Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Spoti Dokta: Kugongwa kichwani na kufariki

Marc Vivieen Foe Wachezaji wa Cameroon wakiwa na picha ya Marehemu Marc Vivien Foe

Sat, 28 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki iliyopita tasnia ya soka nchini ilipata pigo mara baada ya mchezaji wa timu ya vijana ya U17 Singida Big Stars, Mohamed Banda kugongana na mchezaji mwenzake na kufariki uwanjani.

Tukio hili la kusikitisha la ajali ya kimchezo lilitokea Januari 19, 2023, Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa Magereza mkoani Singida wakati timu hiyo ikiwa mazoezini ndipo walipogongana vichwa na mchezaji mwenzake wakati wakiwania mpira wa juu.

Jitihada zilifanyika kumpa huduma ya kwanza pale uwanjani lakini baadaye ikaonekana hakuwa anapumua tena wala kuonyesha dalili za kuwa hai hivyo kumkimbiza ya Hospitali ya rufaa ya mkoa.

Kama ilivyo taratibu za kitabibu ambazo zinaendeshwa kwa miongozo ya kitiba ililazimika kumpeleka katika Hospitali ya mkoa ya Rufaa Singida kwa ajili ya uchunguzi na kujiridhisha kama hakuwa amefariki.

Taarifa ilitolewa na wataalam wa tiba kuwa mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 17 ilielezwa kuwa tayari alikuwa ameishafariki.

Ilikuwa ni taarifa ngumu kuipokea hasa kwa wachezaji ambao ni muda mfupi wakishiriki naye mazoezi. Haikua na jinsi tena Zaidi ya kuipokea taarifa hiyo.

Ajali kama ile na kutokea kifo hapohapo uwanjani zinatokea kwa uchache hapa nchini na haijawahi kuwa ni tishio kiasi cha kuweza kukataza vijana wasicheze mchezo huo.

Hili linathibitishwa na takwimu za ajali za michezo hapa Tanzania ambazo hazihitaji kuwa mtafiti wa kina kizijua.

Ni ukweli usiopingika kuwa mchezo wa soka ni burudani na pia ni ajira kwa vijana ila ajali za mchezoni ikiwamo kugongana au kukumbana ni ngumu kukwepa kwani mchezo wa soka unahusisha kukabana au kuruka kunyang’anyia mipira ya juu.

Lakini baadhi wamekuwa wakijiuliza imekuaje mpaka wamegongana kichwani kiasi kwamba mgongano huo kusababisha kifo kwa mchezaji mwingine.

Mara nyingi mchezo unaosababisha ajali mbaya za kichwa na kujeruhi ubongo ni pamoja na mchezo wa Pikipiki, Baiskeli, magari ya kasi, wateleza katika barafu na wacheza mpira wa magongo.

Wengi hatujazoea kusikia katika mchezo wa soka kuna ajali za kugongana kichwani na kufariki.

Leo nitawapa ufahamu wa ajali kama hii kutokea na kusababisha kifo sababu inakuwa ni nini.

Majeraha ya ubongo yako hivi

Ajali ya kichwani inayohusisha kujeruhiwa kwa ubongo kutokana na kugongana na kitu kigumu kizito inaweza kuleta athari za muda tu au athari za kudumu.

Ajali kama hizi kwakuwa zinahusisha eneo nyeti la mwili pale inapotokea mgonjwa atahitaji kuchunguzwa haraka viashiria na dalii alizonazo.

Wakati huo huo mjeruhiwa wa kichwa atahitajika kupewa msaada wa huduma ya kwanza ili kuokoa uhai au kuzuia madhara zaidi ikiwamo, atapewa usaidizi wa upumuaji, kuongezewa hewa ya oksijeni na udhibiti mwenendo wa msukumo wa damu.

Katika ajali za kichwani zinaweza kuanishwa katika makundi matatu ikiwamo daraja la kwanza ambalo huwa ni kutikisika kwa ubongo pasipo kuhusisha uvujaji damu ndani ya ubongo concussion.

Aina hii ya jeraha huwa na athari za muda tu na inaweza kuhusisha upoteza fahamu au kupoteza kumbukumbu kwa sekunde mpaka dakika kadhaa.

Daraja la pili la ajali ya kichwani ni kupata ajali na hatimaye ubongo kuchubuka na kuvimba bila kuchanika kwa tishu za ubongo, inaweza kuwa katika jeraha la wazi au lisilo la wazi la kichwa. Kitabibu jeraha hili hujulikana kama contusions.

Daraja la tatu ndio jeraha baya la kichwa kwani linahusisha kuchanika kwa tishu za ubongo mara baada ya kugongwa au kupigwa na kitu kizito kichwani, kitabibu hujulikana kama Brain Laceration.

Pamoja ya kwamba ubongo wa mwanadamu umepewa ulinzi na mfupa wa kichwa ambao ni moja ya mfupa mgumu sana usiovunjika kirahisi lakini kugongana na mfupa mwingine wa kichwa ni tatizo.

Hali ya kutojua kuwa kuna kitu kizito kinakuja kutua kichwani kinafanya mwili usiwe katika hali ya kujihami hivyo huwa ni hali ya ghafla tu.

Kifo kinatokea kwa sababu hizi

Kugongwa na kufariki ni dhahiri kuwa ubongo ulijeruhiwa na kunawezakana pia damu ilivuja mara baada ya tishu za ubongo kupata mchaniko.

Ubongo ndio hudhibiti mambo yote ya mwili ikiwamo upumuaji, udundaji wa moyo, utambuzi wa mambo mbalimbali na hisia zote za fahamu.

Ajali ya kichwa inaweza kutokea na kusababisha eneo linalodhibiti tendo la upumuaji kuathirika hivyo kushindwa kudhibiti tendo hili hatimaye kifo kinaweza kutokea.

Hata pale ubongo unapochanika na kuvujisha damu katika tishu za ubongo ina maana kuwa ile mishipa ya damu inayopeleka damu katika ubongo imepasuka hivyo tishu hizo itakosa damu.

Huchukua dakika 5 tu seli za tishu za ubongo kufa pale inapokosa damu yenye oksijeni.

Ajali za kichwani zinaweza kusababisha majeraha katika tishu ambazo nyingine huwezi kuziona kwa macho labda mpaka kwa darubini.

Kugongwa na kitu kichwani kunaweza kusababisha ubongo kuburuzuka au kujigonga kwa kasi katika kuta za mfupa wa fuvu hatimaye ubongo kujeruhiwa na kuchanika na damu kuvuja.

Ajali hizi zinaweza kusababisha mpaka mfupa kuvunjika au kubonyea hatimaye tishu za ubongo kujeruhiwa.

Ukubwa na athari za jeraha la kichwani hutegemea pia na uzito, ugumu na kasi ya kitu kilichoganga kichwa na vile vile eneo gani limepiga kichwani.

Mfano eneo la mfupa wa pembeni eneo jirani na sikio linaweza kumweka mtu hatari ya kufariki kutokana na mishipa muhimu ya damu inapita hapo kuingia kutawanya damu katika ubongo. Ushauri Kilichotokea ni ajali ya kimchezo tu, ila ni vizuri wachezaji kuchukua tahadhari na kujifunza mbinu za kuepuka majeraha ya kichwa wakati wa urukaji au wa kinyang’anyiro cha mipira ya juu.

Columnist: Mwanaspoti