Nimetazama msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya mechi 28, sijaona ubovu wowote wa Simba. Nimetazama uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, bado Simba inaonekana kuwa timu bora nchini. Ukitazama idara ya ulinzi ya Simba, utagundua hakuna tofauti yoyote kati yao na Yanga.
Simba na Yanga baada ya mechi 28 za Ligi Kuu, kila moja imeruhusu mabao 15. Hakuna tofauti yotote. Ukitazama ubora wa idara ya ushambuliaji, Simba imefunga mabao mengi kuliko Yanga. Kwenye mechi 28, Simba imefunga mabao 66 huku Yanga ikiwa na mabao 56 tu. Simba imekosea wapi tena msimu huu? Binafsi sipati jibu la moja kwa moja, kama unajua ilipokosea naomba unitumie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.
Simba imetoka sare saba msimu huu, ni kosa kubwa sana kutoka sare nyingi kiasi hiki kwa timu inayotaka ubingwa. Kwa namna ilivyokuwa na safu bora ya ushambuliaji, haikutakiwa kutoka sare nyingi kiasi hiki!
Ukiniambia Simba ina timu mbovu, siwezi kukuelewa kabisa. Simba ina wachezaji wazuri, Simba ina timu nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Azam Sports Federation Cup.
Tunapokwenda kwenye dirisha la usajili, viongozi huwa wanafanya maamuzi mengi ya kuwafurahisha tu mashabiki na wanachama wao hata kama hayana tija. Sidhani kama Simba inahitaji wachezaji wengi wapya.
Simba inahitaji wachezaji kama wanne tu kuboresha timu, Simba ina wachezaji wengi ambao kocha anapaswa kuboresha viwango vyao. Pape Ousmane Sakho na Peter Banda bado hawajaishi matarajio ndani ya timu. Ni kazi ya Kocha kuinua viwango vya vijana hawa.
Kama Sakho na Banda wataimarika, ni zaidi ya usajili mpya, ni kweli Simba imekosa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo lakini haina tafsiri ya moja kwa moja kuwa ina timu mbovu.
Namba hazidanganyi, Simba ina safu bora ya ulinzi kwenye ligi yetu. Simba ina safu bora ya ushambuliaji. Sidhani kama inahitaji mabadiliko makubwa, sidhani kama Simba itapaniki na kuongeza watu wengi kikosini.
Simba imepoteza alama nyingi sana kwenye sare saba ilizopata msimu huu lakini bado Mnyama ina timu nzuri. Kuna tofauti kubwa sana kati ya kusajili wachezaji bora na kusajili wachezaji wengi. Simba inahitaji wachezaji bora wasiozidi wanne tu msimu ujao. Simba haihitaji wachezaji 10.
Simba inahitaji kiungo mmoja 'Mtu Kazi' wa chini ili aende kuongeza chaguo kwa Kocha mbele ya Sadio Kanouté na Mzamiru Yassini. Beki mmoja wa kushoto kumsaidia Mohammed Hussein ambaye ametumika sana kwani hata yeye ni binadamu kuna kipindi anachoka sana.
Kwa sababu ziko taarifa za Beno Kakolanya kuondoka, kama ni kweli Simba itahitaji kuleta kipa mwingine wa daraja la juu. Mohamed Ouattara ni beki mzuri sana, sijui kwa nini haaminiki! Simba inabidi iamue, kama inataka kumtumia au wamwache aondoke.
Mchezaji hawezi kuimarika kwa kukaa benchi, kocha ni lazima awape nafasi wachezaji wengi ili kulinda viwango vyao. Pale Yanga hakuna asiyecheza, wote wanacheza tofauti ipo kwenye muda tu. Pale Simba ni kama kocha amekariri hakuna mzunguko mkubwa wa wachezaji, kila siku sura ni zile zile.
Simba sio mbovu kama wengi wanavyodhani, inahitaji nyongeza ya wachezaji wachache sana. Okrah Magic ni fundi kweli kweli anapaswa kuwa kikosi cha kwanza akiwa fiti.
Ukiwa na Okrah kushoto, Kibu Dennis kulia huku nyuma yao kuna Chama na Ntibanzonkiza unahitaji nini tena hapo? Ni kweli Simba imekosa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo lakini Simba haina timu mbovu. Pale Simba kuna timu, ni kazi ya benchi la ufundi kuchanga karata zao vizuri.
Simba ina safu bora ya ulinzi kwenye ligi yetu, ina safu bora ya ushambuliaji kwenye ligi yetu. Imekosaje ubingwa kwa mara ya pili mfululizo? Naomba maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.
Banda na Sakho wanatakiwa kupambana au waondoke kwa umri wao na vipaji, bado hawajaitendea haki jezi ya Simba. Ni kazi ya kocha kupata ubora wa hawa vijana wawili. Moses Phiri na Jean Baleke kama atasalia ni washambuliaji wazuri sana wa kuibeba timu.
Uzuri wa Simba, imejaa viungo wengi wenye uwezo wa kufunga, haishangazi kuona wamewazidi Yanga kwa tofauti ya mabao 10 ya kufunga. Simba haitakiwi kufanya usajili wa wachezaji wengi. Inahitaji wachezaji wachache wenye kuleta mabadiliko kikosini wakizidi sana ni wanne tu.
Tofauti kubwa kati yao na Yanga, wanzao kila mchezaji anayeingia anakuja kuwasha moto kwa sababu wanapata dakika za kucheza. Pale Simba kuna wachezaji wanaocheza na wasotea benchi. Kuna shida ya kuwapa wachezaji wengi uwanjani. Ukiniuliza kwa nini Simba imekosa ubingwa, siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja.
Timu yenye safu bora ya Ulinzi ipo, timu yenye safu bora ya ushambuliaji ipo pia. Kama kuna shida yoyote umeigundua kwenye kikosi cha Simba msimu huu, tafadhali usisite kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.