Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Somo la Comoro Afcon sio mchezo

Ngoma Kavu Timu ya Soka ya Comoro

Fri, 28 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wataalamu wa kandanda wanasema ushindi wa mchezo hasa wenye ushindani hupatikana kwa njia nyingi za ndani na nje ya Uwanja. Njia hizi ni pamoja na ushirikina, wenyeji kuwakaba wageni kwa njia mbalimbali au kumtumia mwamuzi kuipendelea timu ili ushindi uliotengenezwa juu ya meza upatikane.

Hali za aina hii tumeziona katika mashindano na kimataifa ya mabara, Kombe la Dunia, Olimpiki na mengine. Katika fainali za Kombe la Mataifa la Afrika (Afcon) zinazoendelea Cameroon mchezo mchafu wa kulazimisha timu moja ipate ushindi tumeiona katika baadhi ya michezo, lakini kilichotokea Cameroon walipokutana na Comoro ni uonevu wa hali ya juu wa kuhakikisha wenyeji wanasonga mbele.

Katika ushindi mwembamba 2-1 wenyeji Cameroon walitumia mbinu ziliokosa ustaarabu ili kulitoa taifa dogo la Comoro ambalo lilionyesha maajabu na kuonekana kuwa na uwezo wa kuwatimua wenyeji nje ya mashindano. Kwanza wachezaji na viongozi 12 wa Comoro walizuiliwa kucheza kwa vile walisemekana kuwa na maabukizi ya Uviko-19.

Kati yao ni kipa Moyadh Ousseini na Ali Ahamada, lakini wa tatu ambaye ndiye namba moja, Salim Ben Boina alikuwa majeruhi na hakuweza kucheza.

Hakuna mchezaji wa Cameroon aliyegundulika kuwa na mambukizi ya ugonjwa huo. Comoro walitaka mchezo usogezwe mbele ili wamuagize kipa mwingine kutoka nyumbani au Ufaransa, lakini walikataliwa. Kwa hivyo ilibidi watumie wachezaji wa akiba waliokuwa hawana uzoefu.

Zipo tetesi kwamba matokeo ya uchunguzi yalikuwa feki ili kuidhoofisha Comoro. Hapo tena beki wa kushoto, Chaker Alhadhur ilimbidi avae glovu na kuwa kipa - nafasi ambayo hajawahi kuicheza katika mchezo wowote wa mashindano.

Hata hivyo, alilinda lango kwa ujasiri na kuwashangaza watazamaji na wachezaji wa Cameroon. Kama mchezo huo mchafu haukutosha mwamuzi kutoka Ethiopia, Bamlak Tessema alimpa kadi nyekundu Jimmy Abdoud dakika ya 10 na kuifanya Comoro kuwa na wachezaji 10 kwa dakika 80 za mchezo.

Comoro imeaga mashindano, lakini imeacha rekodi nzuri hasa kwa kuwatoa Ghana nje ya mashindano kwa ushindi wa mabao 3-2 na kwa kuchezewa mchezo mchafu wa kuhakikisha haisongi mbele. Mashabiki wa kandanda nchini na nje wanajiuliza ilikuwaje Comoro iliyokuwa inaonekana timu dhaifu katika Bara la Afrika na kulinganishwa na wepesi wa mung’unya imeweza kuonyesha maajabu ya kuingia fainali hizi na kwa kuvitoa jasho vigogo?

Kilichoonyeshwa na Comoro ni matokeo ya mipango mizuri na kuwekeza katika kandanda tofauti na Tanzania ambayo inadorora katika soka la kimataifa na inafaa kujifunza kutoka katika nchi hii ndogo yenye watu 870,000.

Comoro ina klabu 24 za kandanda zilizosajiliwa wakati Tanzania inazo zaidi ya 1,000. Ligi Kuu ya Comoro iliyoanza 1979 inashirikisha klabu 10 tu. Uwanja mkubwa wa michezo wenye jina la Mohammed Sheikh unachukua watazamaji 2,000 wakati Uwanja wa Amani wa Zanzibar ni kwa watazamaji 15,000 kwenye viti na 3,000 wa kukaa pembezoni mwa uwanja, huku ule wa Mkapa uliopo Dar es Salaam ukichukua watu 60,000. Miaka saba iliyopita Comoro ilianzisha vyuo vidogo vya kandanda na kukusanya vijana wa chini ya miaka 15 waliofundishwa na kocha mzalendo, Amir Abou. Vijana hao na wenzao wanaocheza nje hasa Ufaransa, siku hizi wanazisambaratisha timu zilizosifika kama Morocco, Misri, Cameroon, Togo na wiki iliyopita Ghana katika Afcon. Hivi sasa Comoro ni nchi ya 132 na matokeo ya karibuni yataipandisha chati. Mpaka hivi karibuni habari za Comoro zilikuwa za migogoro ya kisasa, lakini leo inasifika kwa kuwa na kikosi kizuri cha kandanda wakati mpaka mwanzo wa karne ya 21 haikusikika hata ilipojiunga na Shirikisho la Kandanda la Africa (Caf) mwaka 2007.

Mchezo wake wa kwanza wa kimataifa ulikuwa 1979 ilipofungwa 3-0 na Madagsacar na ilianza kushiriki mashindano ya Caf na Kombe la Dunia 2007, miaka 40 tangu Tanzania kufanya hivyo. Comoro ilipocheza kilichosubiriwa sio kupata mshindi, bali kuondoka na kipigo cha mabao waliyofungwa.

Tanzania ilikuwa ikiifunga Comoro mabao matano au zaidi, lakini Wangazija wa juzi sio wa leo. Katika kuwania tiketi ya fainali za Afcon 2021 Comoro ilitoka sare bila kufungana na Togo katika mchezo wa mwisho na kuwa ya pili katika kundi kwa kukusanya pointi 10, sawa na Misri iliyoongoza na kuziwekwa pembeni Kenya iliyopata pointi nne na Togo mbili. Comoro iliilaza Togo 1-0 katika mchezo wa kwanza na kwenda suluhu ya 0-0 marudiano. Ilitoka sare bila kufungana na Misri katika mchezo wa kwanza na kufungwa 3-2 waliporudiana. Ilitoka sare ya 1-1 na Kenya kwanza na baadaye kuishinda 2-1.

Matokeo hayo yalitokana na kuchukua hatua za kuendeleza kandanda huku wachezaji wa zamani wakitoa ushauri wa nini kifanyike. Serikali ikawezekeza. Shirikisho la kandanda likaitandikia mipango na klabu zikajipanga kwa kutegemea wachezaji wa ndani ya nchi na sio kubeba mizigo kutoka nje.

Hapa kwetu tunatafuta wachezaji nje ya nchi kuimarisha timu zetu wakati Comoro wanategemea wachezaji wa nchini na vijana wao wanaochezea klabu za Ulaya, hasa Ufaransa. Tatizo la Tanzania ni kwa klabu kubwa kutegemea wachezaji wa nje na matokeo yake ni tabu kupata wawakilisi wazuri wa timu ya taifa.

Ni vizuri tukatunga sheria itayopunguza wachezaji wageni ili kuwapa nafasi chipukizi kwa vile utakuwepo uwezekano wa kuchezea klabu kubwa za hapa nchini. Kukuza kiwango cha kandanda sio kujenga viwanja vizuri na kusubiri timu ishinde kwa bahati na kuipeleka bungeni - Dodoma kupongezwa.

Tuibue vipaji shuleni, vijijini na mitaani na kuviendeleza ili kupata timu itayotupa uwakilishi mzuri. Serikali iweke bajeti ya taifa na kuwepo na motisha kwa wachezaji waliolitumikia taifa. Kama tunatoa kiinua mgongo kwa wabunge kwa utumishi uliotukuka wa miaka mitano kila kipindi cha Bunge kikimalizika kwa nini tusiwe na kifuta machozi kwa wastaafu wa timu ya taifa?

Siku hizi wageni wa heshima katika michezo ni mawaziri, wakuu wa mikoa au wilaya. Tubadilike na kutoa nafasi hizo kwa wachezaji wa zamani na sehemu ndogo ya mapato apewe mgeni wa heshima kama zawadi. Katika nchi nyingi majengo makubwa, barabara, shule, vituo vya afya na hoteli hupewa majina ya wanamichezo walioipatia heshima nchi yao, tusione tabu heshima hio kuwapa wanamichezo waliojitolea kuilinda heshima ya nchi wakati wa ujana wao.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz