21 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara tayari ameshajulikana wakati msimu huu wa 2021/22 ukielekea ukingoni ambapo Klabu ya Yanga imefanikiwa kutwaa taji hilo kabla ya msimu kumalizika rasmi Juni 29, mwaka huu.

Kwa maana hiyo, Yanga ina tiketi mkononi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Simba ambayo imejihakikishia kumaliza katika nafasi ya pili msimu huu kutokana na kufikisha alama 54 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.

Ikumbukwe msimu ujao, Tanzania inaingiza timu nne kwenye michuano ya kimatifa; mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho Afrika.

Na kwa mujibu wa Kanuni za Shirikisho la Soka nchini (TFF), bingwa wa ligi hiyo na mshindi wa pili, wataiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa wakati timu itakayomaliza nafasi ya tatu na itakayotwaa Kombe la FA, zikikata tiketi ya kupeperusha bendera ya Tanzania Kombe la Shirikisho Afrika.

Lakini, kama bingwa wa Ligi Kuu ndiye atakayetwaa Kombe la FA, basi timu itakayoiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika itakuwa ni ile itakayomaliza nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ambayo itaungana na iliyomaliza nafasi ya tatu.

Hivyo, kutokana na msimamo wa Ligi Kuu ulivyo, bado hakuna uhakika wa timu zitakazomaliza nafasi ya tatu na ya nne, huku pia fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga na Coastal Union, ikitarajiwa kupigwa Julai 2, mwaka huu.

Hata hivyo, tayari Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limeshatangaza msimu mpya wa michuano yake hiyo, kwamba utaanza Agosti 12, mwaka huu kwa kupigwa mechi za awali. Hiyo ikimaanisha kutoka tarehe ambayo fainali ya Kombe la FA nchini, itapigwa zitakuwa zimebaki siku 40 tu kabla ya michuano hiyo ya CAF kuanza rasmi.

Kwa ujumla muda ni mchache sana wa maandalizi kwa wawakilishi wetu wa kimataifa, na kuna kila dalili kwa michuano hiyo kuanza kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kuanza jambo ambalo linaweza kuchangia timu zetu kushindwa kufanya vizuri.

Hii ni kutokana na kutambua wazi kwamba mwanzo wa msimu wachezaji wengi huanza kwa kujitafuta kwanza kwenye viwango vyao kabla ya kuanza kuchanganya baada ya mechi nne hadi sita, hiyo ikichangiwa hasa na kupata maandalizi duni ya msimu.

Tunasema hayo, hasa tukizingatia ligi imechelewa kumalizika, hivyo dirisha la usajili litachelewa kufunguliwa na kufungwa pia, jambo ambalo litachangia hata maandalizi ya msimu mpya (pre-season) kwa timu kuwa fupi.

Hivyo, TFF pamoja na Bodi ya Ligi nchini (TPLB), hawana budi kuhakikisha kwanza dirisha la usajili linafunguliwa siku moja tu baada ya ligi kumalizika, lakini ikiwezekana kutangaza mapema msimu wa Ligi Kuu uanze Agosti Mosi, mwaka huu.

Kwa kufanya hivyo, kutawezesha wawakilishi wetu kujipanga na kujiandaa vema kuelekea michuano hiyo, ili kwenda kutoa ushindani wa kweli zaidi na si kuishia kuwa wasindikizaji kwa kushiriki tu.

Tunaamini kama ligi yetu itaanza mapema, kutatoa fursa pana kwa mabenchi ya ufundi ya wawakilishi wetu wa nchi kwenye michuano hiyo kurekebisha makosa huku kukisaidia wachezaji wao kurejea mchezoni haraka zaidi katika mechi za kimashindano.

Madhumuni yetu ni kuona wawakilishi wetu wanakwenda kuipeperusha vema bendera ya Tanzania kwenye michuano hiyo, angalau timu itakayofanya vibaya iishie hatua ya makundi, huku malengo ya kila timu yakiwa ni kutinga nusu fainali na kuendelea kwenye michuano hiyo inayoongoza kwa utajiri barani Afrika kwa ngazi ya klabu.

Columnist: www.tanzaniaweb.live