Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba vs Yanga na vifo vya ghafla

Kibu Goal Simba vs Yanga na vifo vya ghafla

Fri, 21 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Gumzo kubwa lililotawala wiki hii ni kichapo cha mabao 2-0 walichopokea Yanga dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa katika Uwanja wa Mkapa, Jumapili Aprili 16.

Katika mechi hiyo ya watani jadi ni kawaida kubeba hisia za maelfu ya mashabiki ndani na nje ya nchi ikiwamo wale wanaotazama mechi hiyo moja kwa moja au wale wanaofuatilia kwa njia ya redio na runinga.

Ndio maana ni kawaida kuona watoa huduma za kwanza wakitoa msaada kwa watu waliopoteza fahamu ghafla pale uwanjani wakati mchezo ukiendelea.

Burudani ya soka hubeba hisia za juu za mashabiki kiasi cha kwamba huwa ni kawaida wengine kuumia kihisia au kujikuta wakipoteza fahamu kutokana na mshtuko wa furaha au karaha.

Tukio la kusikitisha ni lile la Wilayani Chalinze mkoani Pwani la kufariki ghafla kwa shabiki aitwaye Jane toka kata ya Bwilingu wakati akitazama mechi hiyo katika Luninga ikiwa katika nusu ya kwanza ya mchezo.

Shabiki huyo alianza kujisikia vibaya ghafla alionekana kujishika eneo la kifuani na sekunde chache alianguka huku akikoroma na kupoteza fahamu.

Baadaye alichukuliwa na kupelekwa katika huduma za afya ambapo alibainika kuwa tayari alikuwa ameishafariki.

Kifo hicho kimeleta maswali mengi mitandaoni na mtaani ambao wengi wao hawafahamu masuala ya afya kiundani hata kudhani huenda ni imani za kishirikina.

Huwa ni kawaida kwa jamii kujiuliza pale yanapotokea matukio kama haya na wengi hupata na hofu.

Tukio kama hili limewahi kutokea Septemba 2021 wilayani Mpwapwa kwa shabiki kupata mstuko na kufariki wakati akitazama mechi ya ngao ya hisani kati ya Simba na Yanga.

Kitabibu ni kweli hisia kali za ushabiki zinaweza kusababisha kifo cha ghafla ingawa si kwa moja kwa moja.

Mabadiliko ya kimwili ya hisia huambatana na utirishaji wa vichochezi vinavyoongeza kasi ya mapigo ya moyo ambayo yanaweza kuleta athari katika moyo.

Kwa kawaida mwanadamu anapopenda jambo fulani na kumganda mwilini mwake ikiwamo kumkaa akili mwake. Hali kama hii inaweza kumletea kuumia kihisia ikiwamo hisia chanya au hasi.

Mwanadamu anapotazama kitu anachokipenda macho huona kisha picha hiyo huenda kutafsiriwa katika ubongo na hatimaye huweza kujibu mapigo ikiwamo kufurahi sana au kukasika sana.

Mambo haya yanaweza kusababisha mwili kitiririsha vichochezi ambavyo huweza kuusababishia mwili kupata mshtuko ambao unaweza kusababisha moyo kusimama.

Pale hatua za huduma ya kwanza zinapochelewa kumfikia basi kifo kinaweza kutokea.

Jicho la kitabibu litalitazama tukio hili ili kuwapa ufahamu tatizo hili la vifo vya ghafla ambalo shambulizi la moyo ni moja ya sababu zinazochangia watu kupata tatizo hili.

Sababu za vifo vya ghafla

Shambulizi la moyo kitabibu Heart Attack ni moja ya matatizo ya kiafya yasiyoambukiza yanayosababisha mara kwa mara vifo vya ghafla kwa watu wazima wa miaka 45 kuendelea.

Ni kawaida ikatokea sababu ya kifo cha ghafla isijulikane moja kwa moja, lakini yapo matatizo ya kiafya yanayohusishwa na kifo cha ghafla ikiwamo vinavyotokea tukiwa usingizini.

Ukiacha matatizo ya moyo kwa ujumla, katika sehemu nyingine za mwili yaani ubongo na figo vinaweza kupata matatizo ya kiafya na kusababisha kifo cha ghafla.

Moyo ndiyo ogani kubwa inayohusika na usukumaji wa damu mwilini, magonjwa au matatizo yake huwa ni ya kimya kimya na ndiyo yanayoongoza kusababisha vifo vya ghafla duniani.

Maradhi ya moyo huwa yanapiga hatua kimya kimya pasipo kujijua kwa anayeugua, mara nyingi watu hugundulika wakiwa na matatizo ya moyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa jumla.

Mara nyingi kuharibika kwa mishipa ya damu katika moyo ni sababu kubwa inayosababisha matatizo mbalimbali ikiwamo mapigo ya moyo kwenda mrama, misuli ya moyo kufa na shambulizi la moyo.

Mishipa ya damu ya moyo ya Ateri ikiharibika husababisha misuli ya moyo kukosa damu kabisa au kupata kiasi kidogo sana. Uharibifu hutokana na mgando wa tando ya mafuta katika kuta za mishipa hii.

Hali hii husabisha misuli kushindwa kufanya kazi yakusukuma damu kwa ufanisi wakawaida, hupiga mapigo bila mpangilio na siku yoyote isiyojulikana ghafla moyo husimama.

Misuli ya moyo kututumka pia ni sababu mojawapo kwani husababisha vyumba vya moyo kuwa na nafasi ndogo yakupokea damu na pia kushindwa kusukuma vizuri damu.

Sababu nyingine ni pamoja na moyo kushindwa kufanya kazi, maumbile yasiyo yakawaida ya mishipa ya damu, hitilafu au uambukizi wa valve za moyo na kuzaliwa na moyo wenye hitilafu.

Vile vile uwepo wa matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, upungufu wa madini kama vile magnesium, kuzaliwa na moyo mkubwa, wingi wa mafuta mabaya mwilini na kuwa na hitilafu ya mapigo ya moyo.

Mambo mengine ambayo hayatokani na maradhi ya moyo ni kama vile sumu, mrundikano wa taka sumu, matatizo ya mfumo wa hewa, Kwame wa kitu njia ya hewa, kuvuta hewa chafu na ajali katika ogani.

Walio katika hatari ni wenye shinikizo la juu la damu, kiwango kikubwa cha lehemu, unene, kisukari, uvutaji tumbaku na kutofanya mazoezi, umri mkubwa 45+ na historia ya familia kupatwa na tatizo hili.

Watu wa karibu wa shabiki aliyefariki Chalinze walisema kuwa marehemu Jane aliwahi kugundulika kuwa na tatizo la moyo. Hivyo alikuwa katika hatari ya kupata tatizo hilo.

Inawezekana mtu ukawa na matatizo ya afya ya moyo lakini isijijue, ila pale inapotokea mstuko wowote ule ndipo unaweza kusababisha madhara.

Chukua hii

Hakikisha unafika mapema katika huduma za afya pale unapoona Dalili na viashiria vya matatizo ya kiafya ya moyo.

Dalili ni maumivu ya ghafla ya kifua, mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, kuchoka kirahisi, uchovu, pumzi kukatika, kuona giza, kuishiwa nguvu, kupoteza fahamu, kichefuchefu, kutokwa jasho na kukosa usingizi.

Jengautamaduni wa kuchunguza afya ya mwili mzima angalau kwa mwaka mara moja na pia kushikamana na njia zote za kujikinga

Matukio ya vifo vya ghafla si mzigo kwa afya ya jamii na yanatokea mara chache ukilinganisha na matatizo mengine ya afya kama malaria, Ukimwi na kifua kkikuu.

Elimu ya huduma ya kwanza iendelee kutolewa tangu shule ya awali ili kuwajengea uwezo katika utoaji wa huduma ya kwanza kwa mtu aliyepatwa na mstuko au shambulizi la moyo.

Columnist: Mwanaspoti