Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba v Raja CA Ilikuwa vita ya uwezo na ufundi zaidi

FpQ3Dt4XsAIe58x Simba v Raja CA Ilikuwa vita ya uwezo na ufundi zaidi

Mon, 20 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

'Hakuna kusema mwisho hadi iwe mwisho.' Hiyo ndiyo kauli ambayo wachezaji wa Simba wanatakiwa kutembea nayo licha ya kukubali kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Raja Casablanca kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, juzi Jumamosi.

Simba iko kundi C kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na katika mechi mbili ilizocheza kwenye hatua hiyo ya makundi, wameruhusu mabao manne na hii inaonyesha kwenye safu yao ya ulinzi kuna tatizo na inatakiwa walisuke upya.

Kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Horoya ya Guinea, ilichapwa bao 1-0 kabla ya kuadhibiwa mabao 3-0 na Raja Kwa Mkapa.

Mwanaspoti limeuchambua mchezo huo wa juzi Jumamosi na mambo yalikuwa hivi kwa dakika zote 90.

BAO LA KUONGOZA KWA RAJA

Simba iliingia kwenye mchezo huo ikiwasoma wapinzani wao, tofauti na Raja waliokuwa walikuwa na mpango wa kufunga bao la mapema ili kutuliza presha yao.

Raja ilifanikiwa kwenye hilo na mashambulizi kadhaa ya kushtukiza na silaha yao kubwa ilikuwa ni pasi fupi fupi zilizowapa tabu mabeki wa kati wa Simba, Joash Onyango na Henock Inonga.

Faida ya mashambulizi hayo ilionekana dakika ya 30 na Raja ilipata bao la kwanza lililofungwa na Hamza Khabba aliyepokea pasi ya haraka na kupiga shuti kwenye kona ya juu ya lango na kumshinda kipa Aishi Manula aliyekosa la kufanya akiutazama mpira ukijaa nyavuni.

Bao hilo lilionekana kuiamsha Simba, lakini Raja nao wakizidisha mashambulizi ya kushtukiza na kupata matokeo.

KIUNGO KILIKUFA MAPEMA

Kwenye eneo la kiungo ukabaji Simba walianza Sawadogo na Mzamiru Yassin huku upande wa Raja wao walianza Zakaria Habti, Mohamed AL Makahasi na Yousri Bouzok ambao walikuwa wepesi mno.

Simba wao Mzamiru alikuwa mwepesi kwenye kukaba na kuachia mpira mapema kwenda eneo la ushambuliaji, huku Sawadogo akianza vizuri kucheza mipira ya juu na kukaba kwa chini lakini hakuwa mwepesi kuachia mipira.

Jambo hilo liliwafanya benchi la ufundi kumtoa dakika 45 za kipindi cha pili na kuingia Jonas Mkude ambaye alianza kwa kucheza pasi fupi na ndefu zilizoonyesha wazi sababu ya yeye kuingia.

Mkude aliituliza timu akicheza sambamba na Mzamiru huku wakiachia mipira kwa wepesi lakini bado ilikuwa ni changamoto kupenya safu ya Raja na hata walipofanikiwa umakini wa kuweka wavuni mpira ulikuwa mdogo.

BOCCO AWEKWA MFUKONI

Simba iliingia na mfumo wa 4-2-3-1 na eneo la ushambuliaji ilimsimamisha John Bocco mwenye kimo kirefu ili kukabiliana vizuri na mabeki wa Raja Casablanca. Bocco alikuwa mtulivu lakini alipocheza mipira ya juu, Saidi Ntibazonkiza, Clatous Chama na Ousmane Sakho walichelewa kuipata.

Mabeki wa kati wa Raja, Jamal Harkass (1995) na Abdessamad Badaoui (1999) walikuwa wepesi kuiwahi mipira hiyo na hata kukabiliana na washambuliaji wa Simba.

Upande wa Sakho alilazimika kutolewa na kuingia Moses Phiri, huku Jean Baleke akichukua nafasi ya Bocco. Hata hivyo, bado kulikuwa na wakati mgumu na hivyo kujikuta wakipiga mashuti mengi ya nje ya lango.

