Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba ina shoo ya kibabe

Simbbaa Pic Kikosi cha Simba SC

Sat, 11 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba leo Jumamosi usiku watatupa karata ya kwanza katika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Horoya ya Guinea mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa General Lansana Conte, jijini Conakry.

Mchezo huo utapigwa kuanzia saa 1:00 usiku na utachezeshwa na refa Amin Mohamed Omar atakayesaidiwa na msaidizi namba moja, Mahmoud Abo El Regal huku Ahmed Hossam Taha akiwa refa msaidizi namba mbili na refa wa akiba akiwa ni Mahmoud El Banna wote wakitokea Misri.

Hii ni bonge la shoo la dakika 90 za kibabe ambazo kama Simba itatoboa itajiweka kwenye nafasi nzuri kwa mechi yao ijayo itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco.

Kikosi cha Simba kilichopo chini ya kocha aliyeifikisha Vipers hatua ya makundi na kupangwa Kundi C sambamba na Wekundu hao wa Wamorocco, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, tayari kimeshafanya maandalizi ya mwisho na jana usiku kilipasha uwanjani hapo tayari kwa vita hiyo.

Licha ya kuwakosa baadhi ya nyota wake akiwamo Saido Ntibazonkiza, Peter Banda, Augustine Okrah, Jonas Mkude na Jimmyson Mwanuke, bado Simba ina nafasi kubwa ya kufanya maajabu ugenini japo haitakuwa na dakika 90 nyepesi mbele ya wenyeji hao.

Historia Guinea

Mchezo dhidi ya Horoya, utakuwa ni wa kwanza kuikutanisha Simba dhidi ya timu ya Guinea katika michuano ya Afrika, kwani kabla ya hapo haikuwahi kuumanana timu yoyote kutoka nchi hiyo ya Afrika ya Magharibi.

Hata hivyo, utakuwa mchezo wa 23 kuikutanisha Simba dhidi ya klabu kutoka Afrika Magharibi katika michuano tofauti Afrika, japo takwimu zimeonyesha imekuwa na unyonge dhidi ya timu kutoka ukanda huo.

Simba imekutana na klabu za Afrika Magharibi mara 22 ambapo imepata ushindi mara sita tu, imetoka sare sita na imepoteza mechi 10.

Katika mechi hizo 22 ambazo Simba imekutana na timu za Afrika Magharibi, imefunga mabao 21 na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 33.

Lolote kutokea

Licha ya kutokuwa na rekodi nzuri kwenye ukanda huo, bado Simba ina nafasi kubwa ya kufanya maajabu kutokana na kuwa na wachezaji wanaotoka ukanda huo, akiwamo Sadio Kanoute, Ismael Sawadogo, Mohammed Ouattara na Pape Ousmane Sakho ambao ni wenyeji wa Afrika Magharibi.

Ni wazi wachezaji hao wanalijua soka la ukanda huo na kwa kushirikiana na nyota wengine wakali wa timu hiyo kama Jean Baleke, Clatous Chama, Henock Inonga, John Bocco na wazoefu wengine wa michuano ya Afrika wataibeba mbele ya Horoya.

Wenyeji hawana rekodi za kutisha msimu huu kwani katika mechi zao tano zilizopita za Ligi Kuu ya Guinea, wameshinda mbili, kupoteza mbili na kuambulia sare moja, huku ushindi mkubwa ukiwa ni Januari 21 ilipoifumua Suquence kwa mabao 4-0, tofauti na Simba ambayo kwenye idadi ya mechi kama hizo, imeshinda zote ikiwamo ushindi wa kishindo wa 7-1 dhidi ya Tanzania Prisons na zilizobaki nyingi ni ule usiopungua mabao matatu kuonyesha ilivyo moto.

Kocha Robertinho anayeshirikiana na Juma Mgunda bila ya shaka leo wataonyesha lile soka lililopewa jina jipya la SambaLoketo mbele ya wenyeji na dakika 90 huenda zikaisha kwa Simba kuanza na moto kwenye mechi za kundi hilo la kibabe.

Deni Morocco

Mara baada ya mechi hiyo ya leo itakayorushwa mubashara kuanzia saa 1:00 usiku, Simba itapaa kurudini nyumbani kwa ajili ya kuiwinda Raja Casablanca ya Morocco itakayovaana nayo wikiendi ijayo jijini Dar es Salaam.

Ushindi kwenye mechi hiyo ijayo dhidi ya Raja Casablanca, utaifanya Simba ifute rasmi unyonge dhidi ya timu za Morocco kila inapokutana nazo kwenye mashindano ya klabu Afrika kwa nyakati tofauti.

Kiujumla Simba imekutana na timu za Morocco mara tatu kwenye mashindano tofauti ambapo kati ya hizo, mara moja imeshinda na mara mbili ilipoteza mechi. Mara ya kwanza kwa Simba kukutana na timu kutoka Morocco ilikuwa ni Mei 28, 2011 ilipokutana na Wydad Casablanca katika mchezo maalum wa mchujo wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ilipoteza kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Petro Sport huko Misri.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) liliamua timu hizo kukutana baada ya Simba kushinda rufaa yake kwa TP Mazembe ambayo ilimtumia kimakosa mchezaji Besala Bokungu.

Mchezo wa pili dhidi ya timu za Morocco ulikuwa ni Februari 27, 2022 ilipochapwa mabao 2-0 na RS Berkane huko Morocco katika mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na ziliporudiana Dar es Salaam, Machi 13,2022, Simba ilishinda bao 1-0 na zote kwenda robo fainali, lakini Wamorocco hao walifika hadi fainali na kubeba ndoo kwa kuifunga Orlando Pirates iliyoizuia Simba isitinge nusu fainali.

Columnist: Mwanaspoti