Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba hii itatia aibu mashindano ya CAF Super Cup

Simba SC Saa 10 Wachezaji wa Simba SC

Mon, 27 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Nimeitizama Simba inavyocheza katika mechi kubwa. Nimeitazama tena na tena. Ukweli ni kwamba Simba iko ‘unga’. Timu imechoka sana.

Simba hii imeshuka sana ubora kulinganisha na ile ya miaka miwili nyuma. Haiko imara katika kushambulia wala kuzuia. Kwenye mechi kubwa za CAF imekuwa kama Mtibwa Sugar au Namungo.

Simba haiko vizuri katika kujenga mashambulizi. Inacheza taratibu. Ni kama vile imepoteza ile nguvu yake iliyokuwepo miaka miwili nyuma.

Haina wachezaji wagumu wa kuamua mechi kama ilivyokuwa wakati wa Luis Miquissone na Meddie Kagere katika ubora wao.

Mastraika wako hoi. Tukianza na John Bocco. Huyu amefanya makubwa sana pale Simba. Alikuwa tishio tangu akiwa Azam FC. Lakini ukweli ulio wazi kwa sasa Bocco yuko dhoofulihali.

Amekuwa straika wa kawaida sana. Pengine kwa sababu amecheza sana. Huu ni mwaka wa 15 anacheza soka la ushindani. Amecheza katika kiwango bora sana. Tunamheshimu kwa hilo.

Lakini kwa sasa Simba haipaswi tena kumtegemea Bocco. Huko ni kukwama. Bocco alipaswa awepo lakini asiwe tegemeo. Ni hapo Simba wanapokosea.

Yule Jean Baleke alikuwa straika mahiri sana pale TP Mazembe, lakini naye bado hajaingia vyema katika mfumo wa Simba. Japo amefunga katika baadhi ya mechi, lakini iko wazi kuwa Baleke siyo Fiston Mayele.

Siyo straika mwenye vitu vingi. Hana kasi kubwa. Siyo mzuri katika kukokota mpira na ndiyo sababu ni ngumu kumuona akifunga bao kama amepokea mpira wakati mbele yake kuna mabeki.

Sasa Simba itamtegemea nani? Ni swali gumu sana kwa sasa. Yule Moses Phiri angeweza kuleta kitu cha tofauti lakini majeraha yamemrudisha nyuma.

Mechi hizi za CAF zinahitaji mshambuliaji msumbufu na anayejua kulazimisha mambo. Ni kama yule Makabi Lilepo wa Al Hilal ya Sudan.

Ni kama vile Kagere katika enzi za ubora wake. Angeweza kuwalazimisha mabeki wa timu pinzani kufanya makosa.

Lakini kwa sasa kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba nani anaweza hivyo? Habibu Kyombo? Kibu Denis? Hapana.

Kyombo bado anahitaji kuendelea kujifunza katika mechi hizi za CAF. Ila Simba ni kama inategemea awe mkombozi. Haiwezekani. Huku ni kukwama.

Saido Ntibazonkiza ni mchezaji mzuri na

mbunifi lakini umri umesonga. Hana kasi kubwa sana na umri umekwenda. Angeweza kuongeza kitu lakini pia siyo tegemeo. Simba ikibanwa huwezi kumuona sana.

Pape Sakho huyu siyo yule wa mwaka jana. Huyu amepoa sana. Anacheza kivivu. Hajitumi sana. Hatari yake mbele ya lango imepungua. Msimu uliopita kwenye mechi hizi za CAF angalau alionyesha kitu cha tofauti.

Majuzi kwenye mechi dhidi ya Azan alikuwa hoi. Wachezaji wenzake

wakalalamika atoke kwani anawategea. Ndipo Simba ilipofikia sasa. Ilihitaji sana ubora wa Sakho.

Yuko wapi Augustine Okrah? Sijui. Huyu alisajiliwa kwa ajili ya mechi hizi za CAF lakini haonekani. Alikuwa ni mchezaji mahiri sana huko alikotoka, lakini hatujui nini kimemtokea pale Simba.

Alipokuja alianza msimu vizuri. Akafunga na kutoa pasi za mabao. Kasi yake ilikuwa mwiba kwa wapinzani.

Nadhani baada ya muda akaanza kuzoea mazingira. Akawa anacheza kivivu kwenye baadhi ya mechezo. Nikasikia viongozi wanalalamika kuwa amekuwa mvivu sana mazoezini.

Ubora wake uwanjani ukapungua sana. Akaanza kuwekwa benchi na sasa hatumuoni kabisa. Yule Peter Banda hakuna cha maana anafanya pale Simba tangu asajiliwe. Majeraha yanamwandama sana. Pengine maisha yake nje ya uwanja yanamfanya aumie mara kwa mara.

Matokeo yake pamoja na kusajiliwa kwa fedha nyingi hakuna alichofanya katika mechi hizi za CAF.

Kwa kikosi cha Simba cha sasa. Kwa uwezo wa huyu kocha Roberto Oliveira na aina yake ya ufundishaji ni wazi kuwa wana wakati mgumu katika kundi lao.

Haijalishi kilichotokea pale Uganda jana dhidi ya Vipers, lakini ukweli ni kwamba Simba haina mechi ya uhakika kushinda. Ni ngumu kusema watamfunga Horoya kwa Mkapa au Raja Casablanca pale Morocco. Ila kwangu hili sio tatizo sana. Inanifikirisha zaidi kwenye mashindano ya CAF Super Cup ambayo wameomba kushiriki. Naona wakienda kutia aibu kubwa huko.

Kwenye

Super Cup kuna wababe wote wa Afrika. Kuna Al Ahly, Wydad Athletic, Raja Casablanca, Mamelodi Sundowns na wengineo. Hizi ni timu za daraja la juu.

Simba itaweza kuwamudu hawa wababe wa soka la Afrika ikiwa na wachezaji hawa? Inafikirisha sana. Naona Simba wakipata aibu kubwa, labda kama watajipanga upya kabla ya Agosti michuano hiyo itakapoanza ikishirikisha klabu nane.

Wamewahi sana kutaka kushiriki mashindano haya. Wangeendelea kuijenga timu kwanza iwe na ushindani mkubwa zaidi. Ila kwa Simba hii mmh. Mtihani mkubwa uko mbele.

Columnist: Mwanaspoti