Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Sinema nyingi na hofu ya Pacome, Aucho Yanga

Mastaa 6 Yanga Kuikosa Namungo Leo Sinema nyingi na hofu ya Pacome, Aucho Yanga

Tue, 19 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Niliachana na pambano la Manchester United dhidi ya Liverpool na kukimbilia uwanja wa Mkapa kutazama pambano la Azam dhidi ya Yanga. Nani alikwambia mpira wa Ulaya unapendwa kuliko Simba na Yanga. Aliyedhani hivi anajidanganya.

Kituko cha kwanza uwanjani ni pale Prince Dube alipowasili uwanjani akiwa na walinzi binafsi (bodyguards). Ilinishangaza kidogo. Mbwembwe za nchi yetu zimeanza kuwaingia hata wageni. Mambo mawili ya kujiuliza.

La kwanza. Kwanini Dube aje uwanjani? Mambo yalivyo kwa sasa yana utata kidogo. Dube hayupo katika kambi ya Azam. Ameomba kuondoka na hana mahusiano nao mazuri. Hayupo katika orodha ya wachezaji watakaoanza wala kukaa katika benchi wala kupanda basi la timu.

Kwanini aje uwanjani? Si angekaa tu nyumbani akatazama pambano hili akiwa katika makochi? Lakini hapo hapo akaamua kuja uwanjani na Mabaunsa. Amewakodi mwenyewe? Nani alimkodia? Kwa lengo gani? kama yeye mwenyewe au kuna timu imemkodia kulikuwa na hofu kwamba anaweza kutekwa au kupigwa? Kwa ubaya gani?

Nadhani ujio wake uwanjani zilikuwa mbwembwe tu. Amekaa miaka minne Tanzania na nadhani anazifurahia mbwembwe za akina Diamond Platnumz na Harmonize. Anafurahia tu drama zetu. Nadhani haya ndio mambo aliyokuwa anayahitaji katika kuja timu za Kariakoo. Ile timu ya Chamazi haina mbwembwe sana.

Halafu mpira ukaanza. Yanga wakapata bao la kuongoza mapema tu. ilionekana kama vile ingeweza kuwa siku nyingine nzuri kwa Yanga. Mfungaji? Clement Mzize. Bado naungana na wanaoshangaa kwanini Mzize hakwenda Afcon. Hata kama sio kwa kucheza basi angeweza kujifunza baadhi ya vitu akiwa Ivory Coast.

Na dakika chache baada ya pambano kumalizika alikuwa ndani ya ndege akielekea katika nchi ya Azerbaijan ambapo Taifa Stars imealikwa kucheza mechi za FIFA.

Baada ya muda Azam wakasawazisha. Uzembe wa safu ya ulinzi ya Yanga. Sidhani kama watacheza hivyo wakicheza dhidi ya Mamelodi Sundowns. Vinginevyo si wanaweza kufungwa mabao 12-1. Sidhani kama itakuwa hivyo.

Fei Toto akafunga bao la pili. Hadithi tamu ilikuwa imeandikwa. Namna ambavyo Fei aliondoka Yanga. Namna ambavyo alichukiwa na anachukiwa. Ghafla ni yeye ndiye ambaye aliwafungia Azam bao la ushindi. Ni kama filamu fulani tamu ya mapenzi yenye kisasi ndani yake.

Fei akaomba msamaha kwa Wanayanga kwa kufunga bao hilo. Mambo ya Ulaya haya. Kwanini aliomba msamaha wakati kuna chuki inatawala baina yao? Kwamba anawashukuru kwa kumleta Tanzania Bara na kumlea licha ya ukweli kwamba alisaini Singida United na hakuwahi kugusa jezi yao?

Sijui kama baada ya msamaha huo aliouomba Yanga watakuwa wamemsamehe. Labda kinachoweza kutokea ni kwa baadhi ya Wanayanga kupunguza hasira dhidi yao. Niliwasikia jukwaani wakisema ‘Mtoto wetu huyu basi tu.’

Kilichofuatia ni sinema nyingi baada ya Azam kuongoza bao la pili. wachezaji wake wakaanza kukaa ardhini kwa muda mrefu baada ya kukimbia uwanjani. Yanga imekuwa tishio hivi? Ningeweza kuafiki wakati Kagera Sugar walipoanza kukaa zaidi ardhini wakati pambano lao la Yanga likielekea sare pale Kaitaba. Lakini Azam? hapana.

Azam ni timu ya tatu kwa ukubwa baada ya Simba na Yanga. Sio timu ya tatu kwa jina tu, bali hata kwa matumizi ya pesa. Kwa namna kikosi chao kilivyo nadhani mbinu pekee kwao ya kupoteza muda ilikuwa ni kukaa na mpira kwa muda mrefu.

Azam ni kama Manchester City. Inacheza na Manchester United au Liverpool. Haiwezi kuongoza mabao mawili halafu wachezaji wakakaa ardhini kwa muda mrefu kwa sababu ya kupoteza muda. Hakuna haja. Miaka yote hii Azam wamekuwa wakipimana ubavu na Simba na Yanga. Wanashinda, wanatoka sare, wanafungwa lakini hawalali ardhini bila ya sababu.

Azam ya akina Kipre Tchetche ingeweza kusaka bao la tatu. Hata Azam ya majuzi ya akina Dube ingeweza kusaka bao la tatu. Walikuwa wanapoteza muda wakati Pacome Zouzoua na Yao Kouassi wapo nje. Walikuwa wanapoteza muda katika siku ambayo Khalid Aucho hakuwepo na pacha wake, Mudathir Yahaya alikuwa anacheza kama mchezaji wa veteran. Walinishangaza kidogo.

Kama Azam haiwezi kuipa Yanga mechi ngumu na kichapo kikali, nani mwingine awape? Azam wangeamua kupiga mechi ngumu zaidi nadhani Yanga angeweza kufungwa zaidi. Hata mwamuzi alipoongeza dakika saba ilikuwa ni huruma tu dhidi ya Azam. Angeweza kuongeza hata dakika kumi kwa utoto ambao Azam walikuwa wanaufanya.

Baadaye mechi ikaisha. Ikatokea sinema nyingine ya kusisimua. Yanga walikubali matokeo hapo hapo. wakaanza kuwapigia makofi wachezaji wao. Wachezaji nao pia wakajibu. Nadhani ni kwa sababu mashabiki walikuwa wanajikumbusha bado kuna pengo kubwa kati ya Yanga na wengineo pindi unapotazama msimamo wa Ligi. Hawakuwa na presha.

Lakini ukweli ni kwamba timu yao imewapa furaha katika vipindi virefu kuliko huzuni. Leo Yanga ni wakuwapigia makofi wachezaji wao licha ya kufungwa? Ni kitu kinachotokea mara chache katika maisha yao ya soka. Nje ya uwanja hakukuwa na mafungu mengi wala malalamiko mengi. Walitawanyika wakarudi nyumbani.

Nadhani kitu pekee ambacho watakuwa na hofu nacho zaidi sio matokeo. Bali ni namna ambavyo Yao pamoja na Pacome waliondoka uwanjani wakiwa wamebebwa katika mabega ya watu. Wataiwahi mechi ya Mamelodi kweli?

Hayo yote yanaendelea huku wakiwa na wasiwasi kama dokta wa mpira, Aucho atakuwepo uwanjani pambano dhidi ya Mamelodi. Kwa namna ambavyo kiungo chao kilikuwa hakijatulia juzi, kuna kila haja ya kuwa na wasiwasi kama Aucho akikosekana pambano la Mamelodi.

Columnist: Mwanaspoti