Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Somo la Historia na kiu ya JPM kuona uzalendo

606f648f254152914238fdd113254971 Somo la Historia na kiu ya JPM kuona uzalendo

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

DHANA ya uzalendo ni pana sana na pengine inawezekana kutoeleweka vyema kwa wengine. Uzalendo ni moja wapo ya hisia za kawaida za mtu, hisia ambazo mtu hujenga dhidi ya jamii yake au taifa lake kwa ujumla.

Ni hisia kwa sababu inahusisha hali ya kuwa na mapenzi ya dhati kwa taifa lake na kuwa tayari kulifia. Kimsingi, mapenzi ni hisia ambazo huhitaji kujengwa, haziji hivi hivi tu.

Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili iliyotolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa la Tanzania mwaka 2015; Uzalendo unaelezwa kama hali ya mtu kuipenda sana nchi yake kiasi cha kuwa tayari kufa kwa ajili ya kuitetea.

Je, unaweza ukakipenda kitu kwa dhati kiasi cha kuwa tayari kufa kwa ajili ya kitu hicho wakati hukijui vyema, kilianza vipi, sasa kiko wapi na wewe ni nini dhima yako katika hicho kitu?

Mara nyingi ili kufanikisha hii dhana kunahitajika mambo mengi sana ya kumjenga mlengwa ili awe mzalendo. Jambo mojawapo la msingi kabisa ni kujua historia taraji kwa mlengwa.

Ni katika muktadha huu, Rais Magufuli amekuwa akisema mara kadhaa umuhimu wa kuwafundisha vijana wetu somo la historia ili kuwafanya waijue vyema nchi yao.

Historia ni nini? Kamusi Kuu ya Kiswahili inaeleza kwamba historia ni elimu ya taaluma ya kumbukumbu za taarifa ya matukio ya zama zilizopita ambazo hufundishwa katika vyombo vya kielimu.

Kwa mantiki hiyo ni kupitia somo la Historia watoto wanajua ni wapi taifa limetoka na msitakabali mzima wa taifa lao linakoelekea. Historia itawafanya vijana waijue nchi yao kwa undani na kuwafanya waipende na kuitetea kwani mtu hukitetea na kukipenda kitu anachoijua vizuri.

Inawezekana kwa namna moja au nyingine baadhi ya wapinzani wa JPM wasimuelewe lakini ni wazi kabisa kwamba somo hili litasaidida kwa kaisi kikubwa katika kujenga na kukuza dhana ya uzalendo.

Imani yoyote inajengwa vyema katika umri mdogo. Iwe ni imani ya kidini, kisiasa au nyingine. Ni katika muktadha huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ametangaza somo hilo kuanza kufundishwa tangu darasa la kwanza kuanzia Julai mwaka huu.

Niwe mkweli, tangazo la Waziri wa Elimu lilinifariji sana kwa kuwa sasa linatuliza kiu ya wadau walio wengi wenye maono mapana ya taifa letu, siyo tu kwa sasa lakini hata miaka ijayo.

Wakati Rais akiwaapisha mawaziri alielekeza jambo hili kutekelezwa lakini kukawa kimya sana na akakumbushia tena Februari 12 akiwa Morogoro.

Waziri wa Elimu Sayansi na Taknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema mara maada ya tamko la Rais kutoka walianza mara moja maandalizi ambapo mpaka sasa wamekamilisha zoezi la kuandaa mihtasari kwa ngazi zote.

Waziri Ndalichako anasema walipokea maelekezo ya Rais Magufuli aliyoyatoa Desemba 9, 2020 ya kutaka somo hilo kuanza kufundishwa ambapo wao kama wizara walianza mchakato wa kuandaa mihutasari ya somo hilo kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita.

“Leo tumemsikia Rais akiwa Morogoro nimuombe radhi kwa kuchelewa lakini nimhakikishie kuwa maelekezo yake tunayafanyia kazi kwa uadilifu na kazi iliyopo sasa hivi ni kuandaa vitabu, tunajua jinsi gani anatamani kuona vijana wa kitanzania wanafundishwa somo la Historia na sisi kama wizara tunamhakikishia kuwa litaanza kufundishwa kwa uweledi mpana,” anasema Waziri Ndalichako.

