Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Simba,Yanga zinavyowatesa waamuzi Bongo

Kayoko Pic Data Mwamuzi Ramadhan Kayoko

Sat, 15 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jana katika ripoti yetu juu ya fungia fungia ya waamuzi wa soka nchini, tuliona namna hali ya mambo yalivyo na changamoto zake, huku ikielezwa kuna tatizo kubwa kwenye sheria namba 11 inayosimamia masuala ya wachezaji kuotea (off-side).

Leo tunaendelea kwenye mfululizo wa makala haya tukiangalia waamuzi waliofungiwa hadi sasa na jinsi timu za Simba na Yanga zinavyowatesa waamuzi kila wanapozichezesha mechi zao na tutaangalia kama fungia fungia hiyo inasaidia kuwaimarisha aua inazidi kuongeza tatizo;

WALIOFUNGIWA

Agosti 15 mwaka jana TPLB katika kikao kilichofanyika Arusha kilifanya maboresho ya kanuni mbalimbali ikiwemo ya kudhibiti waamuzi kwa kuwaonya, kuondolewa kwenye ratiba, kufungiwa miezi 3 hadi sita na kwa makosa ya kujirudia au rushwa anafungiwa miaka mitatu, kushushwa daraja na kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi wanaotambulika na TFF.

Msimu ulianza na Wamuzi wa kati wanaochezesha Ligi Kuu wapo 32 waamuzi wasaidizi wapo 42 na wenye beji ya Fifa wapo sita (kati) na waamuzi wa pembeni wapo 10 huku jinsi ya kike yupo, Jonesia Rukyaa na Tatu Maloko (kati), Janeth Balama, Glory Tesha na Zawadi Yusuph.

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassor Amduni anasema; “Hakuna anayependa kuwafungia waamuzi wala kuwasimamisha sababu lengo letu ni kuona ligi inachezwa kwenye mazingira mazuri na kila mmoja azidi kuipenda, watazamaji nao wafurahie na kuifanya ligi yetu kuwa imara na bora zaidi.

“Tumejitahidi kupunguza malalamiko kwa kutoa adhabu japo wengi wanashauri wasifungiwe bali washushwe daraja lakini ukweli ni kwamba hakuna ligi inayohitaji waamuzi wabovu ndio maana tunakuwa wakali na kuchukua hatua haraka,” anasema Amdun.

Miongoni mwa waamuzi ambao wamefungiwa msimu huu ni pamoja na Ahmed Arajiga (Manyara) aliyefungiwa miezi sita kwa kushindwa kutafsiri kanuni katika mchezo wa Azam dhidi ya Yanga na ule wa Tanzania Prisons dhidi ya Simba.

Mwamuzi mwingine ni Amina Kyando aliyechezesha mchezo wa Azam dhidi ya Geita Gold na Namungo dhidi ya Coastal Union huku Ahmed Simba (Kagera) akifungiwa miezi mitatu baada ya kuboronga katika mchezo kati ya Singida na Mbeya City akiwapa penalti Singida ambayo ilikuwa na utata.

Raphael Ikambi (Morogoro) aliyechezesha mchezo wa Yanga dhidi ya Coastal Union aliondolewa kwenye ratiba mizunguko mitatu, Abel William na Ferdinand Chacha wakapewa onyo kwa kushindwa kutunza kumbukumbu za mabadiliko ya wachezaji.

Msimu wa 2018/19 ligi haikuwa na mdhamini mkuu waamuzi wengi walifanya kazi kwa kujitolea wakiahidiwa mambo yatakapokuwa sawa basi watalipwa stahiki zao.

Msimu uliofuata neema ikaanguka kwa kupatikana wadhamini walioweka donge nono. Kilio cha waamuzi kikaongezeka kwani kati ya waamuzi waliochezesha msimu huo hadi sasa kwenye Ligi Kuu wamebaki wachache akiwemo Anoldo Bugando na Charles Simon.

Mfano msimu huo alikuwa, Alex Mahagi, Abdalah Kambuzi, Jimmy Fanuel, Gasper Ketto, Abdalah Uhako, Athuman Senkala, Jacob Adongo na Agness Pantaleo lakini hadi sasa wachache ndio wamebaki.

Abdi aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya waamuzi ambaye kwa sasa ni mkufunzi anasema sio kila kosa mwamuzi anafungiwa sababu kuna makosa mengine yanakuwa bahati mbaya lakini kuna makosa yanafanyika mbele ya mwamuzi na yanakuwa ya kujirudia hivyo tunasema amefanya makusudi.

“Haiwezekani hadi dakika 90 zinamalizika mwamuzi asifanye kosa lolote lakini hatuwezi kuona akifanya kila kosa ambalo litamfanya ashushwe daraja au kufungiwa.

TUJIKUMBUSHE

Julai 24, 2014, aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi alitangaza kuwasimamisha Oden Mbaga na wenzake Jesse Erasmo na Hamis Chang’walu kwa tuhuma za kupanga matokeo, ambazo hazikuwekwa wazi.

Februari 27, 2019 Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) chini ya Mwenyekiti wake Vassilios Skouris ilimfungia maisha Mbaga ambaye alikuwa Katibu wa Chama Cha Waamuzi Tanzania (FRAT) kwa kujihusisha na masuala ya rushwa ya upangaji matokeo.

