Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Spoti Dokta: Mwili wa kispoti unatengenezwa hivi

Mwili Wa Mchezaji Mwili wa kispoti unatengenezwa hivi

Fri, 20 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Katika ulimwengu wa kisasa watu wa kawaida hununua mavazi na vifaa vya kimichezo na kuvaa, huku pia huvutika kuwa na mwonekano wa kispoti kama walivyo wanamichezo mastaa.

Muonekano wa kispoti unaonekana kuwavutia mashabiki duniani ikiwamo wenye miili minene kuhamasika kufanya mazoezi ya kimwili ili kuupata mwili wa kispoti.

Ni kawaida vijana wanaoenda na wakati kupenda kuvaa mavazi ya kimichezo kama vile fulana, pensi, kofia, raba au track suti za michezo na miwani yote hii ni kutaka kuupata mwili wa kispoti.

Huwa na ndoto za kuwa na umbo la kispoti kama anavyooneka Cristiano Ronaldo, Adama Traore, Zlatan Ibrahimovic au kwa hapa Bongo kama vile Stephane Aziz Ki, Khalid Aucho, kwenye soka au Hassan Mwakinyo katika ndondi au Ali Kiba ambaye ni mwanasoka-mwanamziki.

Kijana anapoupata mwili wa kispoti huwa ni fahari kubwa wakati kwa mtu mzima hujiona mpya anapopata mwili huo kwani kumfanya naye kuvaa mavazi ya kimichezo ambayo huibamba vyema miili hiyo.

Wenye kuvutika zaidi hupendelea kukata futa la kitambi ili kupata umbo la tumbo kakamavu lijulikanalo kama ‘six pack’, umbo ambalo linatokana na misuli ya tumbo kutuna kutokana na mazoezi au kazi.

Umbo la kispoti haikushangaza kuitwa “sexiest body” kwani umbo hili huwa na mvuto kwa wanawake wa sasa. Umbo hili ndio linalomfanya mwanaume kujiamini.

Umbo la kispoti liko hivi Kwa mujibu wa gazeti maarufu duniani lijulikanalo kama Men’s Health, kuwa na umbo la kispoti ni lile umbo linalowiana vyema kuanzia ukakamavu wa komo la kichwa mpaka dole gumba.

Wakimaanisha kuwa lazima kuwepo na ukakamavu wa kispoti kuanzia juu mpaka chini, misuli ya mwili iwe imejengeka kuanzia kichwani mpaka miguuni.

Mtazame mkimbiaji maarufu duniani Usain Bolt au supastaa wa soka Ronaldo, ndio maumbo ya kispoti yanavyotakiwa kuonekana hata pale wanapobakiwa na nguo za ndani kama boxer.

Huwa wamejengeka vyema kuanzia chini mpaka juu, ikiashiria takribani asilimia 80+ ya misuli ya mwili imehusika kufanya kazi mpaka kufikia kujengeka kispoti.

Umbo la kispoti katika majarida makubwa ya michezo duniani kama Men’s Health au Sex Magazine huyaita maumbile haya kama sexiest bodies.

Mwanaume kuwa na mwili wenye muonekano mzuri ulio na misuli imara na iliyojengeka ni jambo ambalo linapendwa lakini si kila zoezi linaweza kuujenga mwili wote.

Ronaldo, mwanamitindo Tyson Beckford na mwanamuziki mwanamitindo aliyekua akijirusha visiwani Zanzibar, Tyrese Gibson, wamewahi kupata tuzo ya jarida maarufu duniani la Men’s Health Magazine la nchini Marekani.

Jarida hili ndio linalotoa tuzo ya mwanaume bora wa mwaka mwenye umbo lenye kujengeka na kuvutia yaani umbo la kispoti.

Mazoezi ya kujenga mwili wa kispoti

Wapo baadhi ya wafanya mazoezi ambao hubeba vyuma vizito kiholela ili kuujenga mwili lakini matokeo yake hupata mwili usiowiana kispoti ikiwamo kifua na mikono kuwa mikubwa lakini chini umbo dogo.

Ieleweke kuwa si kila zoezi linaweza kukupa muonekano wa kispoti na pia sio kila zoezi linaweza kujenga mwili wa kispoti.

Yapo mazoezi ambayo yanakubalika na wataalam wa sayansi ya fiziolojia ya michezo na wa mazoezi ya viungo ambayo ndio yanakufanya kujenga mwili wote kispoti.

