Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

TABIA ZIMEJENGEKA

44dc797f1d057404c83d46d4fbfc1575.png TABIA ZIMEJENGEKA

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tabia zimejengeka,

Si vema zikabomoka,

Ni njema tunasifika,

Vile tunawajibika,

Huu si muda kuchoka,

Hata watu kutucheka,

Tuzidi kuwajibika,

Tujenge taifa letu.

Magufuli lipo fika,

Alitunyosha hakika,

Ofisini tukifika,

Watu tuliwajibika,

Tabia imetushika,

Kazi zinavyofanyika,

Tusije tukabweteka,

Hiyo ni hasara kwetu.

Wananchi lisikika,

Vile tulivyosifika,

Ofisini wakifika,

Kuhudumiwa haraka,

Zamani kucheka cheka,

Kote kulishatoweka,

Tusije nyuma geuka,

Hiyo ni faida kwetu.

Sipitali ukifika,

Waganga wachakarika,

Taratibu zafanyika,

Huduma yako kufika,

Wakati unapotoka,

Moyo umefurahika,

Haya tuzidi kushika,

Kwa maendeleo yetu.

John alisukasuka,

Legelege hakutaka,

Wengi waliwajibika,

Fyekeo liliwafika,

Ili lisije kufika,

Lazima kuwajibika,

Yapo tumefaidika,

Kwa maendeleo yetu.

Sasa ameshatoweka,

Kifo kimeshamteka,

Vizuri mema kushika,

Kila tukimkumbuka,

Tuzidi kuwajibika,

Kwa kazi bila kuchoka,

Huko si kutaabika,

Twajenga uchumi wetu.

Umoja tuzidi shika,

Usije kutetereka,

Tuzidi kujumuika,

Mema yetu kitendeka,

Tuendako tutafika,

Bila ya kubabaika,

Hiyo ninayo hakika,

Tukifanya kazi zetu.

Na Lwaga Mwambande (0767223602)

Columnist: www.habarileo.co.tz