Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sopu kambi popote

Sopu Pic Abdul Suleiman ‘Sopu’

Mon, 21 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyobarikiwa vipaji vingi vya wachezaji wa mpira wa miguu na katika hilo hutaacha kumtaja nyota wa Coastal Union, Abdul Suleiman ‘Sopu’ anayezidi kuonyesha kiwango bora katika kikosi hicho.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na nyota huyo ambaye amezungumza mambo mbalimbali yanayohusiana na kazi yake uwanjani.

ALIPOANZIA

Sopu anasema alianza soka katika klabu ya Mbagala Market na kiwango bora alichoonyesha kilimfanya kuchaguliwa kujiunga na Serengeti Boys, kisha safari ya kucheza Ligi Kuu Bara ikaanzia hapo baada ya kujiunga na Ndanda FC msimu wa 2017/18.

“Baada ya hapo nilisajiliwa na Simba (U-20), lakini nilikuwa nafanya mazoezi na timu ya wakubwa ingawa kutokana na uwepo wa wachezaji kama Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima ulinifanya nitafute changamoto kwingine,” anasema.

SERENGETI BOYS

Mchezaji huyo anasema kitu anachojivunia katika kikosi cha Serengeti Boys ni kutoa wachezaji wazuri ambao hadi sasa wanazisaidia timu mbalimbali kama Kibwana Shomari, Dickson Job (Yanga) na Kelvin Nashon wa Geita Gold.

“Ilitupa sifa sana (Serengeti) kuonekana na wengi wetu kusajiliwa klabu mbalimbali. Kiukweli ilikuwa timu nzuri na kila mchezaji aliyekuwa na malengo makubwa ya kufika mbali angelitamani kuwepo sehemu ya kikosi,” anasema.

Akizungumzia changamoto anasema, “wengi wao waliniambia siwezi kufanikiwa katika mpira, lakini hilo sikulipa nafasi kwani maneno hayo yalinifanya nipambane ili nifikie malengo yangu niliyojiwekea jambo ambalo kila kukicha najivunia.”

TRY AGAIN AMPA NENO

Sopu anasema mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ ni miongoni mwa watu wanaomshauri kuongeza juhudi.

“Nafahamiana naye vizuri kwa sababu nilikuwa Simba. Ni kiongozi ambaye anatambua na kuthamini kipaji changu,” anasema.

ANACHOJIVUNIA

Sophu anasema anajivunia sana kucheza kwa muda mrefu bila kupata kadi nyekundu mchezoni.

“Kwa hakika jambo hilo nalifurahia na natamani niendelee na nidhamu hii ili niweke rekodi ya kipekee maishani mwangu.”

ATHARI BENCHI LA UFUNDI

Mchezaji huyo anasema licha ya timu yake kubadilisha makocha mara kwa mara, lakini kiwango chake kinazidi kuimarika kwani kila kocha anayetua anampa nafasi ya kucheza.

“Ni changamoto, lakini hakuna kocha aliyeandikiwa kudumu kwenye klabu moja, hivyo kikubwa ni mchezaji mwenyewe kujituma, kujitambua na kufuata maelekezo unayopewa bila kujali aliyepo kwenye benchi la ufundi.”

ANAYEPENDA KUCHEZA NAYE

Mchezaji huyo anasema katika kikosi anapokuwa na kiungo Gustavo Simon hujisikia fahari uwanjani kutokana na ubora na uwezo mkubwa wa nyota huyo. “Sina maana wengine hawana uwezo ila kiukweli binafsi ninapocheza halafu nyuma namuona yupo Gustavo, naiona timu ikiwa sehemu salama kwa sababu anajua kucheza nafasi nyingi,” anasema Sophu.

ISHU YA MKATABA

Sopu anasema mkataba wake na Coastal Union unamalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa hakuna mazungumzo mapya juu ya hilo, ingawa malengo yake makubwa ni kucheza katika klabu kubwa zaidi zitakazompa nafasi ya kuonekana.

Licha ya mkataba wake kubakisha miezi sita ila anasema kwamba baadhi ya klabu zimeonyesha nia ya kutaka saini yake kwa ajili ya msimu ujao huku klabu za Simba, Yanga na Azam zikionekana kumnyatia kimyakimya.

“Mpira ni kazi yangu na endapo nitapata timu ambayo itakidhi mahitaji yangu, basi nitaenda kuitumikia kwani jukumu kubwa kwangu ni kupambana ili niweze kuisaidia timu yangu kufanya vizuri ili nionekane,” anasema.

MECHI TAMU, ANAYEMVUTIA

Sopu anasema kati ya mechi ambayo hataisahau ni ile ya mchujo (play off) msimu uliopita wakati Coastal Union ilipocheza dhidi ya Pamba FC na kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 5-3 ulioiwezesha kusalia Ligi Kuu Bara.

ANAYEMVUTIA

Sopu anasema nyota anaowaangalia katika soka na anapenda kufikia walipo au kuwazidi ni nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anayekipiga Royal Antwerp ya Ubelgiji na Saimon Msuva anayeichezea klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco.

“Ili kufanikiwa ni lazima kuiga kwa waliokuzidi. Samatta, Msuva ni kioo kwa wachezaji wengi na binafsi huwa nafuatilia sana aina ya uchezaji wao na natamani kufika kule ambapo wamefika au hata kuwazidi,” anasema.

USHAURI KWA VIJANA

Sopu anasema vijana wenzake wanapaswa kutambua soka ni ajira,“kitu kikubwa ni nidhamu, kujituma na kupenda unachokifanya. Waamini kila jambo linawezekana na kinachotakiwa kwao ni uvumilivu tu na kukaza zaidi.”

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz