Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Stars Kombe la Dunia mbona inawezekana!

Stars Stars Kombe la Dunia mbona inawezekana!

Sun, 17 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

WIKI iliyopita ilikuwa ya faraja kwa soka la Tanzania baada ya timu zetu za Taifa - ile ya wanawake ‘Twiga Stars’ kufanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Shirikisho la Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) kwa wanawake yaliyofanyika nchini Afrika Kusini, lakini pia ile ya wanaume ‘Taifa Stars’ ilipata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Benin katika mashindano ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Stars ilifanikiwa pia kuongoza kundi na kurejesha matumaini ya Watanzania ambayo kwa kiasi kikubwa yaliamshwa na timu hii katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi pale ilipopata matokeo ya sare kwenye mechi dhidi ya DR Coongo iliyochezwa Lubumbasi nchini humo na kujenga imani kuwa inawezekana kapata nafasi ya kuvuka hatua hii na kuingia katika hatua ya kumi bora.

Matumaini ya kufika mbali hata kama si kushiriki katika fainali za Kombe la Dunia za mwakani zinazotarajkiwa kufanyika nchini Qatar yanaedana na uhalisia ambao kwa kiasi kikubwa unaonyesha hadi timu ilipofika upo uwezekano mkubwa wa kufanya vyema na wachezaji na benchi la ufundi kutengeneza historia kama walivyoweka historia wachezaji wa zamani kina Leodegar Tenga walipofanikisha kwa mara ya kwanza kushiriki Fainali za Afcon 1980 zilizofanyika nchini Nigeria.

Ukiangalia katika makundi kumi ambayo timu zitakazoongoza ndizo zitaingia katika hatua ya kumi bora ambapo kwa sasa zimekwishachezwa mechi nne na kubaki mbili tu kabla ya kumaliza hatua hii, utagundua kuwa timu zenye uzoefu wa kushiriki Kombe la Dunia hunufaika na uzoefu wake.

Ni vivyo hivyo pia timu ambazo hazijawahi kufika hatua ya fainali nazo hunufaika na kutoshiriki kwake, hivyo kuwa na utashi wa kutaka kuandika historia kwa kuwa siku zote historia huandikwa na waliofaikiwa na sio walioshindwa kama ilivyofanya timu ya aifa ya Senegal iliposhiriki fainali za Kombe la Dunia mara ya kwanza 2002 nchini Japan na Korea kusini.

Katika makundi hayo ukiangalia Kundi A timu za Algeria na Burkina Faso ndizo zinaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa kuongoza kundi hilo - zote zikiwa na alama 10, huku Ageria ikionekana kunufaika na uzoefu ilionao wa kushiriki katika fainali hizo ambayo imeshiriki mara nne, huku mara ya kwanza ikiwa ni 1982.

Katika Kundi B, timu ya Tunisia ina nafasi kubwa ya kufanikiwa kuingia hatua ya pili ikiwa inaongoza kundi hilo kwa alama 10 na yenyewe pia ikiwa na uzoefu wa kushiriki katika fainali hizo kwa kuwa imeshiriki mara tano, huku mara ya kwanza ikiwa ni 1962.

Katika kundi C timu ya Taifa ya Nigeria inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuingia katika hatua ya mwisho kwani hadi sasa ndio inaongoza kundi hilo ikiwa na alama tisa ikifuatiwa na Cape Verde yenye alama saba. Hivyo Nigeria pia inaonekana kuendelea kunufaika na uzoefu ilionao wa kushiriki Fainali za Kombe la Dunia ikiwahi kushiriki mara sita, huku mara ya kwanza ikiwa ni 1994.

Katika kundi D - Ivory coast na Cameroon zinaonekana kuwa na nafasi kubwa licha ya Ivory coast kuongoza ikiwa na alama 10, huku Cameroon ikiwa nazo tisa, lakini nafasi kwa timu zote mbili kuwa wazi kutokana na uzoefu walionao kushiriki fainali hizo, hivyo kuonekana kuwa na ushindani ulio sawa ambao unahanikizwa na uzoefu katika Fainali za Kombe la Dunia.

Katika Kundi E - Mali ambayo haijawahi kushiriki Kombe la Dunia inaongoza kundi, hivyo kuwa sawa na Tanzania ambayo inaongoza Kundi J ikiwa na alama 10 ikufuatiwa na Uganda yenye nane, hivyo zote kuonekana kutaka mafanikio na kuwa na nafasi ya kufika kumi bora kupitia mechi mbili zilizosalia.

Kama ambavyo timu hizo zinavyotaka kuweka rekodi kadhalika Tanzania pia ina nafasi hiyo katika Kundi J ambayo inaongoza ikiwa na alama saba ikifuatiwa na Benin yenye nazo saba, hivyo kufanya zote mbili kuwa na fursa iliyo sawa, ingawa zote pia hazijawahi kushiriki Kombe la Dunia, hivyo kuwa na utashi wa kutaka kutengeneza historia.

Katika Kundi F timu ya Taifa ya Misri inaonekana kuwa na nafasi kubwa kuvuka hatua ya pili, kwani inaongoza ikiwa na alama 10 ikifuatiwa na Libya yenye alama sita. Misri ina uzoefu wa kushriki mara tatu Kombe la Dunia mara ya kwanza ikiwa ni 1934.

Kwa Kundi G Afrika Kusini inaongoza na alama 10 ikifuatiwa na Ghana yenye nazo tisa, hivyo kuwa na fursa shindani kwa timu zote kutokana na uzoefu wa kushiriki Kombe la Dunia, ambapo zimewahi kushiriki mara tatu - Afrika Kusini mara kwanza ilikuwa 1998, huku Ghana ni 2006.

Katika Kundi H timu ya Senegal na kundi I timu ya Morocco ndizo mbili pekee zilizoshinda mechi zote nne katika makundi na kuwa na alama 12 na kuwa timu za kwanza kuvuka na kuingia hatua ya kumi bora - alama ambazo haziwezi kufikiwa na timu zote katika makundi hayo kwenye mechi mbili zilizosalia, hivyo kuendelea kuthibitisha kunufaika na uzoefu wa kushiriki fainali hizo mara kadhaa.

Hivyo, kwa uhalisia huo katika makundi hayo kumi na rekodi ya timu mbalimbali utaona kuwa Tanzania pia ina nafasi ya kuweka rekodi kama tulivyoona kwa baadhi ya mataifa kama vile Senegal ilivyofanya 2002. Na hii ni hasa ukizingatia kuwa kwa sasa zimesalia mechi mbili ambazo Taifa Stars itacheza moja ugenini dhidi ya Madagascar ambayo haina nafasi ya kuongoza kundi na ya pili itakuwa nyumbani dhidi ya DR Congo, hivyo kuwa na uwezekano wa kupata matokeo chanya iwapo timu itajiandaa vizuri.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz