Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simu za mkononi na mabadiliko ya jamii

7969cd04a1b5c129fd3dd6d492078892 Simu za mkononi na mabadiliko ya jamii

Thu, 17 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MIAKA ya hivi karibuni jamii imeshuhudia maendeleo makubwa ya sekta ya mawasiliano duniani. Hata hapa Tanzania, idadi kubwa ya Watanzania mijini na vijijini imefikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu na mtandao wa intaneti. Huduma ya mtandao imekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba, idadi ya laini za simu za mkononi hadi Septemba 2020 zilizosajiliwa zilikuwa ni 49,215,857 ambazo zinamilikiwa na takribani watumiaji milioni 27.3.

Tanzania inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 56, hivyo idadi hiyo ya Watanzania wana uwezo wa kuongeza kipato binafsi na taifa kutokana na matumizi ya simu kutokana na idadi ya laini hizo zilizosajiliwa. Hii pia inamaanisha mawasiliano miongoni mwa wananchi yamekuwa makubwa zaidi.

Simu za mkononi zilianza zikiwa kubwa sana sawa na kompyuta. Inaelezwa kwamba wakati zinaanza ungeweza kuzitumia iwapo una nguvu za kuibeba au ikiwa imeunganishwa na mfumo wa gari lako kwani betri zake zilikuwa nzito. Simu hizo zilikuwa kubwa kuliko boksi la viatu na ziligharimu maelfu ya dola.

Hivi sasa kuna simu za mkononi takribani bilioni 1.35 duniani kote ambazo zinaweza kutosha kwenye kiganja cha mkono au zaidi na za kisasa zilizobadilisha dunia kuwa ofisi moja yenye vitengo mbalimbali ingawa simu hizo zimesababisha baadhi ya watu kukosa kazi au marupurupu.

Baadhi ya nchi, zaidi ya nusu ya wakazi wake wanamiliki simu lakini kwa upande wa Afrika takwimu zilizopo zinaonesha kwamba watumiaji wengi wa simu ni wakazi wa mijini.

Jarida la The Bulletin la Australia linaripoti kwamba idadi ya simu za mkononi zinazotumiwa zinakaribia idadi ya televisheni na kompyuta.

Katika nchi zaidi ya 20 idadi ya simu za mkononi (pia hujulikana kama simu za kiganjani) inapita idadi ya simuwaya. Licha ya hatua kubwa ya teknolojia iliyofikiwa, simu zimebadili sana maisha ya jamii.

Umuhimu wa simu za kiganjani umejidhihirisha pia wakati dunia inapokabiliana na ugonjwa wa corona. Pia zimekuwa na umuhimu na mchango mkubwa katika chaguzi mbalimbali za viongozi duniani. Hii ni mbali ya shughuli za kijamii, biashara, elimu nk.

Pamoja na manufaa mengi, simu za mkononi pia zinatumika vibaya kwa uhalifu na kuratibu masuala ambayo ni kinyume na sheria za nchi na maadili ya jamii.

Masomo

Simu za mkononi zilizoboreshwa kwa maana ya sumumtelezo (wengine wanaita simujanja) ni sawa na kompyuta kwa sasa. Iwapo mzazi atamwelimisha mtoto wake matumizi mazuri ya simu za mkononi itamrahisishia uelewa wa masomo na masuala mbalimbali.

Katika dunia ya sasa kuna vitu ambavyo haviepukiki katika nchi, familia na jamii, simu hurahisisha masomo na kuyafafanua zaidi iwapo mzazi atachambua kiufasaha masomo mbalimbali yanayopatikana katika mitandao.

Katika muktadha huo, serikali inashauriwa kutumia wataalamu wa elimu na vipindi husika kufuatilia ufasaha wa masomo kupitia mtandaoni kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu. Kiwango cha ufaulu na fursa mbalimbali za ajira kitapanda kupitia simu za mkononi.

Baadhi ya watu wamekuwa wakifikiria kutafutwa kwa programu ambazo zitamfanya mwanafunzi akiishaingia katika eneo la shule, simu isiwe na uwezo wa kufungua mambo yasiyohusu masomo kutokana na uwezo wake wa kutumika kama kompyuta huku wazazi wengi wakiwa na uwezo wa kununua simu kulinganisha na kompyuta.

Mwalimu wa shule moja ya serikali jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema yeye kama mwalimu, simu inamrahisishia sana ufundishaji wa masomo na maandalizi.

Hata hivyo, anasema hakubaliani na pendekezo lolote la kuruhusu matumizi ya simu kwa wanafunzi. Kwa nini? Anajibu kwamba walishafanya msako wa ghafla shuleni kwao na kuibua mambo mazito katika simu walizokutwa nazo wanafunzi.

“Labda kama serikali itaweka utaratibu maalamu wa kuchuja programu zisizofaa. Hata hivyo, inaweza kutokea watoto watundu wakazifungua,” anaonya.

Mwalimu Daudi Makoba ambaye masomo yake yanayopatikana bila malipo mtandaoni yamenufaisha wengi, anasema kuwanyima wanafunzi matumizi ya simu ni kuwakosesha maarifa zaidi.

“Mimi najitahidi kuwapatia masomo ya ziada baada ya masomo ya darasani kutokana na ukosefu wa vitabu vya kiada na ziada. Tatizo ni kwamba watoto wengi hawaruhusiwi kutumia simu hata wakiwa majumbani mwao na hivyo inakuwa ngumu kuyapata haya masomo,” anasema.

Makoba anasema matumizi ya simu yakiruhusiwa shuleni yatamsaidia mwanafunzi hasa wa shule za vijijini kuelimika kwani masomo yatakuwa kwenye viganja vyao.