UMRI, SPIDI ZAIBEBA RAJA

Simba ilitawala mchezo kwa kiasi kikubwa na kupata wastani wa 62% katika kumiliki mpira, huku Raja ikipata 38%. Hata hivyo, Raja ilionekana kuwa na kasi na hilo lilibebwa na umri wa wachezaji wake.

Katika kikosi cha kwanza kilichoanza mchezo huo, mchezaji mwenye umri mkubwa ni kipa Anas Zniti aliyezaliwa 1988 na mshambuliaji Roger Aholou aliyezaliwa 1993, huku waliobaki ni wa kuanzia mwaka 1995.

Upande wa Simba ni tofauti kwani kwa walioanza mkubwa ni Ntibazonkiza aliyezaliwa 1987 na Bocco 1989, Chama 1991 na hawa wote ni washambuliaji ambao wanaenda kukabiliana na vijana.

Ilikuwa ni rahisi kukabwa kwa sababu mikimbio ni miwili tofauti na hata eneo la ulinzi kwa Simba pale kati Onyango ndio mkubwa akiwa amezaliwa 1993 akikabiliana na Hamza Khabba aliyezaliwa 1996.

SIMBA ILIJIAMINI, RAJA IKAWAPA SOMO

'Kwa Mkapa hatoki mtu' ni msemo ambao umekuwa ukiwapa Simba jeuri na kujiamini. Ni kweli mechi kadhaa za kimataifa Simba imecheza kwenye uwanja huo na kupata matokeo tofauti na mchezo wa juzi.

Simba iliamini katika hilo na hata dakika 45 za kipindi cha kwanza walionyesha hilo. Maisha yanabadilika. Wachezaji waache kukariri.

Ukubwa wa Raja umedhihirisha ni namna gani walivyowekeza na juzi ndio wao walioamua mechi.

Simba inatakiwa kujipanga kweli inapokutana na timu kubwa kama Raja kwani mbali na hamasa waliyoipata na kujiamini Kwa Mkapa hatoki mtu, ila mziki wa juzi utakuwa umewapa somo.

BEKI ILIZINGUA

Kocha wa Raja ni kama alijua wazi Simba inatumia zaidi mabeki wake kwenye kupeleka mashambulizi kwani waliweza kumtuliza nahodha msaidizi, Mohamed Hussein 'Tshabalala' asipeleke mashambulizi.

Tshabalala huwa ni mzuri kwenye kuipandisha timu lakini katika mchezo wa juzi, alishindwa kufanya hivyo na upande wake waliutumia Raja kupandisha mashambulizi langoni mwa Simba.

Hata hivyo, beki huyo alikuwa akipanda kwa kushtukiza na mwepesi kurudi na kuzuia.

Kwa upande wa kulia, Kapombe hakuwa mwepesi kurudi baada ya kupandisha mashambulizi na Raja walitumia mapungufu hayo kuhamia upande huo na kupeleka mashambulizi, huku Onyango akiwa na kazi kubwa ya kuziba pengo hilo.

MSIKIE ROBERTINHO

Kocha mkuu wa Simba, Oliviera Robertinho alisema anawapongeza wapinzani wake kwa kutumia vizuri nafasi walizozipata, huku wao licha ya kucheza vizuri lakini hawakuweza kuingia ndani ya boksi mara kwa mara kwa wapinzani wao.

Robertinho alisema wamesahau matokeo hayo na sasa wanajipanga na mchezo wao ujao dhidi ya Vipers kuhakikisha wanatoka na pointi tatu wakiwa ugenini nchini Uganda.

"Wachezaji walikuwa wanaumwa hivyo hata waliporudi bado hawakuwa bora, leo wapinzani wangu wamefunga mabao matatu licha ya sisi kucheza vizuri, Simba ina wachezaji wazuri hivyo tutatengeneza programu nzuri kwa ajili ya mchezo ujao;

"Napenda sana vijana wangu na ninahitaji muda zaidi wa kutengeneza timu kiutimamu wa mwili na mbinu, nimekuwa na mechi mfululizo tangu nifike hapa lakini kila kitu kitakuwa sawa."

Columnist: Mwanaspoti