Baada ya uchunguzi uliofanyika kuanzia Julai 11,2018 Mbaga alikutwa na hatia ya kuhusika kwenye upangaji wa matokeo ikiwa ni kinyume na kanuni za Maadili za Fifa.

Mbaga alitakiwa kulipa faini ya kiasi cha fedha ya Uswisi Faranga 200,000 ndani ya siku 30 tokea apate taarifa hizo na anaweza kulipa kwa fedha ya Swiss au kwa dola za Kimarekani, vilevile Mbaga alitakiwa kulipa gharama za shauri hilo kiasi cha Faranga za Kiswiss 1,000 ndani ya siku 30 tokea amepata taarifa.

Aprili 27, 2016 TFF liliwaondoa waamuzi, Abdallah Kambuzi na wasaidizi wake, Godfrey Msakila na Consolata Lazaro kwenye orodha ya marefa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kwa mechi kwa michezo iliyosalia kufunga msimu.

Hatua hiyo ilikuja siku moja baada ya watatu hao kuboronga katika mchezo wa Ligi Kuu kati ya KMC na Simba iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza wakidaiwa kuwapa Simba penalti mbili za utata ambapo Simba ilishinda mabao 2-1.

Oktoba 27, 2020 Mwamuzi, Shomari Lawi alifungiwa miezi 12 kwa kushindwa kumudu mchezo kati ya Simba na Prisons uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela Oktoba 22.

Novemba, 2022 Florentina Zablon alisimamishwa kuchezesha kwa kushindwa kumudu mchezo kati ya Geita Gold dhidi ya Yanga Uwanja wa CCM Kirumba kwa kutoa penalti iliyozaa maswali mengi.

JE, KUFUNGIA INASAIDIA?

Lawi anasema; “Wenzetu wanafungia miezi mitatu au michezo miwili lakini huku kwetu kwakweli adhabu ni kali kwani inawatia uoga hata wale wanaoendelea kuchezesha akihofia kufungiwa mfano nilifungiwa mwaka, kina Arajiga miezi sita wapo wa miezi miwili na msimu mzima sasa hakuna adhabu kama hizo.”

Abdallah Kambuzi ambaye sasa amegeukia ukocha akimiliki kituo chake cha michezo ‘Kambuzi Sports Center’ kilichopo Shinyanga anasema kwa sasa hafikirii kurudi kwenye uamuzi.

Kambuzi mwenye leseni ya Caf Diploma C anaongeza moja ya vitu ambavyo vilimtoa kwenye uamuzi ni kutokana na changamoto nyingi zilizokuwa zikimsonga na nyingi anaona zilikuwa za kutengenezwa na watu.

“Mpira umegawanyika katika makundi manne nilipoona kwenye urefa kumekuwa pagumu nikaingia kusoma ukocha, hivyo bado natembea kwenye mpira hata kama kwenye uamuzi nimetoka.

Kambuzi anasema haoni kama alifanya kosa katika mchezo wake kati ya KMC dhidi ya Simba ambao mwisho wa siku alifungiwa bali alisimamia ukweli.

“Tatizo lipo kwa uongozi ambao haukutaka kusimamia ukweli na hawawezi kukusaidia sababu wao wanaangalia maslahi yao yabaki kama yalivyo, kiukweli niseme kwamba sijawahi kupata changamoto tofauti na hiyo na kuwafungia waamuzi sio sahihi sababu kuna wengine wanaonewa kama ilivyonitokea mimi.”

SIMBA, YANGA ZINAVYOWAPONZA

Waamuzi wengi wamejikuta matatani hasa wanapozichezesha michezo zinazohusu Yanga na Simba na kwa kuangalia mifano iliyopita wakijikuta wakifungiwa au kupelekwa kwenye kamati ya maadili.

Aprili 16 Simba itakuwa nyumbani kuikaribisha Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu huku zikiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopita uliochezwa Oktoba 23 mwaka jana.

Katika michezo 15 ya mwisho ya michuano mbalimbali zilipokutana, Elly Sasii ndiye mwamuzi aliyehusika zaidi (13) katika mitanange hiyo ya wababe wa soka, akisimama katikati na kuna muda alikuwa mwamuzi wa akiba huku Kayoko akisimama katikati mara nne.

“Kuchezesha dabi sio shida bali presha inakuwa zaidi nje ya uwanja sababu mashabiki, viongozi na vyombo vya habari namna wanavyouchukulia mchezo,” anasema Lawi.

Kambuzi ambaye mchezo wa mwisho kuuchezesha ulikuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wakati Simba ikishinda mabao 2-1 mabao yote ya Simba yakipatikana kwa njia ya penalti Aprili 25,2019 anasema kuna shida mahali.

Lawi ambaye kwa sasa anachezesha Ligi ya Championship mchezo wake wa mwisho kuchezesha Ligi Kuu ilikuwa kati ya Tanzania Prisons iliyoshinda bao 1-0 dhidi ya Simba Uwanja wa Nelson Mandela Oktoba 22, 2020.

Hata hivyo kati ya waamuzi walioonekana kuchezesha zaidi Dabi hizo hadi sasa anayeonekana uwanjani ni Rukyaa na Kayoko huku Arajiga ambaye amemaliza adhabu yake bado haijajulikana atarudishwa lini uwanjani. Hii hapa safu ya waamuzi katika dabi 15 za mwisho.

Columnist: Mwanaspoti