Anaishauri serikali iongeze bajeti katika elimu ili kuboresha na kujenga maktaba zinazojitosheleza sambamba na elimu ya matumizi bora ya mitandao kwa kushirikisha vyombo vya habari.

Anasema kuna baadhi ya shule ambazo zinawanyima wanafunzi vitabu kwa kuhofia vitabu hivyo kuchanika au kupotea.

“Suluhisho ni kuwafundisha wanafunzi utunzaji wa vitabu na hilo litawezekana iwapo wazazi watatambua wajibu wao kielimu na kutunza vitabu kwa faida ya watoto na kizazi kingine,” anasema Mwalimu Makoba.

Biashara

Biashara kwa njia ya mtandao ipo wazi kwa sekta zote kuanzia sekta rasmi na isiyo rasmi (machinga). Mitandao inaweza kuwarahisisha watu kufanya biashara zao na kubuni njia mpya za kuuza.

Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba Marekani, India, China, Uingereza, Finland na zinginezo zinazalisha wafanyabiasara wakubwa kila siku wanaotajirika kupitia viwanda na biashara za simu.

Shirika moja kubwa duniani liliwahi kusema: “Simu ya mkononi ndicho kifaa cha kielektroniki kinachouzwa kwa wingi zaidi.”

Lugha mpya

Mawasiliano ya simu za mkononi si kwa ajili ya kuzungumza pekee bali pia kuandikiana ujumbe.

Watumiaji simu za mkononi hasa vijana hutuma ujumbe mfupi ambao huibua lugha mbalimbali zisizo za kawaida katika matumizi rasmi.

Kwa kuwa mawasiliano hayo huhusisha kuandika ujumbe kwa kutumia vibonyezo vidogo vya simu, wale wanaofanya hivyo hufupisha maneno kwa kuchanganya herufi na nambari ili kupeleka ujumbe waliokusudia.

Simu na mahusiano

Simu zinatajwa sana katika kusaidia kuboresha au kuharibu mahusiano.

Kuna ndoa zimevunjika kutokana na simu huku wanaume wakituhumiwa zaidi kwani kuna msemo kwamba “simu ya mume ni sawa na limao, mke akiikimbilia atajikuta anatoka machozi”.

Uchunguzi mmoja uliofanywa nchini Uingereza ulionesha kwamba asilimia 42 ya vijana kati ya umri wa miaka 18 na 24 hutuma ujumbe mfupi kwa simu ukihusu mapenzi, asilimia 20 hutuma ujumbe ili kupanga kukutana na watu wa jinsia tofauti na asilimia 13 wametuma ujumbe ili kuvunja uhusiano.

Baadhi ya watu wanaochunguza hali za kijamii wana hofu kwamba njia ya kuandika maneno na lugha inayotumiwa katika ujumbe mfupi inaathiri uwezo wa lugha wa vijana.

Wengine hawakubaliani na maoni hayo kwani wanasema kwamba njia hiyo ya kuwasiliana “imechochea mapenzi ya kuandika katika kizazi kipya.”

Msemaji wa shirika ambalo hutayarisha kamusi nchini Australia aliliambia gazeti Sun-Herald hivi: “Si kawaida kupata nafasi ya kubuni lugha mpya... ujumbe wa simu na intaneti huwafanya vijana waandike sana. Inawabidi wawe wenye ufasaha ili watambue na kujifunza maneno yanayotumiwa sana.”

Kifungo cha simu, uhatari

Ingawa simu ya mkononi ni kifaa chenye faida katika mawasiliano ya kirafiki na ya kibiashara, kifaa hicho huwafanya wafanyakazi wengi wahisi kwamba wamefungiwa ofisini.

Uchunguzi mmoja ulionesha kwamba asilimia 80 ya watu wanaofanya matangazo ya biashara na asilimia 60 ya wajenzi huwalazimu wawe na simu za mkononi kila wakati ili wapokee simu kutoka kwa waajiri au wateja wao.

Simu za mkononi zinaweza pia kuhatarisha umma. Uchunguzi uliofanywa huko Canada ulionesha kwamba kutumia simu ya mkononi unapoendesha gari ni hatari sana kama vile kuendesha gari ukiwa umezidisha kileo.

Profesa Mark Stevenson, wa Kituo cha Utafiti wa Majeraha katika Chuo Kikuu cha Western Australia, anasema kwamba ni vigumu kuzungumza na mtu kwa simu unapoendesha gari kuliko kuzungumza na mtu aliye ndani ya gari hilo.

Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni ulionesha kwamba dereva mmoja kati ya watano nchini Australia alituma ujumbe mfupi wa simu huku akiendesha na theluthi moja walipiga au kupokea simu wakiendesha magari. Yote hayo yanatajwa kuwa ni hatari.

Usafiri wa ndege pia unaathiriwa na matumizi mabaya ya simu za mkononi. Ijapokuwa nyaya za ndege za kisasa zimekingwa zisiathiriwe na mawimbi ya redio ya simu za mkononi, ndege za zamani zinaweza kuathiriwa.

Gazeti New Scientist linaripoti: “Majaribio yaliyofanywa katika ndege mbili na Shirika la Usafiri wa Ndege la Uingereza yamethibitisha kwamba mawimbi ya simu za mkononi huathiri mitambo muhimu ya ndege.”

Msemaji wa shirika hilo alionesha hatari moja kubwa inayosababishwa na simu za mkononi akisema: “Simu hizi hutoa nguvu nyingi zaidi kadiri inavyokuwa mbali na kituo cha kurusha na kupokea mawimbi. Hivyo, kadiri ndege inavyozidi kupaa ndivyo mawimbi ya simu yanavyozidi kuwa na nguvu na hilo huathiri zaidi mitambo ya ndege wakati ambao ni muhimu sana.”

Columnist: habarileo.co.tz