Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba walivyomwogopa Manji

Manji.jfif Yusuf Manji

Sun, 14 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga imepita katika nyakati nyingi. Imepita katika nyakati ngumu na za neema. Imepita safari ndefu kufika hapo ilipo leo.

Nani anamkumbuka Marehemu Abbas Gulamali. Huyu anatajwa kuwa miongoni mwa matajiri ambao walibadilisha sana soka la Tanzania. Aliifanya Yanga kuwa tishio katika nyakati zake.

Hata hivyo, leo sitamzungumzia sana Gulamali. Nataka nizungumze kidogo kuhusu aliyewahi kuwa Mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji. Kichaa wa soka. Tajiri aliyebadilisha kila kitu kwenye mpira wa kisasa nchini.

Kabla Manji hajaingia Yanga, Simba ilikuwa na jeuri kubwa ya Kundi la Friends of Simba. Hawa ni baadhi ya matajiri ambao walijiunga ili kuishika mkono Simba kila ilipopita katika nyakati ngumu.

Walisaidia usajili wa wachezaji wa maana. Wakasaidia kambi ya timu na gharama nyingine nyingi. Kuna nyakati walikuwa wakiikopesha Simba na kurejeshewa fedha pindi zikipatikana.

Hawa ndio waliifanya Simba kuwa tisho mwanzoni mwa miaka ya 2000. Ndiyo kipindi waliwasajili kina Boniface Pawasa, Selemani Matola, Steven Mapunda, Juma Kaseja na wengineo. Simba ikawa na nguvu.

Ni katika nyakati hizo ambapo Yanga ilikuwa inajitafuta. Ilizidiwa kila kitu na watani zao hao. Nini kilitokea? Ni stori ya kusisimua. Kama hujui ni kipindi hicho ilifikia hatua Yanga ilicheza kwa misimu minane bila kupata ushindi mbele ya watani katika Kariakoo Derby ya Ligi Kuu, yaani kuanzia 2000-2008. Rudia tenani tangu Idd Moshi alipofunga mabao mawili akitokea fungate Agosti 5, 2000 hadi Oktoba 26, 2008 pale Mkenya Ben Mwalala alipoakata mzizi wa fitina kwa kufunga bao pekee.

Kumbukumbu zinaonyesha mwaka 2006 Manji alibadili kila kitu alipojitokeza na kuwa mfadhili wa Yanga. Timu ikaanza kuishi kwa fedha zake. Akaifanya Yanga kuwa timu jeuri zaidi nchini.

Manji alitoa fedha za usajili wa maana kwa Yanga. Aliajiri makocha wenye wasifu mkubwa. Ndio nyakati hizo tuliona kocha kama Micho akitua Yanga. Manji aligharamia kambi na vitu vingine vingi.

Kwa kifupi aliibeba Yanga katika mabega yake.

Nani angewaza katika nyakati zile Juma Kaseja angeweza kuhama Simba na kwenda Yanga? Hakuna. Ila Manji alikifanya kionekane ni kitu chepesi.

Kiongozi mmoja wa Simba aliwahi kuniambia kuwa Kaseja alipokwenda kuwaeleza ofa ambayo amepewa na Manji walistaajabu sana. Ilikuwa ni fedha nyingi mno. Anakiri kuwa Simba isingeweza kumpatia hata nusu yake. Wakamruhusu aende Yanga.

Ndiyo Manji. Hakuwa na mkono mfupi lilipokuja suala la Yanga. Angeweza kufanya chochote anachojisikia. Kuna wakati alinunua tiketi zote ili mashabiki wa Yanga waingie uwanjani bure. Hakujali kitu.

Ilikuwa ni vigumu sana kushindana na Yanga ya Manji. Ndiyo maana katika miaka yake 10 kama Mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga walitwaa ubingwa mara saba. Simba ingefanya nini? Hakuna.

Manji ndiye mtu ambaye amefanya wachezaji wazawa kufurahia maisha yao ya soka.

Kumbuka namna alimsajili Kelvin Yondani kutoka Simba. Namna alivyowapora Simba, Mrisho Ngassa mwaka 2013. Aliifanya Yanga iishi katika dunia yake.

Ukizungumza na wachezaji waliocheza Yanga wakati wa Manji watakwambia namna maisha yao yalibadilika. Wengi walifanya vitu vya maana wakati huo. Kila mchezaji mzuri alitamani kucheza Yanga.

Nguvu ya Manji ndio imeleta mabadiliko haya tunayoona sasa. Ndio sababu Mohamed Dewji aliamua kuingia Simba. Alihitajika tajiri wa kushindana na Manji kwa kuwa Friends of Simba walimshindwa. Ndio akaja Mo Dewji.

Bahati mbaya kwa Yanga ni kwamba wakati Mo Dewji anaingia Simba, Manji naye alikuwa anaondoka Yanga. Ushindani ukapungua. Yanga ikaishi katika nyakati ngumu sana. Ikaanza kuchangisha fedha kwenye ndoo. Maisha yalikuwa magumu sana.

Simba ikawa imara chini ya Dewji. Yanga ikaona umuhimu wa kuwa na mwekezaji. Iliona pengo la Manji. Ikafahamu namna mpira wa kisasa unaendeshwa sasa.

Ndiyo sababu GSM ilipohitaji kuwekeza kwenye timu yao viongozi wa Yanga hawakufikiria mara mbili. Walishaona ukweli kuwa soka linahitaji fedha. Wakati Manji anatoa fedha walikuwa wakiona kama anajipendekeza tu, lakini ukweli ni kwamba ilihitaji moyo kuwa kama Manji. Ili kuweza kushindana ndani na nje ya nchi lazima uwe na fedha za kutosha. Inatajika fedha za usajili wa wachezaji mahiri. Fedha za kuweka kambi za maana. Kumudu gharama za kusafiri kwenda kucheza sehemu mbalimbali Afrika. Ni fedha nyingi.

Kucheza mechi mbili za CAF ukiwa nyumbani na ugenini inahitaji karibu Sh300 milioni. Ni fedha ndefu sana. Ndiyo sababu timu nyingine huwa zinashindwa kumudu.

Wakati huu nikikumbushia stori ya Manji, ni vyema tukakumbushana kuheshimu kinachofanywa na hawa kina Dewji na GSM. Wamebadilisha sana soka letu. Wameifanya nchi iwe na heshima Afrika.

Unadhani Yanga ingefika fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka jana bila nguvu ya GSM. Hakuna. Wasingeweza gharama. Kuna sehemu wangeshindwa kuonyesha ushindani wa kweli kutokana na ugumu wa maisha. Unadhani Simba ingefika robo fainali CAF mara kwa mara bila nguvu ya Dewji?  Soka la kisasa linahitaji fedha na ndiyo kitu ambacho Dewji anafanya Simba. Ameifanya kuwa na ushindani sokoni na uwanjani.

Columnist: www.tanzaniaweb.live