Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TFF imarisheni ulinzi Ligi Daraja la Kwanza

TFF LOGO TFF imarisheni ulinzi Ligi Daraja la Kwanza

Mon, 6 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKATI tayari Gwambina FC ya jijini Mwanza inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kutoka Kundi A imeshakata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, kumekuwa na malalamiko mbalimbali yanayoendelea kwenye ligi hiyo ya pili kwa ukubwa hapa nchini.

Gwambina FC inayonolewa na mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Novatus Fulgence ina pointi 44, ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine katika kundi hilo msimu huu.

Kwa upande wa Kundi B, ambalo Dodoma FC na Ihefu FC ya jijini Mbeya, ambazo zinalingana pointi, zinaendelea kuchuana na kupambana kusaka tiketi ya kupanda daraja moja kwa moja kutoka kwenye kundi hilo.

Kwa mujibu wa msimamo, Dodoma FC inaizidi mabao ya kufunga Ihefu, hivyo umakini na usimamizi unatakiwa kuongezwa katika mechi zinazohusisha timu hizo ili upangaji wa matokeo usitokee.

Nipashe inalikumbusha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhakikisha waangalizi wa mechi za timu hizo na nyingine kuongezeka kwa ajili ya kupata timu zitakazopanda daraja kihalali na si kwa njia za 'ujanjaunjanja'.

Hii inamaanisha kuwa, timu iliyojiandaa vema na iliyopata pointi zake bila ya 'kubebwa', ndio itakayopanda kwa haki, na kwa kifupi itakuwa tayari kukabiliana na ushindani na changamoto mpya kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao wa 2020/21.

Tunasema hivi, kwa sababu tumeshuhudia baadhi ya timu zikipata pointi za mezani kutokana na wapinzani wao kuanzisha vurugu ambazo zimesababisha mechi kuvunjika na hivyo, kamati husika kuamua ushindi mezani.

Baadhi ya mechi huko mikoani zimeonekana zinachezwa katika mazingira yasiyokuwa salama kabla ya kuanza na ikidaiwa yameachwa kwa ajili ya 'kuwabeba' wenyeji katika kampeni 'chafu' ya kuondoka na ushindi.

TFF wakati umefika wa kuhakikisha mechi zote zinachekwa na kumalizika kwa Fair Play, ili mwisho wa msimu bingwa au timu zinazostahili kupanda daraja zifanikiwe na si kuzipa nafasi klabu zisizojiandaa.

Tunaamini wachezaji wanaotoka katika timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili au mashindano ya Kombe la FA, huungana na nyota waliotamba kwenye Ligi Kuu Bara na wanaocheza soka la kulipwa kuunda kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars).

Kama malalamiko yameendelea kutolewa katika mechi zinazohusisha vigogo wa soka nchini, Simba, Yanga na Azam, haishangazi michezo mingine ambayo haionyeshwi mubashara hali ni mbaya zaidi.

Tufike wakati, TFF iweke wasimamizi ambao wataandika ripoti zisizokuwa na upendeleo wa upande wowote, kwa malengo ya kusaidia maendeleo ya soka hapa nchini na kutojihusisha na 'kampeni chafu' za kuandaa bingwa au klabu za kupanda daraja.

Kwa kufahamu Tanzania imefuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ndani (CHAN), TFF inatakiwa kumwandalia mazingira rafiki Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mrundi Etienne Ndayiragije, ili wachezaji atakaowateuwa wawe ni wenye uzoefu, na si wale ambao timu zao zilipata ushindi ambao hauna mashaka.

Safari ya Tanzania na klabu zake kufanya vema katika mashindano ya kimataifa, inatokana na wachezaji wake kuandaliwa vizuri kuanzia wanaposhiriki ligi za ndani na wasifikiri nyota hao wanaweza kuimarika wanapokuwa kwenye kikosi cha Stars au pale wanaposajiliwa na klabu kubwa.

Inawezekana kupata bingwa wa uwanjani endapo kila timu itafanya maandalizi yanayostahili kabla ya kuanza msimu na kuachana na mbinu 'chafu' za kutafuta pointi nje ya uwanja.

Columnist: www.tanzaniaweb.live