Mazoezi hayo hujulikana kama ni mazoezi mepesi kitabibu hujulikana kama Aerobics exercise yameonekana kuwa na ukipekee katika kuushughulisha mwili karibu asilimia 80% ya misuli toka juu mpaka chini hatimaye kuendana vyema kimaumbile.

Kama mtu atafanya mazoezi mepesi yafuatayo mara kwa mara angalau dakika 30-60 kwa siku katika siku 5 za wiki sawa na dakika 150-300 kwa wiki huweza kuleta matokeo chanya hatimaye kupata umbo la kispoti.

1.Kuogelea

Zoezi hili linaujenga mwili kwani kuogelea kunahusisha misuli mingi zaidi kuanzia miguu, kiwiliwili, mikono na kichwa. Jaribu kuwatazama wavuvi, wapiga mbizi, wanamichezo waogeleaji utagundua wamejengeka kispoti mwili mzima.

2. Kucheza muziki wa kasi

Kucheza muziki, lakini sio muziki laini kama ilivyo bluzi au taarabu asilia. Muziki changamfu kama wa dansi, afro, house, hot funky, pop na ngoma za kitamaduni inahusisha kuchezesha misuli mingi mwilini hivyo kufanya misuli mcheza mziki kufanya kazi sana.

3. Kukimbia

Mwanadamu anapokimbia huweza kuhusisha misuli ya mwili mzima. Ukiwatazama wanariadha wengi duniani wana miili imara yenye misuli iliyojijenga vema ikiwamo Alphonce Felix Simbu wa JWTZ. Upo ushahidi wa kitafiti unaoonyesha ufanyaji wa zoezi hili kuchangia mamilioni ya wakimbiaji kuwa na miili iliyojengeka huku wakiishi maisha marefu zaidi.

4. Michezo ya kila siku

Michezo kama sarakasi, michezo ya karate, mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mchezo wa rugby na kuendesha baiskeli yanaweza kujenga misuli na kuleta umbo la kispoti.

5. Kutembea umbali mrefu

Kutembea umbali mrefu angalau kilomita 2.5-5 kwa siku huku ukitupa mikono na miguu kama vile mwanajeshi wa nchi kavu (Infantria) katika siku 5 za wiki. Zoezi hili ndio rafiki kwa watu wenye umri mkubwa wanaohitaji kujenga mwili wenye afya njema hatimaye kuupata mwili wa kispoti.

6. Unyanyuaji wa vitu vya uzito wa wastani

Unapofanya mazoezi mepesi unaweza kuchanganya na mazoezi ya gym ikiwamo unyanyuaji wa vitu vya uzito wa wastani au kusukuma vitu vya uzito wa wastani.

7. Kazi hizi

Kazi kama vile za bustani au kilimo, kazi za ndani, wapagazi, watembeza bidhaa, makuli, wasukuma matoroli, mafundi mbao na wabeba mizigo ni kazi ambazo huweza kuushughulisha mwili bila ya mazoezi hatimaye mwili kujengeka kispoti.

Chukua hii

Kadiri unavyozidi kuwa na hamasa ya kufanya mazoezi ndivyo pia huleta matokeo makubwa kwa kukupa mwili wa kispoti pamoja na kukupa mwili wenye afya njema hatimaye kuishi maisha marefu.

Mazoezi haya ndio yanachangia mamilioni ya wanamichezo duniani kuishi muda mrefu zaidi ukilinganisha na wasiofanya mazoezi haya kwani yanawaepusha na magonjwa yasiyoambukiza.

Mazoezi ndio chanzo cha kuwa na mwili imara wenye afya njema hivyo kuepukana na maradhi yasiyoambukiza ikiwamo kisukari cha aina ya pili, maradhi ya moyo, kiharusi na unene uliokithiri.

Ili kuweza kuleta matokeo makubwa itahitajika kuwa na mwenendo na mitindo bora ya kimaisha ikiwamo mlo kamili uliozingatia kanuni za lishe.

Mienendo na mitindo mibaya ya kimaisha ni pamoja na ulaji holela wa vyakula vyenye mafuta mengi, wanga na sukari nyingi, unywaji pombe kupita kiasi na utumiaji tumbaku. Ikumbukwe ulaji holela ndio chanzo cha unene uliokithiri hivyo kuharibu ule mwonekano wa ukakamavu wa mwili wa kispoti.

Panga ratiba ya mazoezi haya na shikamana nayo yawe ni sehemu ya maisha yako kwani si tu yanaujenga mwili kispoti bali pia kukufanya kuwa na afya.

Columnist: Mwanaspoti