Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sote tushirikiane kukuza neema ya utalii

5a3a63d7776818e6a457b7e96b4dd3e7 Sote tushirikiane kukuza neema ya utalii

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JANA katika gazeti hili tulielezea jinsi neema ya utalii inavyozidi kufunguka nchini, baada ya ujio wa kwanza wa idadi kubwa ya watalii kutoka nchini Urusi katika makundi mawili tofauti kwa kipindi kifupi.

Tunasema ni neema kwa kuwa kwa kipindi kirefu Tanzania ilikuwa ikipokea watalii kutoka Marekani na nchi nyingine za Ulaya na Ulaya Magharibi, lakini si nchi kama Urusi.

Watalii hao 57 kutoka Urusi, waliowasili juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) wakitokea Zanzibar, ukichanganya na wale 53 waliofika Desemba 30, wanafanya idadi ya watalii kutoka taifa hilo kufikia 111.

Kimsingi, hii si idadi ndogo hasa ikizingatiwa kwamba, haya ni makundi ya mwanzo makubwa kutokana nchini humo.

Sisi tunaamini kufunguka kwa neema hii kunatokana na juhudi mbalimbali za serikali katika kukabiliana na changamoto zinazofunga utajiri huu wa utalii hasa katika kipindi ambacho dunia imegubikwa na majanga mbalimbali hasa ugonjwa wa Covid-19, unaoteteresha uchumi wa dunia.

Kwa kitendo cha serikali kufanya wajibu wake wa kukabiliana na changamoto hizo, huku utajiri wa amani na upendo kwa wageni ukiendelea, Taifa hili sasa litaweza kumudu kutumia vyema moja ya matunda ya ulinzi wa rasilimali zake za asili.

Tunapenda kuamini hayo kwa kuwa watalii hao waliokuja nchini na watakaoendelea kuja licha ya uwepo wa janga la Covid 19 duniani , wanafanya hivyo kwa kuwa wanaamini ukweli kuwa Tanzania iko salama na kwa wao kufanya uamuzi wa kuja kuitembelea, sisi tunazidi kupata umaarufu duniani na kuvutia zaidi wageni.

Kimsingi, vuvutio lukuki vilivyo nchini huku vikiwa havipatikane kwingine kokote duniani, amani na usalama, ni mambo yanayowavuta zaidi wageni kuja nchini na haya, lazima yalindwe na kuimarishwa.

Kutokana na ukweli huo, kinachopaswa kufanywa kwa sasa ni kuwafanya wanaofika nchini kufurahia zaidi safari zao ili wanaporejea makwao, wawe mabalozi wa kutangaza vyema neema zilizopo Tanzania.

Pamoja na kutaka wadau mbalimbali wa sekta hii kutimiza wajibu wao ipasavyo, tunapenda kuipa hongera Bodi ya Utalii Tanzania kwa kuwa na mikakati inayoshirikisha sekta na wadau wengine ili kuleta mafanikio makubwa katika sekta ya utalii.

Sisi tunasema, mipango na juhudi hizi haina budi kuwa endelevu sambamba na kuzidi kutengeneza na kuibua masoko katika mataifa mengine yenye watalii wengi, lakini hayana mazoea ya kuja kwetu.

Haya ni mataifa kama Ukraine, Japan na Jamhuri ya Czech ambayo ni masoko mapya, lakini yenye idadi kubwa ya watalii.

Tunasema, ili tuendelee kufaidi neema hii, kila Mtanzania kwa nafasi yake, hana budi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kukua na kupokea watalii wengi ili malengo yaliyowekwa na taifa ya kuwafikia watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025, yatimie.

Tunachohitaji ambacho pia Bodi ya Utalii Tanzania inakiomba, ni wadau mbalimbali kuzidi kutoa ushirikiano ili kutimiza malengo hayo kwani ujio wa watalii ni fahari kubwa kwa Tanzania na neema katika ujenzi wa uchumi imara unaoendeshwa na rasilimali za Tanzania.

Columnist: habarileo.co.tz