Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Sote tutakufa, lakini tumwachie Mungu’

D9eba563208a1a9636f9ebd4f24ce834 ‘Sote tutakufa, lakini tumwachie Mungu’

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“NDUGU wananchi kwa masikitiko makubwa nawajulisha kuwa leo tarehe 17, Machi mwaka huu, 2021 majira ya saa 12 jioni tumempoteza kiongozi wetu shupavu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk John Pombe Joseph Magufuli ambaye amefariki kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Mzena, Jijini Dar es Salaam…”

“Mipango ya mazishi inafanywa na mtajulishwa, nchi yetu itakuwa katika kipindi cha maombolezo kwa siku 14 na bendera zitapepea nusu mlingoti. Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Ahsanteni sana,” ni maneno ya Makamo wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alipolihutubia taifa, kupitia Televisheni ya Taifa (TBC) kutoka mkoani Tanga.

Makamu wa Rais alikuwa kwenye ziara ya kikazi na kisha kalazimika kuitangazia dunia kifo cha kipenzi cha Watanzania, Rais Magufuli tarehe 17/3/2021, saa tano usiku.

Baada ya tangazo hilo mara moja mitandao ya kijamii ndiyo iliyokuwa ya kwanza kusambaza habari hii huku kila mmoja ikionesha mshituko mkubwa wa kifo cha Rais wetu, mwana mapinduzi, mtetezi wa wanyonge na mtu aliyetumia nafasi yake kuwapigania wananchi.

Mitandao baada ya habari hii mbaya ya msiba ilitoa picha za video zenye jumbe mahususi za enzi za uhai wake.

“Siku mmoja mtanikumbuka na mimi ninajua mtanikumbuka kwa mazuri siyo kwa mabaya kwa sababu nime-sacrifice maisha yangu kwa ajili ya watanzania masikini kwa hiyo tusimame pamoja tusibaguane kwa vyama, tusibaguane kwa ajili ya dini zetu, tusibaguane hata kwa makabila yetu, sisi tuijenge Tanzania…” ni miongoni ujumbe murua ambao ulikuwa umetawala kwa takribani kwenye kila mtandao wa kijamii.

Kama mwanahabari, mambo makubwa mawili yalinijia kwa haraka kwenye kichwa changu mara baada ya kuona mitandao ya kijamii ikisambaza kwa kasi tukio hili la kifo.

Mosi, ni namna ambavyo Serikali aliyoiongoza hadi mauti yalipomkuta alivyoleta mageuzi makubwa kwenye mawasiliano ya kidijitali kwa ujumla wake kiasi kwamba habari inasambaa kwa haraka hivi. Na uzuri ulikuwa kwamba hii ilikuwa ni habari ya kweli tofauti na zile za kubuni buzi zilizokuwa zikutumwa na wabaya wa nchi yetu mitandaoni.

Ni vyema ikakumbukwa kuwa katika kipindi cha pili cha uongozi wake alianzisha wizara maalumu ya sekta ya mawasiliano ambayo awali haikuwepo inayoongozwa na Dk Faustine Ndungulile.

Vilevile Rais Magufuli atakumbukwa kwa kuendelea kuimarisha sekta ya Habari na Utangazaji kama moja ya sekta za huduma za jamii nchini.

Sekta hii inatoa huduma ambayo ni haki ya msingi ya raia kama inavyotamkwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Ibara ya 18 ya Katiba inasema: (1) Kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.

Pia kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.

Aidha, kutoa na kupokea habari kunatambuliwa duniani kote kuwa ni moja ya haki za binadamu.

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zina matamko rasmi ambayo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais, Magufuli imeridhia kuhusu haki ya kupokea na kutoa habari. Haki hii, kama zilivyo haki nyingine zote, hutolewa kwa kuzingatia wajibu wa kila raia kwa jamii na uhuru binafsi wa binadamu.

Jambo la pili ambalo kwangu ni kubwa pia ni ujumbe mzito na mahususi kwenye video hiyo ambao kwa namna ya kipekee kabisa unamtambulisha Rais Magufuli tofauti kabisa na marais wengi wa Afrika na duniani kote kuwa tayari kujitoa maisha yao kwa ajili ya kuwapigania wananchi wake na hasa wanyonge lakini zaidi sana ni kuweka taifa lenye mshikamano bila kubaguana kwa dini, kabila au rangi huku akimtanguliza Mwenyezi Mungu katika kila jambo.

Mifano ni mingi kwenye eneo hili, itoshe tu kusema kuwa sekta kama madini ambayo awali makampuni ya kigeni yalikuwa yanalinyonya taifa kutokana na mikataba mibovu na kuwaacha wananchi kutoambulia chochote, kuboreshwa kwa miundombinu kama reli, barabara, viwanja vya ndege, ununuzi wa ndege na maboti, elimu, afya na kupiga vita rushwa.