Anasema kazi ya kuandaa mihutasari ya somo hilo wameshirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Elimu ya Juu, Chama cha Wanahistoria na wadau binafsi.

“Somo hili litafundishwa sambamba na somo la Historia lililopo lakini hili litakua somo la lazima," anasema Profesa Ndalichako.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dk Leonard Akwilipo anasema madarasa ya mtihani ya kidato cha nne na sita yatalisoma bila kulifanyia mtihani kwa mwaka huu lakini wale wa kidato cha pili watalifanyia mtihani huku akisema pia litafundishwa kwa lugha ya Kiswahili kwa Shule zote za Msingi na Sekondari.

Majibu haya ya Waziri yanaleta matumaini makubwa kwa watanzania walio wengi wataifahamu vyema nchi yao.

Kinachosikitisha ni kwamba baadhi ya wadau wameonakana kupinga kasi hii ya Mzee JPM katika kufanikisha somo hili litakalowajengea watoto uzalendo kw anchi yao.

Mfano mzuri ni Ndugu Tundu Lissu, aliyeelezea hofu yake akisema kwamba “serikali inaelekea kurudia makosa ya miaka ya nyuma kwenye suala hili la kufundisha Historia ya Tanzania.”

Anadai Tanzania imekuwa na somo la historia kwenye mitaala yake kwa miaka mingi tangu Uhuru na bado somo linafundishwa katika ngazi mbalimbali za elimu, lakini bahati mbaya eti limejaa “propaganda za utawala” hivyo huenda haya yakajirudia.

Lissu anadai eti kinachotafutwa hapa siyo kufundisha watoto wetu historia bali kurudisha propaganda ya kisiasa ya watawala wetu wa sasa kwa kuiita historia.

Huu ni mwendelezo wa viongozi wetu wa upinzani kupinga kila kitu hata mawazo mazuri kama hili wakiamini ukishakaa uande huo kazi yako ni kupinga tu.

Ni vigumu kuelewa Tundu anaamisha nini anaposema somo hili la Historia ya nchi linalenga kufundisha propaganda za kiutawala.

Pengine anamaanisha pale Historia itakapoonyesha mchango wa TANU, ASP na uhuru wa nchi yetu ndio anaita propaganda za watawala. Lakini kiuhalisia huwezi kuvitenganisha na historia ya nchi yetu kwakuwa katika hivyo vyama uhuru ulipatikana.

Au pengine ana hofu ya kutokuwemo kwenye watu wanaoweza kutajwa katika ujenzi wa uzalendo kutokana na hulka aliyoionesha ya kutetea ubeberu ambao upo kwa ajili ya kunyonya matifa kama hili letu.

Lakini mimi ninamwambia Lissu kwamba wakati mwingine haifai sana kupinga kila kitu hata kama unatumiwa na mabeberu.

Sidhani kama somo la historia ni jipya kwa kuwa lilikuwepo tangu awali lakini kutokana na uliberali historia yetu na vitabu vyake vimetupwa kapuni kama ilivyokuwa kwa Azimio la Arusha na hivyo ‘dozi’ ambayo watoto wanapata kuhusu nchi yao ni kidogo sana.

Natambua kufundishwa kwa somo hili ni njia mojawapo ya kujitenga na uliberali na ubeberu na hivyo wanasiasa wetu wanaotumiwa na mabeberu hawawezi kupenda jambo hilo lifanikiwe ndiyo maana hoja kinzani zinakuwa nyingi. Hata wakati wa makinikia walipinga lakini tulishinda.

Huu siyo wakati wa kusikiliza mawazo hasi hasa kwa watu wanoonyesha wazi kwamba hawana mapenzi mema na nchi yetu. Kama watanzania tuzidi kumuunga mkono JPM kwa maslahi mapana ya taifa letu.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni +255-71224-6001 [email protected]

Columnist: habarileo.co.tz