Uwajibikaji kwa watumishi wa Serikali ni miongoni mwa vitu alivyoweza kuvisimamia vema katika kipindi cha uhai wake ambavyo watu wake wanamlilia katika kipindi hiki cha maombolezo katika kila kona ya Tanzania.

Binafsi nilibahatika kusafiri na Magufuli katika ziara zake za kikazi kwenye nchi ya Namibia na Zimbawe mwaka 2019 ambako Serikali na wananchi wa nchi hizo siyo tu walimsifu sana kwa usimamizi wake makini na kuwapigania wananchi wake bali hata vyombo vya habari vya nchi hizo viliripoti kuwa ‘tingatinga na jabali la Afrika limetua’ nchini mwetu!

Kimsingi walimaanisha nchi yao ilikuwa imetembelewa na kiongozi adhimu na kiongozi shupavu ambaye ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine wa Afrika hususani suala zima la kusimamia raslimali za waafrika ambazo zimekuwa zikiporwa na mabeberu.

Pia kitu ambacho bado nimekuwa ninakikumbuka sana kwenye ile ziara ni kila tulipofika na kabla ya kuondoka katika nchi moja na nyingine au tunapowasili alikuwa akielekeza mmoja wetu mkristo na muislamu aombee safari yetu.

Ninakumbuka kakangu na rafiki yangu wa siku nyingi, Mpiga Picha wa Rais, Muhidin Issa Michuzi ndiye aliyeomba dua kwa niaba ya dini ya kiislamu mara tulipotua Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere baada ya kumalizika kwa ziara.

Mwanasiasa nguli, msomi na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi anasema Taifa limepotelewa na kiongozi makini, mnyenyekevu na mcha Mungu ambaye amekuwa akilikabidhi taifa kwa Mungu kwenye kila jambo ambalo amekuwa akilifanya.

Kwa namna ya pekee, wakati wa janga la ugonjwa wa corona Magufuli alikataa kuwafungia wananchi wake ndani na badala yake akaja na dhana ya kulikabidhi taifa kwa Mwenyezi Mungu kwa kufunga na kuomba huku wananchi wakiendelea kuchapa kazi na kufuata masharti yaliyowekwa.

Hii ni tofauti na nchi nyingine ambazo zilifungiana ndani na kusababisha sintofahamu nyingi ikiwemo vifo na hata ghasia.

Pia hadi sasa ni miongoni mwa marais wachache waliokuja na msimamo thabiti ya kuwa makini na chanjo ya ugonjwa wa corona, kwamba lazima tujiridhishe nayo ndipo tuipokee.

Sasa ndio tunaona nchi mbalimbali zilizoendelea, nazo pia zikianza kukataa chanjo hizo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwa chanzo cha baadhi ya vifo.

“Kufa tutakufa tu unaweza kufa kwa malaria, ukafa kwa kansa, ukafa kwa magonjwa mengine kwa sababu kufa kupo lakini kamwe tusimwache Mungu, huo ndio wito wangu tusimame na Mungu,” ni maneno aliyoyatoa Magufuli tarehe 19 Februari mwaka huu akiwa Ikulu, akisisitiza Watanzania kumtanguliza Mungu kwenye kila jambo.

Martha Samtweve, Mwinjilisti na Mwalimu mstaafu kutoka kijiji cha Kifanya, Njombe anasema jambo moja ambalo Magufuli ametuachia ni kumtanguliza Mungu katika kila jambo tunalofanya na amemwombea kwa Mungu amsamehe makosa yake.

Mwalimu Samtweve anasema katika kipindi hiki ambacho Rais Magufuli amelala hawezi, kuzungumza tena kwa watanzania ni muhimu taifa kuenzi mambo yote mazuri ambayo aliyafanya hususan kutanguliza uzalendo wa taifa na kuacha kujilimbilikizia mali.

Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakari bin Zuberi amekaririwa akisema Rais Magufuli alisaidia sana wanyonge, akina mama na wanafunzi na kwamba kilichobaki ni kukubaliana na uamuzi a Mungu kuwa Mungu alimpenda zaidi.

Amemtaka kiongozi mwingine atakayekuja, ambaye kikatiba ni mama yetu Mpendwa Samia Suluhu Hassan kuiga mema ambayo hayati Magufuli ameyafanya.

Mwandishi wa Makala hii ni Mkuu wa Kitengo cha Habari- Wizara ya Habari anapatikana kwa namba 0784 441180 au [email protected]

Columnist: www.habarileo.co.tz